loader
Dstv Habarileo  Mobile
…Aagiza utoroshaji magogo kwenda nje udhibitiwe

…Aagiza utoroshaji magogo kwenda nje udhibitiwe

RAIS John Magufuli ameagiza utoroshaji wa magogo kwenda nje na kulipiwa ushuru mdogo kushughulikiwa mara moja, huku akitaka rasilimali hiyo kutumika zaidi nchini kuimarisha sekta ya viwanda badala ya kusafi rishwa nje.

Pia, ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuanza kujiandaa na fursa zitokanazo na mashamba ya miti ikiwemo kuwezesha ujenzi wa viwanda katika maeneo ya mashamba hayo.

Rais Magufuli aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa shamba la miti lenye ukubwa wa hekta 69,756 lililopo wilayani Chato mkoani Geita jana ambalo alilipa jina la Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo ambapo sasa litaitwa Shamba la Miti la Silayo.

“Tusisubiri mpaka wakati wa uvunaji ufike ndipo muanze kuhangaika kutafuta mahali pa kupeleka magogo, ni lazima tuachane na utaratibu wa sasa wa kuuza nje magogo. Bahati mbaya kwenye magogo nako tunalaliwa sana,” alisema Rais Magufuli.

Alimtaka Profesa Silayo kuweka nguvu za kutosha katika udhibiti wa kusafirisha nje magogo. Alisema usafirishaji nje wa magogo pamoja na kuikosesha nchi mapato lakini pia unakosesha Watanzania kupata fursa za ajira.

“Unaposafirisha magogo nje umeshasafirisha pia ajira nje,” alisema. Alisema ni vyema serikali ikajipanga katika siku za mbele kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini ikiwemo misitu zinatumika nchini na kutengeneza vifaa vinavyotokana na misitu ili nchi ipate fedha nyingi zaidi.

Alitoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, halmashauri pamoja na TFS kuwatengenezea mazingira mazuri wafanyabiashara wadogo wanaojihusisha na biashara ya miti na mbao.

“Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya halmashauri zetu kuwasumbua wafanyabiashara hawa wadogo kwa kuwatoza tozo na kodi kubwa, kuwakamata mara kwa mara huku wafanyabiashara wakubwa wakiwa wanawaachia kutorosha mgogo kwenye makontena bila kutozwa kodi ama kubughudhiwa,” alieleza.

Aidha, alitoa wito kwa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na shule za ufundi nchini kuwajengea uwezo vijana wanaojishughulisha na ufundi serelemala kwa kuwapatia ujuzi na mitaji ili wafanye shughuli zao kwa ubora zaidi.

“Mkiwawezesha vijana wetu hatutakuwa tunaagiza samani kutoka nje kama ilivyo sasa, badala yake samani zote zitatengenezwa hapa nchini na hivyo hatutatumia fedha za nje kuagiza bidhaa hizo,” alisema.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli pia aliwataka wananchi kuacha tabia ya kukata na kuchoma miti hovyo kwa kuwa miti na misitu ni muhimu kwa uhai wa viumbe hai wakiwemo binadamu.

“Pia natoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya hifadhi, mwaka jana serikali ilichukua uamuzi mgumu wa kurasimisha vijiji 920 vilivyokuwa vimejengwa ndani ya hifadhi lakini hiyo isitumike kama kigezo cha kuvamia tena hifadhi,” alisema.

Alisema misitu ina faida nyingi zikiwemo za kiuchumi ambapo katika mwaka wa fedha wa 2019/20, sekta ya misitu na nyuki ilichangia asilimia 3.5 kwenye Pato la Taifa ikiwemo kuipatia serikali mapato ya Sh bilioni 130 na kuajiri Watanzania milioni 100.

Alisema miti na misitu ni uhai kwa sababu ina faida pia kwa viumbe hai kama vile kupatikana kwa hewa ya oksijeni, kuondoa hewa chafu, kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi, inawezesha mvua na upepo wa uhakika, utunzaji wa vyanzo vya maji, hutumika kutengeneza dawa ambayo asilimia 80 ya dawa duniani zinatokana na misitu na makazi ya viumbe hai hususani wanyamana na wadudu.

“Kwa kuzingatia hayo, nchi yetu imekuwa ikitoa kipaumbele kikubwa katika uhifadhi wa mazingira kwa ujumla, asilimia 55 ya nchi yetu sawa na hekta milioni 48.1 imefunikwa na uoto wa misitu. Nchi imetenga takribani asilimia 36 ya eneo lake kwa ajili ya shughuli za uhifadhi,” alisema.

Alitaja mgawanyiko wa maeneo hayo ya uhifadhi kuwa unajumuisha misitu ya hifadhi 463, hifadhi za taifa 22, mapori ya akiba 23 na mapori tengefu 14. Akizungumzia historia ya shamba hilo ambalo lilikuwa sehemu ya Msitu wa Biharamulo Kahama, alisema lilianzishwa miaka 54 iliyopita lakini kutokana na kukithiri kwa shughuli za binadamu lilikuwa linatoweka.

“Tangu nikiwa mbunge nimekuwa nikipokea maombi wananchi wakiomba kulima ndani ya pori hilo, lakini pia walikuwa wakikata miti, uchomaji mkaa, ujenzi wa makazi na uchimbaji wa dhahabu. Sikutegemea kama siku moja tutakuta miti mizuri katika shamba hili, mmefanya kazi kubwa hongereni sana,” alisema.

Alisema kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Silayo pamoja na kumbukumbu ya askari wanaolinda rasilimali za hifadhi za misitu na nyuki, shamba hilo linastahili kuitwa ‘Silayo Forest’ kuanzia jana.

“Ifike mahali wanaofanya vizuri wakumbukwe kwa kazi zao. Badala ya kuuitwa Shamba la Miti Chato sasa litaitwa Shamba la Miti Silayo. Ili Watanzania wakukumbuke kwa kazi nzuri uliyofanya. Silayo ameweka alama katika uhifadhi wa miti,” alisisitiza.

Miaka michache iliyoipita shamba hilo lilivamiwa na shughuli za binadamu za kilimo, uchomaji mkaa na makazi ilikuwa ikifanyika lakini walikubali kuondoka na Novemba 2017 kazi ya upandaji miti ikaanza.

Profesa Silayo alisema shamba hilo lilianza kupandwa miti rasmi mwaka 2017 ikiwa ni sehemu ya mashamba ya miti 23, likiwa la pili kwa ukubwa baada ya Shamba la Miti la Sao Hill lililopo mkoani Iringa.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumabaro alisema sekta ya misitu imekuwa na mchango mkubwa nchini ambapo imeingizia nchi takribani Sh bilioni 373, na kwa Halmashauri ya Mafinga pekee yenye shamba la Sao Hill inapata Sh bilioni 1.3 kwa mwaka kama mapato ya ndani.

Akizungumzia shamba la Silayo alisema litakuwa la kwanza kuwa na miti ya asili na miti ya kupandwa ambapo tangu kuanzishwa kwake limetoa ajira 800 na likakamilika kupandwa lote litatoa ajira 30,000 kwa wananchi wanaolizunguka.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi