loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa amsifu Magufuli alivyobadili nchi kiuchumi

Majaliwa amsifu Magufuli alivyobadili nchi kiuchumi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais John Magufuli ametoa mwelekeo mpya wa kiuchumi na kiutawala nchini ulioiwezesha Tanzania iingie kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda uliopangwa wa 2025.

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ziendelee kutoa elimu ya uchumi wa viwanda kwa wananchi ili washiriki kikamilifu kujenga na kukuza uchumi wa viwanda.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana katika Ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) jijini hapa alipozindua kitabu cha “The Game Changer: President Magufuli’s First Term in Office”.

Kitabu hicho kimehaririwa na Profesa Ted Maliyamkono na Dk Hugh Mason. Amesema mpangilio na muktadha mzima wa kitabu hicho unabeba dhamira ya kukifanya kuwa kimbilio la rejea kwa watunga sera, wafanya maamuzi, wanataaluma na hata wananchi wa kawaida katika masuala ya maendeleo nchini.

“Kitabu hiki tunachokizindua leo, The Game Changer, kimeonesha namna sera na mipango ya Serikali ya Awamu ya Tano ilivyobadili mwelekeo wa Taifa letu kimaendeleo.

Nitoe rai kwa waandishi wa kitabu hiki, waangalie uwezekano wa kutoa chapisho kwa Kiswahili ili Watanzania wengi waweze kukisoma na kunufaika na maudhui yake,” alisema.

Waziri Mkuu alisema kitabu kimefafanua kuwa Tanzania ni nchi yenye kuendeshwa kidemokrasia na kimeondoa shaka waliyonayo wadau wa maendeleo na wawekezaji kwa lengo la kuwawezesha kuongeza uwekezaji wao nchini.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Balozi John Kijazi alisema, “Kitabu hiki kiwe chachu kwa maprofesa wa vyuo vingine, wakae chini wafanye tafiti na kuandika vitabu vya aina hiyo ili kusaidia kuhifadhi historia ya nchi.”

Alisema vitabu vya aina hiyo vitasaidia vijana kutambua kazi zilizofanywa na viongozi mbalimbali nchini pamoja na kuenzi historia ya nchi. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema kazi ya fasihi andishi ni kutunza kumbukumbu na kitabu hicho kitasaidia kuhakikisha mambo mazuri yaliyofanywa na Rais Magufuli yanadumu kwa vizazi vijavyo.

“Hakika kazi yake imetukuka,” alisema Profesa Ndalichako. Mhariri Mkuu wa kitabu hicho, Profesa Maliyamkono akisoma muhtasari wa kitabu hicho, alisema kimeelezea namna Rais Magufuli alivyoingia madarakani, hali aliyoikuta na hatua alizochukua pamoja na mafanikio ya serikali.

Awali, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akitoa maoni kuhusu utendaji kazi wa Rais Magufuli alisema amefanya mambo mengi katika miaka 20 ya utumishi wake serikalini na miaka mitano ya urais.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka alisema Rais Magufuli ni mwanamageuzi wa kweli na ameipambanua nchi katika miradi mikubwa kama ya ujenzi wa reli ya kisasa inayowawezesha Watanzania kushindana katika uchumi.

Alishauri kuwe na maandiko mengi yahusuyo viongozi.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi