loader
Dstv Habarileo  Mobile
…Aagiza wawekezaji watumie nembo za Tanzania

…Aagiza wawekezaji watumie nembo za Tanzania

RAIS John Magufuli amewataka wawekezaji nchini kutumia nembo za Tanzania katika kuzitambulisha bidhaa zao wanazozilisha hapa nchini kwa kuwa jambo hilo ni muhimu katika kujenga uzalendo.

Alisema hayo jana mkoani Morogoro wakati akizindua Kiwanda cha kukoboa mpunga cha Murzal Wilmar.

Rais Magufuli alitoa wito huo baada ya Ofisa Utawala wa kiwanda hicho, Martha David, kutoa maelezo mbalimbali yanayohusu kiwanda chao zikiwemo bidhaa wanazozalisha ambazo zote zilianza kwa jina la ‘Korie.’

Kutokana na hilo, Rais Magufuli aliwataka waone namna ya kutengeneza jina jingine linalohusu Tanzania kwa sababu Tanzania inazalisha vitu vingi kama vile maparachichi yanayozalishwa mkoani Iringa, lakini yanawekwa nembo ya nchi zingine.

“Bidhaa zenu zinaitwa Korie, naomba mwekezaji aangalie kutengeneza jina jingine linalohusu Tanzania kwa sababu Tanzania tunazalisha vitu vingi, kwa mfano maparachichi yanazalishwa Iringa yanawekwa nembo ya nchi zingine, inafaa pawepo na jina linalotangaza Tanzania kwa kuwa itakuwa njia ya kuitangaza nchi yetu. Tuwe na nembo ya Kitanzania ambalo ni jambo muhimu katika kujenga uzalendo, lazima tujivunie uzalendo wetu,” alisema Rais Magufuli.

Hata hivyo, aliwapongeza wawekezaji hao kwa kujenga kiwanda hicho kwa kuwa kilimo na viwanda ni sekta zinazotegemeana. Alisema zaidi asilimia 70-75 ya Watanzania ni wakulima, hivyo viwanda ni silaha pekee ya kuleta mageuzi na kuboresha maisha ya wananchi wengi.

Alisema Tanzania ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya nafaka ukiwemo mpunga na mahindi lakini hayawanufaisha wananchi kwa kushindwa kuyasindika na kuyafungasha vizuri kwa masoko ya ndani na nje, na kuwafnya wasifirishe mpunga badala ya mchele, mahindi badala ya unga uliofungashwa vizuri.

“Nampongeza mwekezaji kwa kujenga kiwanda hiki kwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 20 sawa na zaidi ya Sh bilioni 40. Kiwanda hiki ni kikubwa kuliko vyote nchini na kina uwezo wa kukoboa tani 288 za mpunga kwa siku, kinatoa ajira ya watu 75 za moja kwa moja lakini wanufaika ni wengi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema uwekezaji huo ni muhimu kwa kuwa katika dunia ya leo soko ni jambo kubwa na wakulima watakuwa wamepata soko la uhakika kwa mazao yao. Katika kuwaunga mkono, alinunua mfuko wa kilo 50 wa mchele kwa Sh 90,000 na kutaka apewe risiti kama kaulimbiu inavyosema ukinunua dai risiti.

Aidha, wakati akizindua Kiwanda cha kusafisha na kufungasha mazao jamii ya kunde cha Mahashree kilichopo Mikese, aliwashukuru wawekezaji hao kwa kuiamini Tanzania na kutambua kuwa ni mahali pazuri pa kuwekeza.

Alisema mazao yatakayotoka kwenye kiwanda hicho yanaweza kwenda nchi yoyote duniani kutokana na thamani yake, lakini pia nchi itapata fedha za kigeni na wananchi watapata ajira na mazao yatapata soko.

Ofisa Utawala wa kiwanda hicho, Martha David alisema kilianzishwa mwaka 2016 na uzalishaji ulianza 2019, kina uzoefu wa biashara ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki katika kusindika na kuzalisha mchele.

“Bidhaa zetu zinapatikana Tanzania na Afrika Mashariki. Mwaka wa mazao wa 2020 kampuni ilipokea tani 65,000 za mpunga zenye thamani ya shilingi bilioni 45 ambazo zilizolipwa kwa wakulima,” alisema David.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe alisema wizara yao itafanya kazi ya kuhakikisha ndoto ya Rais ya kuwa na viwanda vingi nchini inatimia.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU mwaka 1974, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alitangaza mpango wa miaka 20 ujenzi wa viwanda Tanzania na ulianza mwaka 1975-1995.

Profesa Kabudi alisema Mwalimu alipanga miaka 20 ya kujenga viwanda na mji alioutenga kujengwa viwanda vikubwa ni morogoro lakini  kila mkoa aliupangia viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Mahashree alisema kiwanda chao kitaingia mikataba na wakulima na ifikapo mwaka 2023 wanatarajia kuwa na mikataba na wakulima 14,000, pia wana malengo ya kuwatumia wataalamu Kitanzania walihitimu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kuboresha uzalishaji kwa kutumia maarifa yao.

“Mheshimiwa Rais tumewekeza Dola milioni 11, uwezo wetu wa kuzalisha ni tani za ujazo 120,000 kwa mwaka. Tuna maabara bora na teknolojia ya kisasa kwa kupima ubora wa bidhaa zetu,” alisema mkurugenzi huyo.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare alisema mkoa una jumla ya viwanda 3,652 vyenye viwango mbalimbali ambapo viwanda vikubwa vipo 25, vya kati 16, vidogo 326, vidogo kabisa 3,285.

Alisema kati ya viwanda hivyo, viwanda 15 vilijengwa na Baba wa Taifa na viwanda 13 kati ya hivyo 15 vimebinafsishwa na viwili vilibaki serikalini kwa maslahi ya nchi, lakini kati ya viwand 13 vilivyobinafsishwa, vinavyofanya kazi ni viwanda sita tu.

Waziri wa Nchi, Ofis ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema kuanzia Jumatatu ijayo mpaka Februari 28, mwaka huu, ameagiza watendaji wote katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, watendaji wa mitaa na vijiji, kupita nyumba kwa nyumba nchi nzima ili kuorodhesha majengo yote isipokuwa taasisi za dini.

Jafo alisema lengo la kampeni hii ni kuhakikisha majengo yote nchini yanalipiwa kodi kwa sababu nchi inataka fedha kwa ajili ya maendeleo.

 

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi