loader
Dstv Habarileo  Mobile
…Aagiza watumishi Moro ‘wazitapike’ fedha za soko

…Aagiza watumishi Moro ‘wazitapike’ fedha za soko

RAIS John Magufuli ameagiza wafanyakazi wote wa Manispaa ya Morogoro na taasisi zingine za serikali mkoani humo wanaomiliki vizimba kwenye Soko Kuu la Manispaa na kuwakodisha wananchi kwa Sh 50,000 kwa mwezi, ‘wazitapike’ (wazirejeshe) haraka kama wanataka kuendelea kuwa watumishi wa umma.

 

Alitoa maagizo hayo jana mkoani humo wakati akizindua soko hilo alilolipa jina la Soko la Chifu Kingalu, lilijengwa kwa gharama ya Sh bilioni 17.696. Alisema Chifu Kingalu ni Chifu wa Waluguru ambaye alifanya kazi kubwa ya utunzaji wa mazingira, lakini pia alishiriki harakati za ukombozi.

 

Alisema soko hilo linalochukua wafanyabiashara zaidi ya 2,500, limejengwa kwa gharama kubwa zaidi ikilinganishwa na Soko la Job Ndugai jijini Dodoma lililogharamu Sh bilioni 14.649 na Soko la Kisutu, Dar es Salaam linalogharimu Sh bilioni 13.4.

 

Soko la Chifu Kingalu lina jumla ya fremu 304 na vizimba 900, lakini pia ni miongoni mwa masoko 22 yanayojengwa na serikali kwa jumla ya gharama ya Sh bilioni 361.033 ambayo masoko tisa kati ya hayo yameshakamilika.

 

Rais Magufuli alisema baada ya kufika sokoni hapo alizungumza na wafanyabiashara waliomweleza kero zao ambazo zilimgusa kwa namna ya kipekee na kugundua kuwa mbali na sheria nzuri zilizowekwa na Bunge na serikali, bado sheria zingine zinavunjwa na moja ya sehemu ambako sheria hizo zinavunjwa ni Manispaa ya Morogoro.

 

Alisema katika Bunge lililopita zilipitishwa sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya kuondoa kero kwa wananchi wa kawaida ikiwemo kero ya wakulima, wafugaji na wavuvi. 

 

Alisema kupitia sheria hiyo, tozo zote zilizokuwa kero kwa wananchi zilifutwa.

 

“Sasa nimeshangaa sana na kweli nimeumia sana, mtu anakuja na kiroba chake cha vitunguu, akifika hapa anamkuta mtu wa manispaa anataka kudai pesa ya kuingiza biashara, anadai pesa ya kizimba na zingine, lakini kitu kingine nilichokiona humu kuna watu waliopewa vizimba vyao bila tatizo, lakini wapo wengine waliopewa vizimba kwa kukodishwa na madalali,” alisema Rais Magufuli.

 

Aliongeza, “Na baadhi ya madalali hao ni wafanyakazi wa manispaa, nilipoingia sokoni nilipata ushahidi wa mtu mmoja aliyeniambia kwamba vizimba vinapaswa kulipiwa shilingi 20,000 kwa mwezi, lakini yeye anatozwa na mfanyakazi wa manispaa anaitwa Aika shilingi 50,000 kwa mwezi.”

 

“Sifahamu huyo Aika kama yupo hapa, nimeshatoa maelekezo kama bado huyo Aika anapenda kazi na wafanyakazi wengine wa manispaa kama bado wanapenda kazi, hizo fedha zote walizozichukua za watu waliowakodisha pale wazitapike kuanzia leo,” aliagiza Rais Magufuli.

 

Alisisitiza kuwa wafanyakazi wote wa manispaa wenye vizimba awe mfanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, manispaa na wengine wote, waziteme fedha zote walizozichukua na waachie wananchi wa kawaida ambao watalipia vizimba hivyo kwa gharama ya Sh 20,000 iliyowekwa na manispaa na wasidaiwe kitu kingine tena.

 

“Hili soko limejengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 17 fedha za serikali kwa ajili ya kusaidia wananchi wa maisha ya chini, kwa hiyo sitaki nisikie tena kwamba hili ni agizo la sheria ndogo, sheria ndogo haiwezi kuzidi sheria kubwa. Waziri wa Tamisemi Jafo simamie hili, nataka wale wote waliochukua hela, njia nzuri ya kuwasamehe warudishe fedha hizo, ole wake atakayekiuka agizo hili,” aliagiza Rais Magufuli.

 

Aidha, Rais Magufuli aliwageukia viongozi wa Mkoa wa Morogoro akiwemo Mkuu wa mkoa, Loata Sanare, Mkuu wa Wilaya, Bakari Msulwa, Mkuu waTakukuru, Meya wa Manispaa waruhusu mambo hayo yafanyike wakati wao wapo. Alisema hayo yanayofanyika ni rushwa na kumfanya ajiulize maswali mengi uongozi wa Morogoro ukoje.

 

Kutokana na hali hiyo, aliagiza uozo wote uliopo kwenye soko hilo ukome kuanzia sasa na asilisikie tena kwa kuwa anataka wafanyabiashara wadogo wawe matajiri na kisha akawapa viongozi hao muda wa wiki moja kuzimaliza kero zote sokoni hapo na watoza ushuru waliokuwepo sokoni hapo waondolewe mara moja.

 

“Sitaki raia wasumbuliwe wakati mimi nikiwa Rais,” alisisitiza Rais Magufuli.

 

Kuhusu waendesha bodaboda kutoruhusiwa kufika sokoni hapo, aliagiza bodaboda zianze kwenda sokoni hapo kupeleka wateja kwa kuwa bila wateja soko hilo litakuwa halina maana.

 

Mbali na mambo ya soko hilo, pia alisema kero zote zilizomo kwenye mkoa huo zikiwemo Barabara za Kidatu-Ifakara, Ifakara-Malinyi-Mahenge na Kisaki atazifanyia kazi. Aliwataka wananchi wa Morogoro na nchi nzima kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kulima mazao ya chakula na biashara.

 

Pia aliwataka Watanzania kuendelea kumtumainia Mungu katika hali ya magonjwa ya aina zote kama ilivyokuwa wakati wa ugonjwa wa Covid-19 kwa kuwa Mwenyezi Mungu hashindwi kitu na ataliponya Taifa hili.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi