loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji madini

Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji madini

MIONGONI mwa mambo muhimu kwa uchumi wa taifa hili kutokana na kusainiwa kwa mkataba wa uchimbaji madini ya nickel yaliyopo Kabanga mkoani Kagera, ni azma ya Serikali na Mwekezaji Kampuni ya LZ Nickel Limited kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji wa madini Afrika Mashariki na Kati.

Kusainiwa kwa mkataba huu, kumetoa fursa ya kuundwa kwa Kampuni ya Ubia ya Tembo Nickel kati ya Serikali na Mwekezaji itakayokuwa na jukumu la kusimamia kampuni zingine mbili ambazo nazo zimezaliwa baada ya kusainiwa kwa mkataba huu mjini Bukoba Januari 19 mwaka huu.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, anazitaja kampuni hizi mbili kuwa ni LZ Nickel Mining Limited ambayo itakuwa na kazi ya kuchimba madini ya nickel pale Kabanga huku Kampuni nyingine ya LZ Nickel Refining Limited itajikita kwenye ujenzi na uendeshaji wa kiwanda cha kuchenjulia madini anuai kitakachojengwa Kahama mkoani Shinyanga.

 

Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya LZ Nickel Limited, Chris von Christierson, ameihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa uzoefu na uwezo wa miaka 40 walionao katika kuchimba, kusafisha madini na kusimamia miradi katika nchi za Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Ghana, Zimbabwe na Mauritania pamoja na nchi za Ulaya, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini na Australia, unatosha katika kuhakikisha uwekezaji katika mradi wa nickel Kabanga unakuwa na manufaa sawa kwa Watanzania na Mwekezaji.

Christierson anabainisha kuwa kampuni yao ina lengo la kujenga kiwanda cha kuchakata madini tofauti na nickel ili kuweza kuchakata madini mbalimbali ya kimkakati hapa nchini na kutoka katika ukanda huu ili Tanzania iwe kitovu cha uchakataji wa madini katika Afrika Mashariki na Kati ili madini yote yaongezwe thamani hapa nchini.

Hii ni hatua kubwa na yenye faida na manufaaa kwa uchumi wa Tanzania na watu wake kwa kuwa ujenzi wa kiwanda hiki utaongeza mapato ya serikali yatokanayo na kodi, utazalisha ajira kwa Watanzania, utasaidia kujengwa na kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara, maji, nishati, utachochea ukuaji wa biashara za ndani na za kimataifa pamoja na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya.

Kwa kuona na kutambua umuhimu wa mradi huu kwa uchumi wa Taifa, ndipo Rais John Magufuli akaikumbusha Wizara ya Madini na wadau wengine wote kuwa katika mradi huu Watanzania wanataka kuona matunda ya mkataba huu na si hadithi za michakato.

“Wananchi wamechoka na michakato kwa kuwa mradi huo umechelewa kutekelezwa tangu mwaka 1976 mimi wakati huo nikiwa mwanafunzi wa kidato cha pili, hakikisheni utekelezaji wake unaanza haraka na msitishwe na maneno ya watu watakaojitokeza kupinga uwekezaji huu,” amesisitiza Rais Magufuli kwa watendaji wake.

Kwa kuwa ujenzi wa uchumi wa taifa lolote ni sawa na kutangaza vita kutokana na upinzani wa kila aina unaoweza kuibuka, Magufuli anasema hata katika utekelezaji wa mradi huu wanaweza kutokea watu wa kuupinga kwa kuwa wapo wengi waliutaka na isitoshe Watanzania wanapaswa kujua kwamba duniani kumejaa wivu wa kibiashara hivyo hata baadhi ya Watanzania wanaweza kutumika kuupinga kama ilivyokuwa kwenye sakata la makinikia.

Ni vizuri kukumbuka kwamba mafanikio haya yote ni matokeo ya uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano mwaka 2017 kufanya mabadiliko katika sheria ya madini pamoja na Sheria Namba 5 na Namba 6 na kuyafanya madini kuwa mali ya Watanzania kwa kuwa madini ni utajiri. 

Rais Magufuli anaweka bayana kuwa madini ya nickel yanatumika kutengeneza vitu mbalimbali vikiwemo vifaa vya kielektroniki, kutengeneza vyuma vigumu, bidhaa za kuzuia kutu na pia hutumika kwenye injini za ndege.

Mbali na kusema kuwa kampuni yao ina uwezo na uzoefu kwa zaidi ya miaka 40 katika sekta ya madini, Makamu Mwenyekiti Christierson, ameihakikishia Serikali ya Tanzania akisema “Kutokana na uzoefu huu tulionao, nakuhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba tuna fedha za kutosha na kwa hakika hatutakuangusha, tupo hapa kwa muda mrefu kabisa ili tuweze kufanya kazi kwa manufaa ya Watanzania wote”.

 

Ili pande zote mbili ziweze kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkataba, Christierson ametaka ushirikiano huu ujikite katika msingi wa uwazi na kuaminiana katika shughuli zote watakazofanya kwa pamoja na kusisitiza kuwa hii ndiyo ahadi yao kwa serikali kama washirika wao katika miradi hii.

“Mradi wa Kabanga utatekelezwe kwa ufanisi, kampuni yetu itatumia teknolojia ya kusafisha madini kwa kuyayeyusha kwa kutumia kemikali na kuyeyusha makinikia ya nickel yaliyopo Kabanga ili kuongeza thamani ya madini, kutengeneza ajira na kuongeza ujuzi kwa wananchi wa Tanzania,” amesisitiza Christierson.

Balozi wa Uingereza hapa nchini, David Concar, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi walioshuhudia utiaji saini wa mkataba huu mkoani Kagera, amesema kwa kuwa yeye na Rais Magufuli wamesoma masomo ya sayansi, hivyo wanaelewa umuhimu wa madini ya nickel na cobalt duniani kwa sasa.

Concar amebainisha kuwa kama ambavyo madini ya chuma yalivyochangia kwa kiasi kikubwa mapinduzi ya viwanda katika karne ya 18, ndivyo ilivyo sasa kwa madini ya nickel na cobalt katika karne ya 21 na kuongeza kuwa mradi huu umekuja kwa wakati na mahali sahihi.

Waziri wa Madini, Doto Biteko, anasema kuwa Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuikuza sekta ya madini kutoka asilimia tatu hadi asilimia 17.7 ya ukuaji na kuwa sekta ya kwanza kwa ukuaji pamoja na mchango wake kwa Pato la Taifa kuongezeka kutoka asilimia tatu hadi asilimia 5.2 pia kuwa sekta ya kwanza kuingiza fedha za kigeni hapa nchini.

Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema maoteo ya awali ya uzalishaji wa madini ya nickel wa Kabanga mkoani Kagera utakuwa na wastani wa mauzo yenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya milioni 664 kwa mwaka.

Katika kuonesha umuhimu wa mradi huu kwa uchumi wa Taifa, Profesa Kabudi anasema kuwa taarifa ya upembuzi yakinifu ya mradi inaonesha kuwa mradi huu utakuwa wa kipindi cha awali cha miaka 33 ya uzalishaji wa nickel kwa kiwango cha uchakataji wa tani milioni 2.2 za mbale (ore) kwa mwaka.

Kampuni ya LZ Nickel Limited ambayo imesajiliwa nchini Uingereza na wamiliki wake kutoka katika nchi hiyo, Marekani na Australia, ilijitokeza kuanzisha mazungumzo na Serikali Julai 21, mwaka jana (2020) ambapo mazungumzo ya awali yalianza Agosti 20, 2020.

Mazungumzo rasmi yalianza Oktoba 20, 2020 kuhusu uendeshaji wa mgodi wa nickel na ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua madini kitakachojengwa Kahama mkoani Shinyanga.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/da8c41c67643de67be57e61735a3e2fb.jpeg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Afrika Mashariki, Kati

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi