loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM asisitiza Kiswahili kortini, ampandisha Jaji kwa kutumia lugha hiyo

JPM asisitiza Kiswahili kortini, ampandisha Jaji kwa kutumia lugha hiyo

RAIS John Magufuli amekipigia chapuo Kiswahili na kutaka kitumike mahakamani kwani lugha inayotumika ya Kingereza inawanyima haki wananchi.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo katika maadhimisho ya Sheria Tanzania na miaka 100 ya Mahakama Kuu, kaulimbiu ikiwa ‘Mchango wa Mahakama katika kujenga nchi, amani na ustawi ‘.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwenye viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Alisema  wakati umefika wa kuweka mikakati Kiswahili kitumike kwenye masuala ya kimahakama na kisheria kwa kuzingatia ukweli kwamba hiyo ni moja ya lugha kubwa duniani.

“Wewe hapa Jaji Mkuu umezungumza tena Kiswahili sanifu kweli kizuri kuliko changu cha Kisukuma lakini ukienda kuhukumu kule unaandika Kingereza, hicho Kiswahili unachokitumia hapa kimepotelea wapi. Hii ni challenge (changamoto) kubwa, ni lazima tubadilike, ni lazima tukipende kilicho chetu,” alisema Rais Magufuli.

 Mkuu huyo wa nchi ameongeza kuwa kushindwa kutumia Kiswahili katika shughuli za kimahakama na kisheria: "Sio tu tunawanyima haki wananchi bali pia kuwaongezea gharama kupitia ukalimani kwa kutafsiri hukumu na mienendo ya kesi.”

Rais Magufuli alisema, Kiswahili kinatumika kwenye mikutano ya Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hivyo haoni sababu kwa nini Mahakama haitaki kuitumia lugha hiyo.

“Mimi nilipoingia madarakani na kuanza kutoa hotuba zangu kwa Kiswahili niliambiwa sijui Kiingereza, wala sikujali, huyu hajui Kiingereza, kana kwamba kujua Kingereza ndio maana yake kusoma ” alisema.

Hata hivyo, Rais alimpongeza Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Zephrine Galeba kwa ujasiri alioonesha kwa kuandika hukumu kwa Kiswahili na akasema mtumishi huyo ni shujaa.

Kutoka na ujasiri huo,  Rais amempandisha cheo na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Alisema Jaji huyo alitoa hukumu hiyo kwenye kesi kati ya mgodi wa dhahabu wa North Mara dhidi ya Gerald Zumbi katika kesi ya mapitio namba 23 ya mwaka 2020.

Jaji Galeba aliapishwa Januari 29,  2019 kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi