loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wizara ya Maji ilinitesa kwa miaka 5 - JPM

Wizara ya Maji ilinitesa kwa miaka 5 - JPM

RAIS John Magufuli amesema Wizara ya Maji ndiyo wizara iliyomtesa kwa miaka mitano iliyopita, ikiwa na miradi mingi ya maji isiyokamilika kwa kipindi kirefu na kutaka watendaji kuwajibika kabla hajawawajibisha.

Alisema hata miradi iliyokamilika, haikuzidi asilimia 30, hali ambayo ameshauri wizara kuzungumza na Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB) kwa kutumia Sheria Namba 17 ya mwaka 1997, iwafute wakandarasi wa hovyo kwenye miradi ya maji wasipate kazi popote nchi- ni na hata Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema hayo jana mjini Kahama wakati kuzindua Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mji mdogo wa Kagongwa na Isaka mkoani Shinyanga, uliogharimu Sh bilioni 23.1 utakaonufaisha zaidi wa watu 115,000.

Rais Magufuli alisema katika miaka hiyo mitano iliyopita, miradi ya maji haikukamilika huku wakandarasi wengi wa maji waliweka gharama kubwa na utekelezaji wa miradi hiyo ulikuwa ni wizi.

“Acha niseme wazi , katika wizara zilizonitesa miaka mitano iliyopita ni hii wizara ya maji, miradi haikamiliki, hata ile iliyokamilika haizidi asilimia 30 na mingi ya gharama kubwa, imewekwa vitu vya ajabu na wizi, nashukuru mmeanza kuchukua hatua kwa wakandarasi feki, wa kule Mwanga(Kilimanjaro ) umewafukuza, ungechelewa ningekufukuza wewe, endelea kufanya kazi na kuchukua hatua,’’ alisema Rais Magufuli.

Alisema anataka kuona miradi yote ya maji ambayo haijakamilika ikikamilika. Alimtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na watendaji wake kutimiza wajibu wao na kuhakikisha miradi inakamilika mapema hata kabla ya muda na kusiwe na gharama za ziada ya mradi.

“Watanzania wamechoka kusubiri, nataka miradi ikamilike na sitaki mradi uzae gharama za ziada au mradi ndani ya mradi, nakusisitiza miradi hiyo ikamilike na iondoa adha kwa wananchi kwa sababu maji ni uhai na hakuna mbadala,” alisema.

Akizungumzia hatua alizochokuwa na Waziri Aweso kwa baadhi ya wakandarasi wa maji kwenye miradi mbalimbali nchini, Rais Magufuli alimpongeza kuwafukuza na kusema moto alioanzisha auendeleze na kamwe asicheke nao.

“Umeanza vizuri hongera sana,moto ulioanza nao endelea nao, usicheke na hawa wakandarasi kamwe, cheka wakati unakunywa maji, halafu zungumzeni na Bodi ya Makandarasi ili kupitia Sheria Namba 17 ya mwaka 1997, wafutwe, wasipate kazi popote Tanzania, kwa vile tuna ushirikiano ndani ya EAC pelekeni majina yao, hatuhitaji watu wa ovyo nchi hii, tunataka ukipewa pesa fanya kazi,” alisisitiza Rais Magufuli.

Alimuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Naibu Katibu Mkuu kuangalia jinsi ya kutafuta wakandarasi washauri wa kizalendo miradi ya maji inayobuniwa ionekane na maji yatoke badala ya kuwa miradi hewa.

“Nataka maeneo mengi yenye shida yapate maji, Katibu Mkuu na Naibu wako tafuteni wakandarasi washauri wa kizalendo ili kila mradi uanzishwapo uwe na matokeo yaani maji yaonekane kwa wahusika.

Awali, akimkaribisha Rais kuzungumza na wananchi katika uzinduzi huo, Waziri wa Maji, Aweso alisema jumla ya miradi 2,450 inatekelezwa nchini na kati ya hiyo, 1,423 imetekelezwa miaka mitano iliyopita. Awesso alisema wameshaainisha miradi yote isiyokamilina na kuweka mikakati ya kuikamilisha.

“Tumeshabainisha miradi isiyokamilika, tumeiita miradi kichefuchefu, tumeweka mikakati ya kuikamilisha”,alisema Aweso.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi