loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mkataba mnono wa nickel wasainiwa

Mkataba mnono wa nickel wasainiwa

TANZANIA imesaini mkataba na kampuni ya LZ Nickel ya Uingereza kwa ajili ya mradi wa uchimbaji wa madini ya nickel uliopo Kabanga mkoani Kagera, pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchenjulia madini mbalimbali kitakachojengwa Kahama mkoani Shinyanga.

Hafla hiyo ya utiaji saini kati ya Serikali na kampuni hiyo ilifanyika jana mjini Bukoba mkoani Kagera na kushuhudiwa na Rais John Magufuli. Mwenyekiti wa timu ya serikali ya majadiliano ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili yaani serikali na mwekezaji.

Profesa Kabudi alisema maoteo ya awali ya uzalishaji wa madini ya nickel Kabanga utakuwa na wastani wa mauzo yenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya milioni 664 kwa mwaka.

Alisema serikali na kampuni hiyo wamekubaliana kufanya upya mapitio ya upembuzi yakinifu ili kuhakikisha yote waliokubaliana yanaakisi hali halisi lakini pia kuwa na hakika ya pamoja kuhusu kiwango cha madini kilichopo na kazi hiyo itaanza mara moja chini ya Profesa Abdulkarim Mruma.

Sambamba na hilo, alisema Serikali itakuwa na umiliki usiopungua asilimia 16 ya hisa za mradi zisizolipiwa na zisizopungua thamani, hivyo kupata gawio kwenye faida itakayopatikana baada ya kulipa kodi zote stahiki za serikali.

“Mgawanyo wa faida baada ya Serikali na Mwekezaji utakaozingatia mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 na sheria za kodi zilizopo, hivyo kuihakikishia serikali mapato stahiki ya mrahaba, tozo ya ukaguzi, tozo ya huduma, kodi ya mapato, kodi ya zuio kwenye gawio pamoja na kodi nyingine zitakazolipwa na wafanyakazi, wakandarasi na watoa huduma mbalimbali katika mgodi wa Kabanga na kiwanda cha usafishaji madini Kahama,”alisema Profesa Kabudi.

Alisema mapato hayo yakijumlishwa yatavuka asilimia ya faida ya mradi pamoja na fedha ambazo wananchi watazipata. Awali, Profesa Kabudi alisema majadiliano kati ya timu hiyo na mwekezaji huyo yalizingatia maelekezo ya Rais, sheria za nchi na maslahi mapana ya nchi kwa sasa na baadaye.

Alisema utafiti uliofanywa na Serikali ya Tanzania kuanzia mwaka 1976-1979, ulibaini kuwepo kwa madini ya nickel katika mwamba unaoanzia eneo la Msongati nchini Burundi hadi Kabanga ambapo kiasi kikubwa cha nickel kinapatikana Kabanga ni ya daraja la kwanza.

Profesa Kabudi alisema taarifa ya upembuzi yakinifu ya mradi inaonesha kuwa mradi huo utakuwa wa kipindi cha awali cha miaka 33 ya uzalishaji wa nickel kwa ki- wango cha uchakataji wa tani milioni 2.2 za mbale kwa mwaka.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, alisema utiaji saini wa mikataba hiyo, utawezesha kuanzishwa kwa kampuni ya pamoja itakayoitwa Tembo Nickel Corporation ambayo ni kampuni ya ubia na itakuwa na kazi ya kusimamia kampuni mbili ambazo nazo zimeanzishwa baada ya utiaji saini huo.

Kampuni hizo ni pamoja na LZ Nickel Miningi Limited itakayoshughulika na uchimbaji wa nickel Kabanga wilayani Ngara na LZ Nickel Refining Company Limited itakayohusika na ujenzi na uendeshaji wa kiwanda cha kuyeyusha madini mbalimbali kitakachojengwa Kahama.

Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya LZ Nickel Limited, Chris Von Christierson, aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa kampuni yao ina uwezo na uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 40 katika shughuli za uchimbaji madini na kugharamia miradi.

Christierson alisema kampuni yao imewahi kutekeleza miradi ya uchim- baji na usafishaji madini katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Zimbabwe, Ghana, Mauritania pamoja na nchi zingine za Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Australia na Ulaya.

“Mheshimiwa Rais, kutokana na uzoefu huu tulionao, nakuhakikishia kwamba tuna fedha za kutosha na kwa hakika hatutakuangusha, tupo hapa kwa muda mrefu kabisa ili tuweze kufanya kazi kwa manufaa ya Watanzania wote,”alisema.

Baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Madini kuhakikisha mradi huo unaanza kutekelezwa kwa haraka kwa kuwa Watanzania wanataka kuona matunda ya mradi huo kwa kuwa wamechoshwa kusikia michakato ikiendelea.

“Namshukuru Mungu kuona mradi huu kama utaanza mapema, ninaiamini sana timu yangu ya majadiliano ambayo ina wataalamu wa kutosha, nina imani kubwa ni waaminifu na watiifu kwa taifa lao, madini ya nickel yanatumika kutengenezea vitu mbalimbali vikiwemo vifaa vya kielektroniki, kutengenezea vyuma vigumu, bidhaa za kuzuia kutu na hutumika kwenye injini za ndege,”alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli ameendelea kutoa wito kwa wawekezaji wengi kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa ni mahali sahihi, nchi salama, pazuri, kuna upendo na pana utulivu wa kisiasa na madini ya aina zote.

Pia alisema uwekezaji wa Uingereza hapa nchini unafikia Dola za Marekani bilioni 5.4 na kutoa ajira zaidi ya laki mbili kwa Watanzania huku ikitanguliwa na China yenye uwekezaji wa Dola za Marekani bilioni 7.5 na kutoa ajira zaidi ya laki tatu kwa Watanzania.

Balozi wa Uingereza hapa nchini, David Concar, alisema kama ambavyo madini ya chuma yalivyochangia kwa kiasi kikubwa mapinduzi wa viwanda katika karne ya 18, ndivyo ilivyo sasa kwa madini ya nickel na cobalt katika karne ya 21, hivyo mradi huo umekuja kwa wakati na mahali sahihi.

Waziri wa Madini, Doto Biteko, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuikuza sekta ya madini kutoka asilimia tatu hadi asilimia 17.7 ya ukuaji na kuwa sekta ya kwanza kwa ukuaji.

Pia Biteko mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia tatu hadi asilimia 5.2 pia kuwa sekta ya kwanza kuingiza fedha za kigeni hapa nchini.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi