loader
Dstv Habarileo  Mobile
‘JPM asiwavumilie wanaomchelewesha’

‘JPM asiwavumilie wanaomchelewesha’

WATU wa kada tofauti wakiwamo wanasiasa, wasomi, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida wameshauri watumishi na watendaji serikalini wasiowajibika kutatua kero za wananchi, wasivumiliwe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili na wengine kupitia majukwaa tofauti ikiwamo mitandao ya kijamii, wamesema watendaji wazembe, wasiojituma, kujisimamia, wasio na ubunifu wanaosubiri amri kutoka juu, wanakwamisha azma ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Kauli hizo za wananchi zimetolewa kutokana na agizo la hivi karibuni liliotolewa na Rais Magufuli kwa viongozi wa halmashauri ya Ubungo na mkoa wa Dar es Salaam akiwataka watatue haraka kero ya ukosefu wa madarasa katika shule ya msingi King’ongo.

Rais alitoa agizo baada ya kuona video fupi iliyorekodiwa na mwananchi mkazi wa King’ongo ikionesha watoto wa shule hiyo wakisomea chini ya mti wakiwa wamekalia mifuko mitupu ya saruji na mabegi yao. Baada ya rais kuagiza na kuahidi kutembelea, viongozi hao wanaendelea na ujenzi wa madarasa, kutengeneza madawati na kuchonga barabara ya Kimara hadi King’ongo.

Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU), Profesa Gaudence Mpangala, aliyesema kitendo cha baadhi ya watendaji serikalini kutowajibika ipasavyo, kinasababisha maendeleo ya nchi kutokwenda kwa kasi na pia wananchi hawahudumiwi kwa kiwango kinachotakiwa.

Profesa Mpangala alisema mtazamo wa baadhi ya watendaji serikalini wa kufanya kazi kwa mazoea, unatokana na utamaduni wa uzembe waliojijengea kwa muda mrefu.

Alisema kuondokana nao itachukua muda licha ya juhudi za Rais Magufuli za kurejesha nidhamu katika utendaji wa umma. “Utaona jambo fulani haliko sawa, lakini baadhi ya watendaji wanaona la kawaida tu na hawaoni haja ya kulishughulikia.

Huku ni kufanya kazi kizembe na kimazoea, hakuna umakini, wanatakiwa kuyaona matatizo na kuyatatua,”alisema Profesa Mpangala. Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda, katika mahojiano na mwandishi wa gazeti hili, alishutumu kutojali kwa baadhi ya watendaji serikali na kufanya kazi kwa mtindo wa ‘bora liende’.

Dk Mbunda alisema ni vyema mamlaka za uteuzi zikawafanyia tathmini mara kwa mara viongozi waliopewa madaraka ya kutumikia wananchi kujiridhisha kama wanatimiza majukumu yao ya kutumikia wananchi inavyopaswa.

“Ukosefu wa ubunifu na kujituma kwa baadhi ya viongozi unaathari kwa kuwa kunaifanya nchi kutopiga hatua ya kimaendeleo kwa haraka, kuna baadhi ya viongozi hawataki kujituma mpaka watumwe,”alisema Dk Mbunda.

Katika mahojiano na mwandishi wa HabariLeo, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padre Dk Charles Kitima, alisema mwendelezo wa watendaji umma kutotekeleza majukumu yao vyema mpaka wapokee amri, kunatokana na tabia ya kushindwa kujitawala katika idara nyingi za umma.

Dk Kitima alisema kumejengeka utamaduni wa watu serikalini kufanya kazi kwa mtindo wa kusubiri wakaguzi jambo ambalo linachelewesha maendeleo na ni kinyume na uadilifu kwa kuwa wanapaswa kujituma hata bila kufuatiliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wanaharakati wa Maendeleo barani Afrika (ForDIA), Bubelwa Kaiza, alisema ili kuondokana na kasumba ya kutowajibika, hakuna budi kuwapo kwa mfumo wa mtu kuwajibika na kuwajibishana.

“Watendaji wengi wanaogopa kufanya jambo kwa kuogopa kuulizwa nani kakutuma au wakati mwingine anaacha kuuliza au kufanya jambo kwa kulinda mshahara wake wa kila mwezi kwa kuogopa kufukuzwa, kwa hiyo hii imekuwa tabia ya Watanzania kwa ujumla kutojituma na tumeibeba mpaka katika maisha ya kazi,”alisema Kaiza.

Aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda, aliliambia gazeti hili kuwa watendaji wa serikali wanapaswa kubadilika kimtazamo kwamba wanapoajiriwa wana uhakika wa kustaafu hata kama hawatekelezaji wajibu wao inavyotakiwa.

Mapunda alitolea mfano masuala ya upungufu wa madarasa, madawati na idadi ya wanafunzi wanaopaswa kujiunga vyuo vikuu kila mwaka kuwa mambo hayo siyo ya dharura bali yanajulikana .

Alisema yalipaswa kushughulikiwa mapema badala ya kusubiri viongozi wa juu wa kitaifa akiwamo Rais Magufuli kuwaelekeza cha kufanya kila wakati. “Mambo mengine wanayofanya baadhi ya watendaji wa serikali ni kumtesa tu Rais bila sababu,” alisema Mapunda.

Alitoa mfano wa viongozi wa Serikali za Mitaa wanaoishi kwenye maeneo yenye changamoto kubwa zinazokabili wananchi na kusema, hawaziibui na kuzifanyia kazi au kuzitolea taarifa kwa mamlaka za juu.

Wakati huo huo katika mitandao ya kijamii, baadhi ya watu walihoji, iweje baada ya video kuhusu wanafunzi waliokaa shule ilizagaa mitandaoni zaidi ya siku nne bila viongozi na watendaji kushituka.

Akiwa mkoani Kagera hivi karibuni, Rais Magufuli alisema katika miaka iliyobaki ya uongozi wake atakuwa mkali kwa wasaidizi wake. Alisema wasaidizi wake wakiwamo mawaziri na wakuu wa mikoa wasiotaka kufanya kazi waache kazi.

Aliwataka wateule wake kujipanga, wasimcheleweshe kwa kusisitiza, “Atakayetaka kunichelewesha atachelewa yeye.”

foto
Mwandishi: Matern Kayera,

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi