loader
Simba, yajipima kwa Mazembe

Simba, yajipima kwa Mazembe

SIMBA leo inatarajia kucheza na TP Mazembe katika mchezo wa michuano ya Simba Super Cup katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes akiwaeleza mashabiki waende kwa wingi kwa ajili ya kupata raha ya mwisho ya michuano hiyo.

Gomes ambaye ataiongoza Simba kwa mara ya pili tangu atue kukinoa kikosi hicho alisema hautakuwa mchezo mwepesi, lakini anaamini kikosi chake kitafanya vizuri kwa namna walivyocheza katika mechi dhidi ya El Hilal.

“Kutakuwa na mabadiliko ya kikosi kwenye mchezo wa kesho (leo) sababu nataka kuwaona wachezaji wengine,” alisema Gomes.

“Nashukuru uwepo wa michuano hii, nimeona wachezaji wengi na kuna wengine waliingia kipindi cha pili katika mechi ya Al Hilal na walicheza vizuri.

“Kwa hiyo nahitaji kuwaona wengine, michuano hii imekuwa mizuri na kufahamiana na timu kabla ya mechi za Klabu Bingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa pili.

Niwasihi mashabiki wawepo uwanjani kwa ajili ya timu yao, nimevutiwa na uhudhuriaji wao kwenye mechi zilizopita, naamini pia kesho (leo) watakuwepo,” alisema Gomes.

Naye nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein, alikiri kuwa kikosi chao kimejiandaa na anaamini mechi hiyo itakuwa ngumu, lakini mashabiki wa Simba watafurahi.

“Mechi hii ni kubwa na TP Mazembe wanafahamika kuwa ni wazuri lakini na sisi tumejiandaa kwa kujua hii mechi ina faida kwetu katika maandalizi ya Caf lakini pia ni kipimo kikubwa kwetu.

“Nawaomba mashabiki waje kwa wingi kama ilivyo kawaida yao, tunawahitaji kwa ajili ya kushuhudia timu yao ikicheza soka la kuvutia kama ilivyo kawaida yetu,” alisema Mohamed

Mechi hiyo ambayo itamtangaza bingwa wa michuano hiyo iliyoshirikisha timu tatu (Simba, Mazembe, Al Hilal) pia Simba watahitaji kulipa kisasi cha kutolewa katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1 msimu wa 2018-19.

Katika michuano hiyo, Simba ilianza kwa kuifunga Al Hilal kwa mabao 4-1, kabla ya Hilal nao kuifunga TP Mazembe mabao 2-1 hivyo leo Simba wanamaliza na wanahitaji kushinda ili kujihakikishia ubingwa.

Kocha wa TP Mazembe, Felix Mwamba alisema michuano hiyo ina faida kwao kwa ajili ya maandalizi ya hatua ya makundi ya klabu bingwa, ambapo wao wamepangwa Kundi B pamoja na Mamelod, Al Hilal na CR Belouizdad ya Algeria.

Simba wenyewe wako Kundi A pamoja na Al Ahly ya Misri, AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Al Merrikh ya Sudan.

 “Jana (juzi) tulipoteza lakini haimaanishi kwamba sisi ni wabaya, kesho ni mchezo mwingine na hatutacheza kama jana itakuwa na mfumo mwingine. Tunajua tulipo na tupo tayari kwa mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Simba. Mtegemee mabadiliko ya kikosi,” alisema Mwamba.

 “Wachezaji wote wa Simba ni wazuri, hawategemei mchezaji mmoja, wanacheza kama timu. Kama nikipewa nafasi ya kuchukua mchezaji mmoja kutoka Simba nitamchukua Bwalya,” aliongeza Mwamba.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema mgeni atakuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa na burudani itatolewa na Tudaman na Zuchu anayefanya vizuri kwa sasa.

Manara aliwasihi mashabiki kujitokeza kwa wingi zaidi kwa ajili ya kuendeleza rekodi ya kujaza uwanja katika michezo yao ya nyumbani na kupata raha hizo zote, ambazo wameandaliwa mashabiki wa Simba na wapenzi wa soka kwa ujumla.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e9b99cb4126d53f4efdcfab03f77f43c.jpg

ZAIDI ya Vijana 25,000 kutoka ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi