loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kiswahili chanukia mahakamani

Kiswahili chanukia mahakamani

RAIS John Magufuli ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria, isimamie kuhakikisha Mahakama za juu zinatumia lugha ya Kiswahili kutoa hukumu.

Aliyasema hayo jana katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, baada ya kumuapisha Jaji Zephrine Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Rais Magufuli juzi alimteua Jaji Galeba kushika madaraka hayo, kutokana na ujasiri wake kuandika hukumu kwa Kiswahili wakati akiwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma.

“Kama AG (Mwanasheria Mkuu) anatoka wizara hiyo ya Sheria na Katiba mnashindwa nini kufanya ammendments (mabadiliko ya sheria). AG kila siku anakwenda kufanya ammendment ya sheria za wizara nyingine za wizara inayomhusu hafanyi,”alisema Magufuli.

Alisema kwa utaratibu wa sasa ukiacha Mahakama za mwanzo, mienendo ya kesi na hukumu katika Mahakama za juu, huandikwa kwa lugha ya Kingereza, hivyo kwa maoni yake Mahakama inashiriki kuwanyima haki wananchi na kuwaongezea gharama.

“Mheshimiwa Jaji Mkuu Watanzania watakuheshimu kwa historia. Umefanya mambo mengi lakini hili nalo limalizie. Mheshimiwa Jaji Kiongozi na waheshimiwa majaji, ndugu zangu wananchi wanalia kwa hukumu ambazo hawawezi wakazisoma. Kutafsiri tu kwenyewe lazima walipe pesa. Tunatengeneza mateso na machozi kwa wananchi wengi, muwaonee huruma Watanzania” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema Watanzania waone fahari, kutumia lugha yao na atafurahi sana Mahakama za juu zitaanza kutoa hukumu kwa Kiswahili, kwa kuwa itapunguza mateso kwa wananchi wasiofahamu lugha ya Kingereza.

“Nitafurahi moyo wangu nitakapoona watu wanapata hukumu kwa lugha ya Kiswahili…kwa hiyo kalisimamie hili (Waziri Mwigulu Nchemba) utakuwa umeweka historia lakini itakuwa historia ya pekee kwa Mheshimiwa Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na kwa uongozi wa Mahakama, lakini itakuwa sifa ya pekee kwa waheshimiwa majaji wa rufaa na majaji wa Mahakama kuu na mahakimu na watendaji wote wa Mahakama kwamba mmefanya a final reform kwa kuhakikisha Kiswahili kilichoenziwa na Baba wa Taifa kinatumika kwa wananchi wake”alisema.

Aliwataka wanaohusika kufanya mabadiliko ya sheria zinazoagiza Mahakama za juu zitumie lugha ya Kingereza, walisimamie hilo ili zibadilishwe hata kwenye Bunge linaloendelea ili hukumu ziandikwe kwa Kiswahili. Magufuli alisema Kiswahili ni lugha kubwa yenye misamiati ya kutosha, kuweza kutumiwa na Mahakama na kuna kamusi ya sheria inayoweza kutumika mahakamani na kwenye shughuli nyingine za kisheria.

“Kamusi ya sheria ipo tangu mwaka 1999 na ina kurasa nyingi tu, imeandikwa maneno ya Kingereza na maneno ya Kiswahili. Sasa kwa hiyo kusema kwa Kiswahili hakina misamiati ya kutosha sio sahihi…tunashindwa kutumia Kiswahili kwa sababu ya kukosa utashi na ujasiri”alisema. Magufuli alisema amemteua Jaji Galeba ili awe chachu ya kutumika Kiswahili kwenye Mahakama ya Rufaa Tanzania.

“Basi Mahakama watuhukumu vizuri pia kwa kutumia Kiswahili, ile mimi nitafarijika sana. Nitafurahi sana siku moja hata niende mahakamani kusikiliza kesi ya mtu mwingine ambayo hainihusu mimi na hukumu yake itoke kwa Kiswahili.Mtakuwa mmefanya mapinduzi makubwa”alisema.

Awali Waziri wa Katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba, alisema kuna sheria inayoeelekeza kuwa lugha ya Mahakama ni Kingereza na wamezungumza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali awaongoze kuibadilisha. Alisema, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, alimweleza kuwa hana pingamizi kuibadilisha sheria hiyo, lakini kwa sasa Mahakama inazingatia sheria iliyopo.

Profesa Juma alisema lugha inaweza kuzuia mtu asipate haki na kwa kuzingatia agizo la Rais Magufuli kuwa Kiswahili kitumike kwenye ngazi zote za Mahakama, ukweli ni kwamba bado nyaraka nyingi zimeandikwa kwa Kingereza, hivyo hawawezi kutekeleza kwa haraka.

Alisema, majaji wamepewa kanuni wazitafsiri na baada ya miezi miwili au mitatu, watakuwa na kanuni zaidi ya 50 kwa lugha ya Kiswahili ili wakati wa kesi mahakamani ubishi usiwe kwenye tafsiri ya lugha.

“Kwa hiyo kwa upande wetu Mahakama majaji wameipokea, wameikubali, wameanza kutafsiri hizo sheria na ningeomba tu upande wa wizara wawahusishe wananasheria wa serikali, isifanyike katika ngazi ya sera tu, wale mawakili ambao tunakutana nao mahakamani wahusike ndio wawe mstari wa mbele…”alisema Profesa Juma.

Wakati huohuo Wizara ya Katiba na Sheria imemkera Rais Magufuli kwa kutoajiri wafanyakazi 200 kwa kuwa alishatoa kibali tangu mwaka jana. Rais Magufuli alisema mwaka jana alitoa kibali waajiriwe madaktari 1,000 na waliajiriwa, alitoa kibali waajiriwe walimu 8,000 wakaajiriwa na alitoa kibali Mahakama iajiri watumishi 200 lakini hadi sasa hawajaajiriwa.

Alisema baada ya yeye kuruhusu ajira hizo, wizara hiyo ilipaswa kueleza inahitaji watumishi wa idara zipi na kutangaza nafasi, kwa kuwa Watanzania wengi wanazihitaji.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi