loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli: Simameni imara

Magufuli: Simameni imara

RAIS John Magufuli amesema kamwe hategemei kutangaza kuwafungia ndani Watanzania kwa sababu ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) unatokana na virusi vya corona.

Badala yake amewataka wasimame imara na wajihadhari kwa kufuata ushauri wa watalaamu wa afya na kujifukiza kwa mitishamba. Pia, Rais Magufuli ametoa tahadhari juu ya matumizi ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo na kusisitiza kuwa sio chanjo zote ni muhimu na zenye faida kwa watumiaji.

Aliyasema hayo Chato mkoani Geita wakati akizindua shamba la miti alilolipa jina la Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, aliloliita shamba la Silayo.

Akizungumza katika hafla hiyo, aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kuchapa kazi na kuwahimiza wakulima kulima kwa kutumia mvua zilizopo ili zitakapoondoka wawe na mavuno mazuri.

“Katika kipindi hiki ambacho kuna magonjwa ya ajabu yanayoibuka kama corona, nchi nyingi wananchi wake watakuwa wamejifungia ndani. Sisi hatutajifungia ndani na hatutegemei kujifungia ndani na wala sitegemei kutangaza hata siku moja kwamba tunajifungia ndani,” alisisitiza.

Alisema anachukua hatua hiyo kwa sababu sababu Mungu yuko hai na ataendelea kuwalinda Watanzania, lakini pia alihimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zingine za kiafya ikiwa ni pamoja na kujifukiza.

“Unajifukizia huku unamuomba Mungu unaswali, unasali huku unapiga zoezi la kufanya kazi, la kulima mahindi na kulima viazi, ili ule vizuri ushibe corona ishindwe kuingia,” alisema Rais Magufuli.

“Mtatishwa sana ndugu zangu Watanzania lakini simameni imara,” aliongeza.

Alieleza kuwa anafahamu kuwa wapo baadhi ya Watanzania wameondoka nchini na kukimbilia maeneo mengine kwenda kuchanjwa na walikochanjwa huko wamerejea nchini na kuleta corona ambayo ni ya ajabu ajabu.

“Simameni imara,” alieleza Rais na kuongeza, “Chanjo hazifai, kama wazungu wangekuwa na uwezo wa kuleta chanjo hata chanjo ya Ukimwi ingekuwa imeshaletwa, hata kifua kikuu kingekuwa kimeshaondoka, hata chanjo ya malaria ingekuwa imeshapatikana na chanjo ya kansa ingeshapatikana.”

Aliwatahadharisha Watanzania na kuwataka wawe waangalifu kwa mambo ya kuletewa, kamwe wasifikirie kuwa wanapendwa sana. “Taifa hili ni tajiri na Afrika ni tajiri kila mmoja anaitamani, tuwe waangalifu,” alieleza.

“Niiombe Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto isiwe inakimbilia mambo ya chanjo chanjo bila yenyewe kujiridhisha. Ipo nchi fulani walichanjwa watoto wake wa kike wenye umri wa miaka 14 wakaambiwa ni kwa ajili ya kuzuia kansa ya kizazi…ilikuja kugundulika ile chanjo ni kwa ajili ya kuwazuia wasizae,” alisema.

Aidha, aliiomba wizara hiyo kutambua kuwa si kila chanjo ni ya maana kwa taifa, si kila chanjo ina faida kwa Watanzania na kusisitiza iwe macho.

“Tuwe waangalifu tutafanyiziwa majaribio ya ajabu yatakayoleta madhara makubwa. Ninaomba tuendelee kusimama na kumuomba Mungu wetu tuendelee kumtanguliza Mungu wetu huku tukichukua tahadhari za kiafya kadri tutakavyokuwa tukiambiwa na watalaamu wetu,” alisema.

Alisema Tanzania imeweza kukaa takribani mwaka mmoja na zaidi bila corona, hivyo endapo wananchi watachukua tahadhari wataweza kuidhibiti.

“Tusitishwe sana na corona Mungu wetu yupo mbele ya shetani na shetani siku zote atashindwa na atalegea katika magonjwa mbalimbali,” alisisitiza.

Aliwaomba Watanzania na hasa Wizara ya Afya ijitahidi sana kuangalia afya za Watanzania bila kuingia kwenye papara ya kuletewa kila jaribio linalofanyika. Kwa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya nchini Mei mwaka jana, Tanzania iliripoti kuwepo kwa watu 509 waliopata maambukizi ya corona, ambao kati yao 21 walifariki na 183 walipona.

Tangu kipindi hicho hakukuwa na mtu yeyote aliyeripotiwa kuwa na maambukizi. Kwa mujibu wa mtandao wa worldometer, hadi jana mchana jumla ya watu milioni 100.9 wamepatwa na maambukizi ya corona duniani, kati yao watu milioni 2.16 walifariki dunia na watu milioni 73 walipona.

Marekani, India na Brazil ni nchi zinazoongoza kwa mujibu wa mtandao huo kwa kuwa na maambukizi ya watu wengi huku nchi kutoka barani Afrika, Afrika Kusini ikishika namba 15 kwa maambukizi.

Kwa jana pekee maambukizi mapya duniani yalifikia 108,967 huku Urusi na Mexico zikiwa na maambukizi mapya ya watu 17,000 na Poland ikiwa ni maambukizi mapya ya watu 6,789.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/517e33cc45e88e4610f736c8d7b2214b.jpg

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameweka jiwe la ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi