loader
Dstv Habarileo  Mobile
Waziri wa Afya, watendaji wake mtegoni

Waziri wa Afya, watendaji wake mtegoni

RAIS John Magufuli ametuma ujumbe kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima na watendaji wake akitaka kujua kwa nini dawa hazipatikani hospitalini wakati serikali imeongeza bajeti ya afya.

Aidha, amelitua suala hilo mikononi mwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango huku akitoa siku saba kwa wanaohusika na bajeti ya afya, kuja na majibu ya kumaliza tatizo la upungufu wa mgawo wa dawa katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia, ametoa changamoto kwa wizara hiyo ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuhusu namna ajira za watumishi wapya wa serikali zinavyopangwa nchini.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wilayani Bukombe mkoani Geita akiwa safarini na katika ufunguzi wa majengo mapya na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Masumbwe mkoani humo.

Akiwa Bukombe, Rais alisoma kero za wananchi anazozifahamu kuwa ni uhaba wa maji, kuunganishiwa umeme, changamoto za usafiri pamoja na uhaba wa dawa na vifaa tiba katika hospitali ya wilaya na vituo vya afya na zahanati.

“Nafahamu tumeongeza bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 31 hadi bilioni 270 ndio maana haya malalamiko ya upungufu wa dawa sifahamu yanatokea wapi? Natuma ujumbe kwa Waziri wa Afya, Katibu Mkuu na watendaji kama bajeti tumeongeza kwanini dawa hazipatikani,” alihoji.

Alisema changamoto hiyo ya uhaba wa dawa anaibeba ili akaangalie endapo kama kuna mchwa mahali na kumshughulikia na hivyo kusaidia mambo yaende na watu wapate dawa.

Pia, alisoma ombi la kupata usajili wa zahanati na vituo vya afya vipya ikiwemo kupatiwa watumishi wa afya na kubainisha kuwa mwaka jana serikali iliajiri watumishi wa afya 14,000 na madaktari 1,000.

“Hili nalo tutaliangalia je hawa watumishi wa afya ambao tunaruhusu waajiriwe wanapangwa wapi? Kwa sababu inawezekana tunapanga kuajiri, hawa watumishi wanabaki Dar es Salaam, hawatawanywi kwenye maeneo,” alisema Rais Magufuli.

Alitoa wito kwa Wizara ya Afya na Tamisemi zijipange vizuri katika kuwasambaza watumishi wanaoajiriwa. Kama wameajiriwa 14,000 wako wapi? Hapa Bukombe wameletwa wangapi?

Akifungua kituo hicho cha afya, alisema bajeti ya dawa mkoani Geita kwa mwaka 2015 ilikuwa Sh bilioni 2.35 na mwaka 2020 iliongezeka na kufikia Sh bilioni 2.75.

“Nilijaribu kujiuliza vizuri kama bajeti hiyo imeongezeka kama ilivyoonekana ni sawa na bajeti ya afya nchi nzima ilivyoongezeka kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2015 hadi mwaka 2020 ambako ilifikia Sh bilioni 270 sasa inakuaje dawa hazipatikani, kuna mahali kuna tatizo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema uwiano wa hesabu za kawaida zinaonesha kuwa bajeti hiyo kwa nchi nzima lakini pia mkoani Geita inaongezeko na kuleta utofauti mkubwa.

“Naiachia kwa Wizara ya Tamiseni na Wizara ya Fedha, inawezekana kuna upunjaji wa mgawo wa dawa kwenye maeneo ya mbalimbali. Bajeti ya dawa imeongezeka lakini dawa zinazosambazwa ni chache. Mnaohusika kupanga bajeti ya dawa mkakae ndani ya siku saba, mje na majibu namna ya kuongeza dawa zinazosambazwa kuendana na mgawo wa fedha,” alisisitiza.

Alisema katika miaka mitano iliyopita serikali ilijitahidi kuboresha sekta ya afya, kwa kuongeza idadi ya vituo vya afya 1,797, zahanati 1,198, hospitali za wilaya 102, za mikoa 10, za rufaa tatu.

Pamoja na suala la afya, Rais Magufuli alitoa tahadhari kwa wachimbaji wenye leseni kuheshimu sheria ya ardhi inayomlinda mmiliki wa ardhi na si kukimbilia kuchimba na kuharibu ardhi lakini pia kusababisha migogoro.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi