loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM: Dk Mwinyi ameanza vizuri

JPM: Dk Mwinyi ameanza vizuri

RAIS John Magufuli amempongeza Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kuanza kuiongoza Zanzibar vizuri na kusema mwanga wa maendeleo ya visiwa hivyo unaonekana na baada ya muda mfupi itakuwa kama Dubai.

Rais Magufuli pia amempongeza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad kwa kuweka pembeni maslahi binafsi na kukubali kuwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani humo, na ameahidi kuwapa ushirikiano na hatawaacha.

Alitoa kauli hiyo jana mjini Chato wilayani Geita alipokutana na kuzungumza na viongozi hao. Aliwapongeza kwa kufanya sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi wiki hii na kusema Dk Mwinyi ameanza vizuri kuiongoza Zanzibar.

“Niwapongeze kwa sherehe za Mapinduzi ya miaka 57, lakini pia nimpongeze Rais Dk Mwinyi ni kiongozi mzuri hata mapato ya Zanzibar yameanza kupaa. Usiogope kutumbua, tumeanza kuona mwanga wa maendeleo na tunaiona Zanzibar ikiwa kama Dubai,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Maalim Seif amefanya jambo jema kuweka maslahi yake pembeni na kuzingatia maslahi ya Zanzibar kwa kukubali kuwa sehemu ya serikali ya visiwa hivyo na kumuomba ampe ushirikiano Dk Mwinyi.

“Maalim Seif amefanya kazi na baba yake Dk Mwinyi yaani Rais wa Awamu ya Pili (Ali Hassan Mwinyi) na leo anafanya kazi na mtoto wake (Dk Hussein Mwinyi), ana uzoefu mkubwa katika uongozi ninaomba mpe ushirikiano sana,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza, “Uamuzi wa Dk Mwinyi kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni uamuzi wa kishujaa, saa nyingine nchi inashindwa kwenda mbele kwa sababu ya ugomvi baina ya wenyewe kwa wenyewe na maadui zetu walipenda kuona Zanzibar ikichafuka, lakini nyie viongozi hamna nia hiyo, mkafanya lililo jema kwa maslahi ya taifa, ninaahidi sitawaacha kamwe,”

Akitoa mfano, alisema chuki Zanzibar zilivunja hata baadhi ya ndoa ambazo kama mwanandoa mmoja ametoka upande wa Unguja na mwingine Pemba kwenye vurugu za vyama vya siasa ndoa nyingi zilivunjika, lakini sasa zimeungana baada ya maridhiano kufikiwa.

“Ndio, siasa zilivunja hata ndoa, kisa mmoja Mpemba na mwingine Muunguja sababu za kibaguzi tu, lakini baada ya maridhiano ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, leo wote ni wamoja na Rais Dk Hussein anaendelea kuvunja ubaguzi huo, Maalim Seif hakikisha unamsaidia rais wako kurudisha mali za Wazanzibari,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amekubali ombi la Dk Mwinyi la kumuuzia wanyama ili waanzishe eneo la kuwahifadhi kuvutia utalii visiwani humo na kusema sheria inaruhusu hivyo watauziwa kwa bei ya serikali.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Dk Mwinyi na Maalim Seif walimshukuru Rais Magufuli kwa kuwakaribisha nyumbani kwake Chato.

Walieleza kufurahishwa kuzungumza na Rais Magufuli na kwamba mazungumzo hayo yana maslahi makubwa kwa Wazanzibari na Watanzania wote. Katika safari hiyo, Rais Mwinyi alifuatana na mkewe Mariam Mwinyi.

Dk Mwinyi alisema mazungumzo hayo yalilenga kujenga nchi, kuwaunganisha zaidi Wazanzibari na alimshukuru Rais Magufuli kwa dhamira yake ya kuendelea kuisaidia Zanzibar ikiwa ni pamoja na kukubali ombi aliloliwasilisha hivi karibuni kwa Mjumbe wa Baraza la Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje ya China, Wang Yi la kuomba Dola za Marekani milioni 75 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 148 za barabara za Zanzibar.

“Kwa hivyo kwanza nianze kukushukuru wewe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utayari wako, wa kufanya kazi na sisi viongozi wa Zanzibar.

Leo tupo hapa mimi na Maalim Seif Sharif Hamad tukiwa wamoja, tukiwa tunaongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa kule Zanzibar, na nataka niseme haya yasingewezekana kama tusingeungwa mkono nawe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu mara zote umekuwa mstari wa mbele kutaka Zanzibar iwe na umoja,” alisema Dk Mwinyi.

Alisema kwa nafasi yake (Magufuli) ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekuwa akimuunga mkono katika juhudi za kuleta umoja Zanzibar.

“Leo tupo hapa tukiwa wamoja, tukiwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, na nataka nikuhakikishie kwamba sio sisi tu kama viongozi ndio tumeungana, bali Wazanzibari wote wana mwelekeo wa kuungana.

Zile tofauti zetu za kisiasa tumeziweka pembeni, sasa hivi sote tunashirikiana katika kuijenga nchi yetu,” alisema Dk Mwinyi.

Maalim Seif alisema walikuwa na mazungumzo mazuri ya namna ya kuwaunganisha Watanzania wote, na amepata matumaini makubwa kuona Rais Magufuli yupo pamoja nao na ana dhamira ya kuwaunganisha Waunguja na Wapemba.

“Tulikuwa na mazungumzo mazuri, mazungumzo ya kindugu, na mazungumzo ambayo mimi yamenipa matumaini kwamba kiongozi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo pamoja na sisi, hasa katika suala zima la kuimarisha umoja, upendo na maelewano katika visiwa vya Unguja na Pemba.

“Nimefarijika sana kumsikia yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais akituhakikishia kwamba yupo pamoja na sisi na anatuunga mkono kwa hali na mali, kwa hiyo Mheshimiwa Rais nakushukuru sana,” alisema Maalim Seif.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/639f7a16707b5c8bb218148a31819d82.jpg

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameweka jiwe la ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi