loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wizara yaagizwa kuwasiliana na Hazina deni la bil 22/-

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iwasiliane na Wizara ya Fedha na Mipango ili taasisi za serikali zilipe Sh bilioni 22 wanazodaiwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL).

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso, deni hilo ni hadi Desemba mwaka jana na limetokana na huduma za simu na data. Alisema hayo baada ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari iliyoundwa Desemba 5, mwaka jana kueleza muundo, mipango na majukumu ya wizara na taasisi zake.

“Taasisi za serikali zinazodaiwa na TTCL kiasi cha Sh bilioni 22 hadi Desemba, 2020 zilipe madeni yao kutokana na kutumia huduma walizopewa na TTCL za simu na data,” alisema.

Kakoso alitaka pia wizara hiyo iwasiliane na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuliondolea mzigo Shirika la Posta (TPC) la kulipa pensheni kwa wastaafu waliokuwa wfanyakazi wa Shirika la Posta na Simu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema shirika hilo tangu mwaka 2016 hadi sasa limeshalipa Sh bilioni 10 wastaafu hao. Aidha, aliupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Mamlala ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuendelea kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi na kudhibiti matumizi ya huduma za mawasiliano na vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Pia kamati hiyo ilimpongeza Waziri wa wizara hiyo, Dk Faustine Ndugulile kwa kuanza kuchukua hatua na kushughulikia changamoto na malalamiko ya wananchi wanaotumia vifurushi na bando za simu za mkononi zinazotolewa na kampuni za simu za mkononi.

Pia aliiitaka wizara hiyo kushughulikia mwingiliano wa mawasiliano kwenye maeneo ya mipakani ili wananchi waishio maeneo hayo waweze kupata huduma za mawasiliano bila kuingiliana na nchi jirani.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Zainab Chaula alisema wizara imekutana na kamati hiyo kwa mara ya kwanza na ipo tayari kushirikiana ili kuongeza msukumo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi.

Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba alisema wataendelea kujenga minara ili kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo ya mipakani, yenye milima na miinuko na watatumia teknolojia rahisi kuongeza wigo wa upatikanaji wa mawasiliano nchini.

Mjumbe wa kamati hiyo, Zuberi Kuchauka alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuunda wizara hiyo mpya kwa kuwa dunia imehamia kwenye mitandao, inajikita kwenye uchumi wa kidijitali na Tehama ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuchangia Pato la Taifa.

Kuchauka pia aliitaka wizara hiyo iwekeze kwenye tafiti za Tehama na kuwaendeleza wataalamu wake ili kutumia teknolojia kulinda usalama wa taifa kwenye mtandao.

MKUU wa Mkoa (RC)  wa Mwanza, ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi