loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hatuwezi kuikwepa sekta ya ubunifu katika kukuza uchumi

SEKTA ya ubunifu (sanaa) na uchumi vimekuwa vikiishi pamoja toka karne nyingi. Tunaweza kusema toka binadamu alipoanza kuishi ndio wakati ambao tunaamini sanaa nayo ilianza.

Ilitangulia sanaa na uchumi ukafuata. Uchumi hutua mahali popote penye thamani, na sanaa ina thamani.

Tumekuwa tukilalamika kuhusu changamoto ya ajira na kazi inayowakabili vijana ambao ni kundi kubwa kuliko yote Tanzania. Imethibitishwa kuwa wastani wa umri wa kijana kwa sasa Tanzania ni miaka 17.7.

Ingawa kumekuwapo na kilio cha uhaba wa fursa, vijana wamejiongeza kwa kutumia ubunifu unaowawezesha kutoa huduma mbalimbali kwenye jamii.

Karne hii ya 21 imekuja na changamoto ya kipekee kwani ni ya ulimwengu mzima inayojulikana kama ‘automation of work’ yaani teknolojia na jinsi ilivyoathiri kazi na ajira za watu.

Nafasi nyingi za kazi zimeondolewa kutokana na uwezo wa mashine na teknolojia mbalimbali zilizovumbuliwa kurahisisha uzalishaji wa bidhaa na huduma kwenye viwanda na kampuni.

Ingawa wengine wanaweza kudai Tanzania hatutakiwi kuwa na wasiwasi; ni ukweli usiopingika kuwa kwa dira yetu ya “Tanzania ya Viwanda” na wawekezaji wa kimataifa tunaowapata lazima mashine zitachukua kazi za aina fulani kwani hakuna mwekezaji mwenye uwezo atakayefumbia macho teknolojia ya kisasa inayoweza kumpa ahueni kwenye gharama za uzalishaji kwa kupunguza gharama za nguvu kazi.

Pamoja na teknolojia kurahisisha uzalishaji na kazi nyingi, tafiti zimeonesha kuwa hii ‘automation of work’ inakuja na fursa zake pia, kwani mashine haiwezi kuwa binadamu hata siku moja hata ipewe uwezo kiasi gani.

Kuna ambavyo ‘robots’ hawawezi kufanya vikiwemo kuwa na utu wa kibinadamu ambao unahitajika kwenye kazi zote.

Ubunifu kwa upana wake unaweza kuwa ndiyo mkombozi wa wote, wale ambao wako kwenye mfumo rasmi wa elimu na wale walioishia kuwa mabaki ya mfumo wa elimu.

Miaka kadhaa iliyopita Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa ilitoa ripoti yake inayoonesha ongezeko maradufu la thamani ya biashara ya bidhaa zitokanazo na ubunifu kutoka dola bilioni 208 mwaka 2002 hadi dola bilioni 509 mwaka 2015.

Ripoti hiyo ambayo ni toleo la pili la tathmini ya uchumi utokanao na bidhaa za ubunifu ilizinduliwa huko Geneva, Uswisi ambapo Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inasema kuwa China ndiyo inaongoza kwa kiasi kikubwa katika biashara ya bidhaa za ubunifu inayohusisha ubunifu wa majengo, mitindo ya mavazi na maonesho, usanifu wa ndani ya nyumba na hata sanaa za filamu na vikaragosi.

Mkurugenzi wa kitengo cha biashara ya kimataifa na bidhaa wa UNCTAD, Pamela Coke-Hamilton anasema takwimu hizi ni muhimu kwa namna mbili, “uchumi wa kiubunifu una utajiri wa kibiashara na pia kiutamaduni.

Thamani hizi mbili zinasababisha serikali duniani kote kujikita katika kukuza na kuendeleza uchumi wa kiubunifu kama sehemu ya mikakati ya mabadiliko ya kiuchumi na juhudi za kuhamasisha mafanikio na maisha bora.”

Aidha Coke- Hamilton anasema tasnia ya ubunifu ambayo ni pamoja na usanifu majengo, sanaa na ufundi, masoko na matangazo ya biashara, vyombo vya habari na uchapishaji, utafiti na maendeleo, programu za kompyuta, michezo ya komputa na vingine vya namna hiyo ni msingi wa uchumi wa ubunifu.

“Katika uchumi wa ubunifu, tasnia ya ubunifu inazalisha kipato kupitia biashara na hakimiliki pia inazalisha fursa mpya hususani kwa ajili ya kampuni ndogo na zile za kati,” anaongeza mwanamama Coke- Hamilton.

China ni wasafirishaji wakubwa zaidi wa bidhaa na huduma za ubunifu. Katika mwaka 2002 biashara ya China katika bidhaa za ubunifu ilifikia bilioni 32 za Marekani na kufikia mwaka 2014 kiwango hicho kimekua zaidi ya mara tano na kufikia Dola za Marekani bilioni 191.4.

Cha msingi kama jamii, ni jinsi gani tunawaangalia na kushirikiana na vijana kwa kutumia huduma zao. Kumbuka hata wale ‘manguli’ walianza na kazi moja ikawapa uzoefu, vijana wetu wanahitaji kupewa nafasi.

Fursa nyingine zilizopo sasa ambazo vijana wanaweza kuendelea kutumia ubunifu lakini katika ‘urasmi’ ni utamaduni wa kiuchumi.

Tanzania tumejaliwa kuwa na mtaji wa kiutamaduni mkubwa sana ambao umetuwezesha kuwa kati ya nchi za Kiafrika zinazofanya vizuri kwenye sekta ya utalii.

Sekta hii pia imetajwa kuwa kati ya zile sekta sita zilizoainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo (FYDPII).

Vijana wana uwezo mkubwa sana wa kurasimisha kazi mbalimbali ambazo tayari zipo kwenye sekta hii ikiwa ni chachu ya kuendeleza uchumi wa kiutamaduni.

Kuanzia wachoraji, wabunifu mavazi, filamu na muziki hadi matamasha; vyote hivi ni fursa za ajira na kazi kwa vijana kama tukiviangalia kwa jicho la vyanzo vya ajira.

Filamu na muziki tu vimeonesha jinsi gani vinaweza kutumika kama chanzo cha ajira rasmi kwa vijana wetu hadi kuwaona kwa mfano wanaonufaika na kulipwa kwa kazi zao kuoneshwa mtandao wa Youtube na kwenye chaneli zilizopo kwenye ving’amuzi vya kimataifa.

Uchumi wa kiutamaduni, unaonadi na kuendeleza tunavyovipenda kwenye utamaduni wetu unaweza kuchangia sana kupunguza kilio cha ajira na kazi kwa vijana.

Kilimo cha jembe na hata cha trekta kimeshindwa kuwapata vijana wengi, wengi wanaishia kukimbilia mjini kwa sababu ya urahisi na matabaka na manufaiko ya kazi tuliyojizoesha kama jamii.

Kilimo kama kiini cha uchumi wa Tanzania kinashindwaje kuwa chanzo endelevu chenye maslahi mapana kwa vijana kama nguvu kazi ya taifa? Tunakwama wapi?

Ubunifu, uvumbuzi, ujuzi na maarifa vinajengwa na elimu rasmi na isiyo rasmi. Yatosha kusema kwamba imefika wakati tuache lawama ya upande mmoja na kujiangalia kama jamii na nafasi ya kila mmoja wetu kwenye suala hili.

Tuanze ngazi ya chini kabisa kwenye jamii, ngazi ya kaya kabla hatujafika kwenye mfumo na serikali au sekta ya umma na binafsi.

Wasanii wanao uwezo wa kutengeneza fedha, kwani huutafsiri mzunguko wa sanaa na huchagiza mwamko wa sekta ya viwanda na biashara. 

Kwa kuwa hivi sasa serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli, imejipambanua kuwa ya viwanda, ni wakati muafaka kutafakari kuhusu viwanda vya kazi za sanaa ambavyo havichanui wala kuonekana kwa sababu wasanii hawana fedha.

Mzunguko wake ni mbaya na soko limebanwa. Wizi na ufisadi vimetamalaki. Tusisahau kuwa wasanii/ wabunifu wanapokuwa na fedha ni fursa nzuri kwa wafanyabiashara mbalimbali. Mathalani wenye maduka ya nguo, watauza sana kwa sababu kubadili mwonekano ni sehemu ya sanaa.

Msanii lazima abadili mavazi katika maonesho yake kwa lengo la kujipa heshima na thamani zaidi ya kibiashara. Katika eneo hili, wabunifu wa mavazi ambao nao ni wasanii, hupata kazi zaidi kwa ajili ya kuwapendezesha wenzao katika sanaa tofauti, hususan waigizaji na wanamuziki.

Tusisahau pia kuwa msanii mwenyewe ni ajira. Anapofanikiwa ataajiri watu ili wamsaidie kufanya kazi zake. Kazi zake zinapoingia sokoni, kuna mnyororo mrefu wa mauzo mpaka kumfikia mnunuzi wa mwisho. Hivyo, kila anayehusika katikati ni ajira tosha.

Ndiyo maana inabainishwa kuwa msanii mmoja anaweza kutengeneza ajira za watu mpaka 200.

Kama wasanii 5,000 tu nchini (kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Sanaa la Taifa ya mwaka 2006 kuna wasanii milioni sita) watafanikiwa kufanya vizuri kibiashara, wanaweza kutengeneza ajira za watu 1,000,000 na zaidi.

Wasanii wenye mafanikio hujiongoza wenyewe. Hata bila kutegemea mapromota, wanaweza kuandaa maonesho yenye mafanikio kwa kuwatumia mameneja na maofisa wao. Msanii pia ni kampuni, angalia mfano mdogo tu wa mwanamuziki Diamond Platnumz.

Sekta ya sanaa ikikua inaweza kuchangia pia katika uwekezaji katika viwanda mpaka wa vyuo vya sanaa, hasa pale sanaa inapoonekana inalipa, huongeza hitaji la watu kuisomea kwa undani zaidi fani ili waifanye kwa weledi. Hivyo, uwekezaji wa sanaa unaenda sambamba na kutanuka kwa elimu.

Kwa msingi huo, mafanikio ya wasanii yanaweza kuwa na matokeo makubwa kabisa n ani ukweli kwamba Taasisi ya Sanaa tuliyo nayo sasa (TaSUBa) haitoshi.

Kwa kawaida wasanii wanapofanikiwa hukuza ushindani. Mafanikio ya msanii huendana na idadi ya mashabiki.

Msanii aliyefanikiwa sana (mfano Diamond Platnumz) maana yake anakuwa na wafuasi wengi na hao ndiyo wateja wake. Msanii na shabiki wake ni sawa na mfanyabiashara na mteja wake.

Ukiachana na hoja hiyo, mafanikio ya wasanii yanaweza pia kukuza idadi ya wasomaji kwenye magazeti, kuongeza wasikilizaji redioni na hata watazamaji katika televisheni.

Kwa mfano, shabiki anayempenda msanii fulani, hataacha kusikiliza redio na kutazama runinga inayocheza wimbo wa msanii anayempenda. Pia hataacha kusoma gazeti lililoandika habari ya msanii anayempenda.

0685 666964 au bhiluka@gmail.com

WATANZANIA kama walivyo watu wa mataifa ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi