loader
Dstv Habarileo  Mobile
Rais ataka dhamana, adhabu mbadala kupunguza msongamano

Rais ataka dhamana, adhabu mbadala kupunguza msongamano

RAIS John Magufuli amewataka majaji na mahakimu wasaidie kupunguza mlundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani kwa kutoa dhamana na adhabu mbadala inapobidi.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha Wiki ya Sheria iliyoadhimishwa sambamba na maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu Tanzania.

Alisema pamoja na kasi ya kusikiliza mashauri, bado kuna changamoto zinazoendelea kuukabili mfumo wa utoaji haki ukiwemo mlundikano wa afungwa na mahabusu magerezani “Magereza hapa nchini yana uwezo wa kuwahudumia wafungwa na mahabusi 29,902 lakini waliopo magerenzani ni takribani ya wafungwa na mahabusu 33,000.

Idadi hiyo imepungua baada ya serikali kuwasamehe na kuwapunguzia vifungo wafungwa zaidi ya 40,000, kwa hiyo tungekuwa na wafungwa na mahabusi 73,000”alisema Magufuli katika maadhimisho hayo ikiwa ni mwanzo wa mwaka mpya wa Mahakama.

Alisema idadi hiyo pia ilipungua baada ya ofisi ya mashitaka kuendelea na ukaguzi wa magereza na vituo vya polisi na kuwafutia kesi mahabusi 4,799 katika kipindi cha miaka mitano “Kuna wakati magereza yalikuwa na wafungwa zaidi ya 38,000, hivyo naunga mkono rai ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa waheshimiwa majaji na mahakimu kutoa dhamana na adhabu mbadala kila inapostahili.

Hii si tu itapunguza rudikano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza bali pia itaipunguzia serikali mzigo wa kuwahudumia wafungwa.”alisema Rais Magufuli.

Wakati huo huo Rais Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya wahakikishe kamati za maadili za maofisa wa mahakama zinakutana na apewe ripoti ya vikao vitakavyofanyika mwezi huu.

“Nimesikia kwamba kamati za maadili za maofisa wa Mahakama wa mikoa na wilaya ambazo kisheria zinaongozwa na Ma-RC na Ma-DC hazikutani, wamepewa madaraka ili kushughulikia masuala ya maadili hawakutani hivyo kushindwa kuchukua hatua kwa watumishi wenye makosa”alisema Rais Magufuli.

Alisema wakuu wa mikoa na wilaya wana wajibu wa kusimamia kamati hizo lakini wamekuwa hawafanyi hivyo. “Hivyo nawaagiza wakuu wa mikoa na wilaya wote kuhakikisha kamati za maadili zinakutana na mwezi huu wa pili nataka nipate ripoti kuwa wamekutana mara ngapi maana unaweza kulaumu huku kumbe walipewa madaraka ya kusimamia wamekaa kimya,”alisema Magufuli.

Pia aliipongeza Mahakama kwa kuwachukulia hatua watumishi 19 kwa kwenda kinyume na maadili ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi watumishi tisa, kuwaonya tisa na kumshusha cheo mmoja.

Alikemea vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watumishi wachache katika vyombo vya utoaji haki, na kusisitiza wachukuliwe hatua ili wasichafue na kukwamisha haki za wananchi.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Bunge litajitahidi kuhakikisha kwamba ndani na nje ya Bunge muhimili wa Mahakama unaheshimiwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alimuomba Rais Magufuli kabla hajamaliza awamu yake ya pili ya uongozi amalizie kiporo cha Katiba pendekezwa yenye maoni ya wananchi.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alimweleza Prof. Lipumba kuwaambia upinzani kuwa waache mchezo wao wa kukimbia bungeni.

“Kawaambie mchezo wa kutoka kwenye bunge waache na mwaka huu 2021 wawe wazalendo na masuala ya kitaifa waache mambo ya kutoka hovyo nje,”alisema.

Alisisitiza kuwa vyama vya siasa nchini vina imani na mahakama na ndio maana mara nyingi hukimbilia mahakamani pindi maamuzi yanapotolewa na ofisi yake na kuwataka kufanya hivyo lakini si kwa lengo la kwenda kujaza kesi bila sababu.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi