loader
‘Dawa lishe ya Nimrcaf ilifanya  vyema kwenye corona’

‘Dawa lishe ya Nimrcaf ilifanya vyema kwenye corona’

UTAFITI kwenye kada ya tiba asilia ni muhimu katika kupambana na magonjwa ya aina mbalimbali na hasa ikizingatiwa kwamba tiba hizo ni nafuu kwa upande wa gharama za matibabu na zinaweza kulipunguzia taifa gharama za kutumia pesa za kigeni kuagiza dawa.

Baada ya Rais John Magufuli kutoa tamko kuhusu umuhimu wa kuthamini tiba asili, hususani zinazothibitishwa na Mkemia Mkuu, wataalamu wa tiba asili wameanza kujitokeza kuelezea dawa wanazotafiti kwa ajili ya magonjwa mbalimbali ikiwemo corona (Covid-19).

Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Paul Kazyoba, anasema kiuhalisia ugonjwa wa corona bado hauna dawa na hata chanjo zinazotolewa hazina uhakika.

Kwa msingi huo anasema kuna umuhimu wa kuendelea kuhamasisha matumizi ya tiba asilia kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali kwani hata tiba za kisasa kwa asilimia 70 zinatumia mimea na miti ya asili.

Anasema wanachofanya kwenye tiba za kisasa ni kutoa kemikali za sumu wanapotengeneza dawa hizo.

Dk Kazyoba anasema matumizi ya tiba asili yameonesha mafanikio ikiwa ni pamoja na kutibu dalili zinazoambatana na magonjwa kadhaa ikiwemo corona.

Anasema kuna wataalamu wengi nchini wamekuwa wakijitokeza kutafiti magonjwa ya aina mbalimbali na dawa zao kuonesha mafanikio. Anatolea mfano wa tafiti za dawa nyingi zilizofanywa mara baada ya kulipuka kwa ugonjwa wa corona kwamba zilionesha mafanikio mazuri.

Dk Kazyoba anasema kuanzia Machi mpaka mwisho wa mwezi Mei mwaka jana, wataalamu wengi walifika Nimr na wengine kuwasiliana na taasisi hiyo na kupeleka dawa za kuponya mfumo wa upumuaji ili zifanyiwe utafiti. 

“Wengi walikuja na kupiga simu kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Njombe, Simiyu, Shinyanga na hapa Dar es Salaama walifika ofisini kwangu zaidi ya 15 kwa ajili ya kuleta dawa zao ili zifanyiwe utafiti,” anasema. 

Dk Kazyoba anasema kwa mwenendo huo inaonesha jinsi watafiti wa Tanzania wa tiba asili walivyo tayari pale kunapolipuka ugonjwa fulani. Anasema ndani ya makabila zaidi ya 126 yaliyopo nchini kumekuwa na mitidawa ya aina mbalimbali inayotibu magonjwa mengi.

Anasema dawa nyingi zilizopelekwa kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya kufanya utafiti hususani katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa corona zilitafitiwa na kuonesha zina uwezo wa kutibu dalili za ugonjwa huo na hata magonjwa mengine.

Anabainisha kuwa kwa dawa lishe inayotengenzwa na taasisi hiyo ya NIMRCAF kuanzia April mpaka Juni mwaka jana imeweza kufanyiwa utafiti wa kina na kutumika katika hospitali na watu binafsi.

Anasema katika utafiti wa majaribio, walipanga kuhusisha wagonjwa 50 waliokuwa wamelezwa hospitalini wakisumbuliwa na virusi vya corona lakini walifanya utafiti kwa wagonjwa 21 kutokana na wagonjwa kupungua kipindi hicho. 

Mkurugenzi huyo wa kuratibu na kukuza utafiti anasema waliweza kuwafuatilia wagonjwa hao mpaka mwisho sambamba na wagonjwa wengine waliokuwa wakipatiwa matibabu kwa dawa za kisasa hospitalini.

Anasema matokeo yalionesha kwamba waliotumia Nimrcaf ukubwa wa tatizo ulipungua kwa kiasi kikubwa na haraka ikilinganishwa na wale waliotumia dawa za kisasa.

“Kwa kuwa lengo letu la kupata wagonjwa hamsini halikutimia, tunaeleza kuwa utafiti huu wa awali wa majaribio ulionesha mafanikio makubwa kwa wagonjwa waliotumia dawa yetu,” anasema.

Amabainisha kuwa mbali na dawa hiyo ya Nimrcaf walifanyia tafiti dawa nyingine kama Covidol, Shengena na nyinginezo ambazo zilipelekwa NIMR na baadhi yake kufanyiwa utafiti na kuonesha mafanikio.

Anasema zipo dawa kadhaa za magonjwa mbalimbali ambazo zimefikishwa kwenye taasisi hiyo lakini kutokana na changamoto za fedha bado hazijatafitiwa lakini baadaye wanatarajia kufanyia tafiti na kuzipitisha au kushauri vinginevyo ikionekana hazina ufanisi.

Mkurugenzi huyo anabainisha kuwa si dawa zote za asili hupelekwa NIMR kwani hiyo ni taasisi ya utafiti na kwamba kutokana na kuwapo kwa wataalamu wengi wa tiba asilia zaidi ya 1,000 wanahakikisha ubora wa dawa kwa matumizi ya binadamu kupitia kwa mkemia mkuu.

Anasema wapo wataalamu wa tiba ambao hawajapeleka dawa zao kufanyiwa utafiti na NIMR lakini zimechunguzwa kwa mkemia mkuu na kupewa cheti kinachodhibitisha kuwa hazina kemikali hatarishi kwa afya ya binadamu huku pia zikipata cheti kutoka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kuonesha kwamba ni salama kwa wagonjwa.

“Sisi baada ya kutafiti tunachofanya ni kusajili na kuidhinishwa ubora wa dawa husika kwa matumizi ya ugonjwa tajwa lakini wapo wanaoomba usajili katika baraza la tiba asili na tiba mbadala na zinatoa matokeo bora,” anafafanua. 

Anasema pamoja na kuwepo kwa dharura ya magonjwa kama corona ambayo hayana tiba wala kinga ni vema wataalamu wa dawa za asili wakaendelea kuangalia misingi ya usalama wa dawa zao kabla ya kuzitoa harakaharaka kwa kuwa tu kuna kiu ya upatikanaji wa dawa.

“Kinachotakiwa kwa dawa asili lazima ziwe salama na zenye tija hivyo ni vyema wataalamu wa tiba asili na dawa mbadala wakajitahidi kuandaa dawa kwenye mazingira salama yaliyoothibitishwa na baraza la tiba asili,” anabainisha.

Dk Kazyoba anasema ni vyema pia dawa hizo zikathibitishwa na mkemia mkuu ili kubainisha kama hazina kemikali za sumu zinazoweza kuleta madhara kwa afya za walaji.

Anasema ni vyema pia kwa wataalamu hao wanapotoa dawa kwa mgonjwa lakini wakaona haimpi nafuu kuwaelekeza haraka kwenda hospitali.

“Dawa asili ni jambo jema, lakini kama dalili za ugonjwa haziondoki pale mgonjwa anapotumia dawa si vema kuendelea kumpa dawa hizo hizo bali apelekwe hospitali ili kutumia dawa zote mbili, itasaidia kuleta nafuu,” anasisitiza.

Anawataka wananchi kuwa makini pia na matumizi ya dawa asili za mimea tiba kwani kuna ambazo zina kemikali nyingi zinazoweza kuwa na madhara.

“Unapotumia sasa huoni madhara lakini madhara yanaweza kuonekana miaka mitatu baadaye au hata zaidi baadaye,” anasema.

Anasisitiza kwamba kimsingi tiba asili zinaweza kusaidia katika nyanja mbalimbali na kwamba nyingi zimeonesha mafanikio katika kukabiliana na magonjwa mengi yasiyotibika kwa dawa za kisasa.

Ni kwa kulijua hilo anasema Nimr inaendelea na tafiti nyingi za magonjwa yasiyo na tiba na kwamba baadhi ya tafiti ya dawa za kutibu magonjwa kama ya saratani na selimundu ziko katika hatua mbalimbali.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/7b023f55f767f1566753e084471ecb3f.jpg

SERIKALI hivi karibuni ilitangaza nyongeza ya ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi