loader
Kaze awatuliza mashabiki Yanga kwa Piston

Kaze awatuliza mashabiki Yanga kwa Piston

KOCHA wa Yanga, Cedric Kaze amewatuliza mashabiki wa Yanga na kuwataka kutokuwa na wasiwasi na kiwango cha mshambuliaji mpya wa kikosi hicho, Fiston Razak kwani anahitaji muda zaidi.

Razak ambaye wengi walitarajia makubwa kutoka kwake katika mchezo wa kirafiki ulimalizika kwa Yanga kufungwa 1-0 dhidi ya African Sports juzi, alishindwa kabisa kuonesha makali yake.

Katika mchezo huo licha ya kucheza dakika 75 kabla ya nafasi yake kuchuliwa na Ditram Nchimbi, alipiga langoni mashuti mawili tu, moja likilenga lango na jingine likitoka nje.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kaze alisema anajua vizuri ubora wa mchezaji huyo na ndio maana alipendekeza kumsajili, lakini aliwataka mashabiki kutompima kwa mchezo huo mmoja na kutaka apewe muda zaidi.

 “Fiston ana muda mrefu hakucheza mpira ni vigumu kuonekana ubora wake kwenye mchezo mmoja nadhani ni hali inayowakuta wachezaji wengi, kikubwa ninachoweza kusema atakuwa msaada mkubwa kwenye eneo la mbele,” alisema Kaze.

Pia Kaze alisema watu wasijadili matokeo yaliyopatikana kwenye mchezo huo wa kirafiki dhidi ya African Sport bali wanatakiwa kuangalia kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake kwani hilo ndilo muhimu zaidi.

 “Wachezaji wangu walikuwa kwenye wiki mbili ngumu za kufanya mazoezi makali na mchezo huu ulikuwa maalum kutengeneza utimamu wa miili yao.”

 “Sioni kama kuna tatizo kwakuwa tumetengeneza nafasi nyingi tulikosa bahati ya kutumia nafasi hizo, lakini kwangu kipimo changu ni kuwaona kama mafundisho niliyowapa wamefanyia kazi.”

“Tulitengeneza nafasi nane za wazi, wachezaji inawezekana walikuwa wamechoka kutokana na mazoezi magumu niliyowapa na naamini hadi kwenye mchezo wa Mbeya City tunaenda kuchukua pointi tatu,” alisema Kaze.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d6e0ef9a2a4925d19d0c1a10247f9b04.jpg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi