loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM: Mahakama msione aibu kutumia Kiswahili

JPM: Mahakama msione aibu kutumia Kiswahili

RAIS John Magufuli amesema kuandika hukumu kwa Kiswahili si dhambi hivyo Mahakama isione aibu kuitumia lugha hiyo kwenye ngazi zote.

Alisema wakati umefika wa kuweka mikakati Kiswahili kitumike kwenye masuala ya kimahakama na kisheria kwa kuzingatia ukweli kwamba hiyo ni moja ya lugha kubwa duniani.

|Alitoa msimamo huo jana Chinangali jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria sanjari ya maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu Tanzania.

“Wewe hapa Jaji Mkuu umezungumza tena Kiswahili sanifu kweli kizuri kuliko changu cha Kisukuma lakini ukienda kuhukumu kule unaandika Kingereza, hicho Kiswahili unachokitumia hapa kimepotelea wapi.

Hii ni challenge (changamoto) kubwa, ni lazima tubadilike, ni lazima tukipende kilicho chetu”alisema Rais Magufuli. Alisema kutoa hukumu kwa Kingereza ni kutengeneza kero kwa wananchi, ni kushindwa kuutumia uzalendo na kutia dosari kwenye uhuru wa Watanzania.

“Kushindwa kutumia lugha hii kwenye masuala ya kimahakama na kisheria sio tu tunawanyima haki wananchi bali pia kuwaongezea gharama kupitia ukalimani kwa kutafsiri hukumu na mienendo ya kesi”alisema.

Rais Magufuli alisema, Kiswahili kinatumika kwenye mikutano ya Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hivyo haoni sababu kwa nini Mahakama haitaki kuitumia lugha hiyo.

“Mimi nilipoingia madarakani na kuanza kutoa hotuba zangu kwa Kiswahili niliambiwa sijui Kingereza, wala sikujali, huyu hajui Kingereza, kana kwamba kujua Kingereza ndio maana yake kusoma”alisema.

Alimpongeza Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Zephrine Galeba, kwa ujasiri alioonesha kwa kuandika hukumu kwa Kiswahili na akasema mtumishi huyo ni shujaa na amempandisha cheo hivyo anakuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Alisema Jaji huyo alitoa hukumu hiyo kwenye kesi kati ya mgodi wa dhahabu wa North Mara dhidi ya Gerald Zumbi katika kesi ya mapitio namba 23 ya mwaka 2020.

“Huyu amekuwa mzalendo wa kwanza kuandika kwa lugha ya Kiswahili. Tunamuenzi Baba wa Taifa kwa kuanzisha Mahakama, kwa kuanzisha chuo kikuu, lakini Baba wa Taifa ndiye aliyeanzisha Kiswahili… hukumu zenu mnazitoa kwa Kingereza…huyu ni shujaa wa Kiswahili katika Mahakama.

Mnajua na ninyi katika Mahakama mpo very rigid (hamtaki kubadilika)”alisema Rais Magufuli. Alisema Jaji huyo ameonesha uzalendo wa kitanzania kwa kukwepa miiko iliyomo ndani ya Mahakama kwa kuandika hukumu kwa Kiswahili.

“Huyu ameamua, na kwa sababu ameamua kuenzi lugha ya Kiswahili mimi leo ninampandisha cheo kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa”alisema Rais Magufuli.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi