ZANZIBAR imechaguliwa kuwa mwenyeji wa michuano ya Afrika kwa nchi zisizo mwanachama wa Caf na Fifa wa moja kwa moja, Conifa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Zanzibar, ZFF, iliyosainiwa na Rais wake, Seif Kombo Pandu, michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Mei, mwaka huu.
Taarifa hiyo ilisema bingwa wa michuano hiyo atafuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za Conifa 2022.
Michuano hiyo itashirikisha nchi 10 ambazo ni mwenyeji Zanzibar, Barotseland, (Zambia), Matebeleland (Zimbabwe), Sahara ya Magharibi (Western Sahara), Kabylia (Algeria), Yoruba Land (Nigeria), Biafra (Nigeria), Barawa (Somalia), Visiwa vya Chagos (Mauritius) na Lesotho.
Aidha, taarifa hiyo ilisema kupitia michuano hiyo timu zinazoshiriki zitapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
Zanzibar iliwahi kushiriki michuano hiyo mwaka 2012 ilipofanyika Kurdistan, Iraq.