loader
Majaliwa atoa miezi 2 uboreshaji vitambulisho wamachinga

Majaliwa atoa miezi 2 uboreshaji vitambulisho wamachinga

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa miezi miwili kwa Serikali Mtandao, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Chama cha Wenye Benki nchini kuhakikisha wanatengeneza mfumo utakaotumiwa na wamachinga kuomba vitambulisho vya biashara.

Alitoa agizo hilo juzi Dar es Salaam kwenye Kongamano la Mashauriano kati yake na wamachinga kutoka mikoa yote nchini.

Katika kongamano hilo, serikali na wamachinga walikubaliana vitambulisho hivyo viboreshwe kwa kuweka taarifa zote muhimu za mfanyabiashara husika ikiwamo picha, alama za vidole na kitambulisho kisomeke kwenye mifumo mingine ya kiserikali.

Waziri Mkuu alizitaka mamlaka hizo kukamilisha mfumo huo utakaosaidia wamachinga kuomba kitambulisho kwa njia ya mtandao kwa kujaza taarifa zake muhimu zitakazohitajika.

Alisema kisha taarifa hizo zithibitishwe na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kabla ya kukabidhiwa kitambulisho.

“Mkurugenzi wa Serikali Mtandao, Naibu Kamishna wa TRA, Mwenyekiti wa wenye mabenki kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Shirikisho la Machinga nchini, nawapa miezi miwili kukamilisha mfumo huu wa vitambulisho …vianze kutolewa Aprili Mosi mwaka huu,” alisema.

Aliziagiza halmashauri na manispaa zote nchini kutowabughudhi wamachinga katika kipindi hiki cha miezi miwili wanachosubiri vitambulisho vyao. Waziri mkuu pia alisema serikali kwa kushirikiana na Bunge iatahakikisha Shirikisho la Machinga linatambulika kisheria.

Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kushirikiana na uongozi wa muda wa Shirikisho la Machinga kuunda uongozi imara wa shirikisho la machinga ngazi ya wilaya, mikoa na kisha taifa.

“Undeni shirikisho imara na muwe na takwimu ya idadi yenu. Kukosekana kwa takwimu hizi kunasababisha ugumu wa kutengeneza vitambulisho, kuwa na mawasiliano thabiti kati ya serikali na machinga, pia inakuwa vigumu kuwapatia mikopo siyo tu ya benki lakini hata ile ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri zetu kwa kuwa hatujui tunampa nani, yuko wapi na anafanya nini,” alisema Majaliwa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde, alisema kuwa kigezo cha kwanza cha kumpatia mmachinga mkopo wa asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ni kitambulisho cha ujasiriamali au umachinga. Silinde alisema Tamisemi pia itatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wamachinga watakaokuwa na vitambulishoi kuwajengea uwezo wa kufanya biashara kisasa.

“Pia tutalifanyia kazi suala la machinga kusumbuliwa na mgambo na tutakuwa na mikutano ya mara kwa mara isiyopungua mitatu kwa mwaka katika ngazi ya halmashauri,” alisema Silinde.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema asilimia 56 ya nguvu kazi nchini ni vijana na wengi wao ni machinga.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndungulile, alisema kwa kuwa machinga wengi wanapitisha fedha zao na kuhifadhi katika mitandao ya simu, hivyo serikali inawahakikishia usalama wa fedha hizo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0dc5a8b9dcda4305f58eadae5460224e.jpg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi