loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli aagiza shida ya maji iishe

Magufuli aagiza shida ya maji iishe

RAIS John Magufuli ameagiza Wizara ya Maji na watendaji wake, kuhakikisha shida ya maji inamalizwa mapema iwezekanavyo kwenye maeneo yasiyopata huduma hiyo.

Amewataka watendaji hao, kutafuta vyanzo vingine mbadala ikiwamo kukinga maji ya mvua na kuyahifadhi. Alitoa maagizo hayo jana mjini Kahama mkoani Shinganya katika Kijiji cha Isagehe, alipokuwa akizindua Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mji mdogo wa Kagongwa na Isaka mkoani Shinyanga, uliojengwa kwa Sh bilioni 23.1, ambazo ni fedha za ndani na wenye uwezo wa kutoa maji lita milioni tisa kwa siku.

“Nashukuru kwa mradi huu, Wizara ya Maji ,Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu fanyeni kazi, nataka maeneo mengine yote yenye shida ya maji nao wapate maji kwa sabau maji ni uhai. Maeneo yote yenye mito na maeneo yenye madaraja ina maana yanapita maji, yakingeni yahifadhiwe shida ya maji iishe,” alisema.

Rais Magufuli alisema nchi imebarikiwa kuwa na vyanzo mbalimbali vya maji kama mito na maziwa likiwamo Ziwa Victoria. Alisema ni vyema vyanzo hivyo vitumike vizuri kutatua kero za maji kwa wananchi .

Alitaka watendaji hao kuhakikisha miradi ya maji inakamilika na vijiji vinavyoizunguka vinapewa maji. Akizindua mradi huo, Rais Magufuli alisema mahitaji ya maji kwa maeneo mawili ya mradi ni lita milioni 4.6 kwa siku, ambapo eneo la Kagongwa linahitaji maji lita milioni 2.9 kwa siku huku Mji wa Isaka unahitaji maji lita milioni 1.6.

Alisema hali halisi ya sasa ni kwamba maji yanayopatikana ni kidogo, chini ya lita 252,000 ambayo ni sawa na asilimia 6.3 huku mji wa Kagongwa ukipata maji asilimia 3.2 na Isaka unapata maji asilimia tisa.

“Lakini mradi huu ni mkubwa, una uwezo wa kutoa maji lita milioni 9.8 kwa siku sawa na asilimia 213.33 ya mahitaji ya miji hiyo miwili na hivyo kuwa na ziada ya asilimia 113 na tumeamua mradi huu uhudumie pia vijiji vingine 22 vyenye watu 63,000”,alisema Rais Magufuli.

Alisema mradi huo utahudumia watu 115,660 wakiwemo 55,100 wa Mji wa Kagongwa na 21,650 wa Isaka. Alisema kuwa mbali ya mradi huo, ipo miradi mingine mingi inayotekelezwa lengo ni kumaliza kero ya maji kwa wananchi.

Alitaja baadhi ya miradi inayotelekezwa mkoani Shinganya ni wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (Ruwasa),yenye miradi 12 inayohudumia vijiji 19 vikiwamo vya Ntunze, Bugangi, Duku, ambayo inagharimu Sh bilioni 26.98 Mradi mwingine ni wa ubia baina ya serikali na mgodi Bulyahulu, unaohudumia vijiji 14 vikiwamo vya Mwakitolyo na Kitwana.

“Ni imani yangu kuwa miradi hii na mingine mingi ikikamilika, itatoa huduma kwa wananchi na ninataka miradi hiyo itoe maji sitaki miradi ya kichefuchefu wala hewa”,alisema Rais Magufuli.

Awali, Meneja Mradi wa Maji wa Kagongwa na Isaka, Felista Lyimo alisema mradi huo ni miongoni mwa miradi kutoka Ziwa Victoria na kuwa katika makutano ya Kinaga mkoani Shinyanga ndipo mradi huo umeanzia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Antony Sanga alisema changamoto kubwa ya mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine nchini ni uhaba wa maji safi na salama na kuwa mwa maeneo hayo walikuwa wakipata maji chini ya asilimia 10.

Alisema mradi huo umetokana na ahadi ya Rais Magufuli aliyotoa kwenye kampeni za urais mwaka 2015 baada ya kusikiliza kero za wananchi hao na kuahidi mradi wa maji kujengwa.

Utekelezaji wa mradi huo ulianza kwa kusainiwa Julai 2017 na umejengwa kwa miezi 24. Kuanzia mwaka 2016 serikali imetekeleza zaidi ya miradi ya maji 1,423 yenye thamani ya Sh trilioni 1.2 katika miji 28 nchini.

Miradi hiyo imeongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama vijijini na mjini. Huduma ya maji safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi asilimia 70 mwaka jana kwa maeneo ya vijijini. Kwa mijini imeongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi