loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli kuzindua shamba kubwa la miti

Magufuli kuzindua shamba kubwa la miti

RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kuzindua shamba la miti lenye ukubwa wa hekta 69,000 sawa na kilometa za mraba 690 wilayani Chato mkoani Geita. Shamba hilo ni la pili kwa ukubwa nchini baada ya lile la Sao Hill lililoko Mafinga mkoani Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel, alisema jana kuwa hafla ya uzinduzi inatarajiwa kuanza saa 12 asubuhi katika eneo la Butengo wilayani Chato lilipo shamba hilo. Gabriel alisema shamba hilo linakuwa miongoni mwa mashamba 23 ya serikali yanayosimamiwa na kuendelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Alisema shughuli za upandaji miti katika shamba hilo zilianza mwaka wa fedha 2017/2018.

“Shamba hili limeanzishwa toka sehemu ya eneo la msitu mkubwa wa Hifadhi ya Biharamulo-Kahama uliohifadhiwa mwaka 1954 kwa Tangazo la Serikali Namba 292 na ilifanyiwa marekebisho mwaka 1959 kwa Tangazo la serikali namba 311,” alisema mkuu wa mkoa.

Aliongeza, “Ni vyema tukaelewa, shamba hili linakuwa la pili kwa ukubwa baada ya shamba la miti Sao Hill lililopo Mafinga mkoani Iringa ambalo lilianzishwa mwaka 1936 likiwa na ukubwa wa hekta 135,900 likijumuisha msitu wa asili wenye hekta 47,000 na eneo la upandaji miti takribani hekta 88,000.”

Kwa mujibu wa TFS, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017/2018 (miaka minne iliyopita) shamba hili limepandwa jumla ya miche 7,449,255 kwenye hekta 2,682 (sawa na ekari 6,705).

Mkuu wa mkoa alisema uanzishwaji na uendelezaji wa shamba hilo unaenda sambamba na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhifadhi mazingira na kuinua uchumi na wananchi, hivyo mradi huo mkubwa wa upandaji miti unakusudiwa kuwanufaisha watu kutoka Geita, Kanda ya ziwa na Watanzania kwa ujumla.

“Tunatarajia shamba hili litachangia manufaa mengi kwa mkoa na taifa letu ikiwemo kuhifadhi mazingira na uhifadhi misitu, kuzalisha malighafi ya viwandani kama nguzo, mbao na karatasi, kutoa ajira na kuchagiza shughuli za ufugaji nyuki ili tuweze kuvuna asali ambayo inahitajika sana kwa siku za hivi karibuni,” alisema Gabriel.

Wakati huo huo, Rais Magufuli atakuwwa na ziara ya siku mbili mkoani Shinyanga kuanzia kesho. Mkuu wa mkoa huo, Zainabu Telack alisema jana mjini Kahama kuwa Rais Magufuli atakwenda kuona utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduni (CCM).

Telack alisema katika ziara hiyo, Rais Magufuli ataweka jiwe la msingi la Kiwanda cha Kahama Food Product Limited kinachomilikiwa na mwekezaji mzawa Mhoja Nkwabi, kinachozalisha maji, juisi na soda.

Aidha, alisema Rais Magufuli atakagua jengo la wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama lililojengwa kwa Sh bilioni 3.9 na Mradi wa Maji uliopo Kijiji cha Isaghehe Kagongwa na Isaka na kuwanufaisha wananchi zaidi ya 50,000 uliotumia zaidi ya Sh bilioni 24.

foto
Mwandishi: Yohana Shida, Geita

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi