loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wabunge mna kazi ya kubadilisha huu mtazamo potofu

BAADA ya Bunge la 12 kuzinduliwa rasmi Novemba 13, mwaka jana na Rais John Magufuli, ikiwa ni wiki chache baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, mjadala uliibuka mitaani wa hili litakuwa Bunge la aina gani?

Katika uchaguzi huo mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba 28 mwaka jana, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliibuka na ushindi wa asilimia 84.4 na kuzoa zaidi ya asilimia 95 ya wabunge wote.

Kwa hiyo, nchi ikashuhudia Bunge likiwa limetawaliwa na wabunge wa CCM kwa zaidi ya asilimia 95 na likiwa halina kambi rasmi ya upinzani. Kwa kifupi, mbali na idadi ya wabunge wa CCM kuwa kubwa, kamati zote 16 za kudumu za Bunge hilo sasa ziko chini ya CCM.

Baadhi ya Watanzania walidai kwamba Bunge hili litakuwa la 'ndiyo mzee', wakimaanisha kwamba kwa kuwa wabunge wengi ni wa chama tawala, CCM, kinachounda serikali, Bunge litashindwa kuwa na meno ya kuihoji na kuisimamia Serikali ya chama chao ipasavyo.

Wengine walifika mbali kwa kutabiri kwamba huenda bunge hili lisiwe na msisimko na joto kubwa la mijadala mizito ya kuibua ufisadi na maovu mengine nchini.

Hata hivyo, kuna wale walioamini kwamba Bunge hili linaweza kuwa bora zaidi kuliko lenye ya kambi ya upinzani kutokana na ukweli kwamba sasa wabunge watajikita katika kujadili hoja za msingi na zenye mashiko kwa ajili ya manufaa ya nchi na siyo vijembe.

Kwamba katika mabunge yaliyopita tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, tulikuwa tunashuhudi upinzani ukikalia kutafuta hata kwa tochi makosa ya serikali huku wabunge wa CCM wakikaa upande wa kutetea, alimradi kufifisha hoja za upinzani, hata kama zina mashiko.

Yaani lilikuwa Bunge la kupiga siasa baina ya pande mbili na kuoneshana umwamba badala ya kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano kwa ajili ya wananchi wanaowawakilisha kwa kuangalia maslahi mapana ya taifa na siyo ya vyama vyao.

Kama waswahili wanavyosema kwamba wapiganapo mafahali wawili ziumiazo nyasi, katika mabunge yaliyopita, wananchi ndiyo walikuwa wakiumia kwa wawakilishi kukosa umoja linapokuja suala la maslahi ya Kitaifa.

Hivyo wenye mtazamo huu, wamekuwa na imani chanya kwamba Bunge hili la 12 lililomaliza Mkutano wake wa Pili wiki iliyopita, litafanya kazi halisi ya uwakilishi wa wananchi na siyo kutafutana uchawi na kupiga siasa.

Na kwa kweli tumeanza kuona wabunge wakisimama katika hoja zinazowagusa wananchi katika majimbo yao na serikali kulazimika kujichimbia katika kutafuta majibu.

Kwa mfano, katika Mkutano wake wa pili, tumeona wabunge wakihoji matumizi ya kikosi kazi katika kudai kodi na kueleza kuwa hatua hiyo inaweza kuwatisha wafanyabiashara na kufunga biashara.

Hoja hiyo iliibuliwa bungeni Februari 9, mwaka huu na Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, akidai ukusanyaji wa kodi kupitia vikosi kazi unaua biashara na kushauri kazi hiyo ifanywe na wenye taaluma chini ya TRA.

Pia, Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Costantine Kanyasu, alisisitiza ni lazima Wizara ya Fedha na Mipango iwasikilize wananchi kwa sababu inawezekana hawana taarifa sahihi, hivyo biashara zinakufa.

Akihitimisha mjadala kuhusu hoja ya mapendekezo ya mpango wa tatu wa maendeleo ya Taifa wa miaka mitano (2021/22 hadi 2025/26) kwa niaba ya Waziri na Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Waziri wa Katiba na Sheria Mwingulu Nchemba alisema:

"Tuna kipindi tumekipita ambacho kulipa kodi, elimu ya mlipakodi, uhiari na uzalendo ilikuwa jambo kubwa na gumu sana kwa watu watu walio wengi, hasahasa wafanyabiashara wakubwa.

"Nendeni mkafuatilie 'hansadi' (taarifa za Bunge kwenye mikutano iliyopita) fuatilieni hansad muone kilio kikubwa kilikuwa wapi.

“Kilio kikubwa kilikuwa walipakodi hasa wakubwa, hawalipi kodi ipasavyo. Walipakodi waliokuwa wanabeba nchi, ni watumishi wa umma kwa kiwango kikubwa, na walipakodi wadogo wadogo na baadhi yao walipakodi wakubwa waliokuwa waaminifu. Kwa hiyo kuna kiwango kikubwa sana cha ukwepaji wa kodi.

 

"Sasa, hivi jambo linaloanza kujitokeza la kwamba task force ndio zinakusanya na TRA imeacha majukumu yake, ninaomba nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba TRA bado wanaendelea kukusanya mapato wao wenyewe, na pale ambapo inatokea task force inakusanya, kunakuwapo hatua zinazofuatwa.

 

“Kunakuwapo na taarifa kwamba kwa mlipakodi huyu kuna viashiria vya kutokulipa kodi ipasavyo. Baada ya hapo, kunatumwa timu ya kwenda kukagua, timu ya kawaida ambayo ni TRA na wataalamu wao huenda kukagua. Wakishakagua wanaambizana, wanaelekezana kwa mujibu wa sheria."

 

Waziri huyo alisema kuwa kabla ya kikosi kazi kwenda kufanya kazi yake, TRA kwa kutumia sheria zake, hujadiliana na mlipakodi katika yale makadirio, wanakubaliana na wakati mwingine wanatiliana saini.

 

Pamoja na kuanza kuonesha mwelekeo mzuri, Bunge la 12 lina kazi kubwa sana ya kuondoa mitazamo hasi ambayo imejengeka kwa baadhi ya watu huku mitaani ili kutoa imani yake kwa wananchi.

 

Kwa bahati nzuri sana Mwenyekiti wa Chama hicho chenye wabunge wengi kwenye Bunge la 12 ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli aliwaasa sana wabunge wake wa CCM kutetea maeneo yao kwa kutoa changamoto zilizopo kwa nguvu zao zote na kuwachachafya  mawaziri wajibu hoja na sio kuwa waoga.

 

Rais alikuwa analiambia bunge la 12 kwamba wanayo kazi ya ziada kuuaminisha umma kwamba kokote pasipokwenda sawa  wataihoji na kuisimamia ipasavyo serikali.

 

Wabunge ambao wananchi wanajua wanalipwa vizuri, wana dhima kubwa ya kukutana na wapiga kura wao wanaowawakilisha, kusikia kero na kuzifikisha Serikalini kupitia Bunge na kuacha kuzungumzia maslahi yao wenyewe au kutega kwa kutohudhuria vikao vya Bunge.

 

Wana jukumu adhimu la kuchapa kazi kubwa isiyo na mashaka ndani yake na kutoa matokeo makubwa zaidi ikiwezekana kuliko Bunge lolote ndani ya historia ya nchi yetu.

 

Bunge hili lililobezwa linapaswa lisiwe bunge bubu au la 'ndiyo serikali' kwa sababu ya wengi kutika chama kimoja tu. Wabunge wanayo kazi ya kuwaaminisha Watanzania na kuwathibitishia kwa kuhakikisha wanaihoji kweli kweli serikali aina ya maamuzi yake na kujenga hoja zenye manufaa kwa nchi.

Bunge la 12 lina kazi ya ziada kuthibitisha kwa umma waliotoa mamlaka hayo ya kuwawakilisha kwa kuhakikisha kila kero ya Mtanzania inajadiliwa ili kutafutiwa ufumbuzi. Wananchi wanataka kuona hoja na kero zao zinasemewa vilivyo bungeni, Serikali ikibanwa kweli kweli na kutoa majibu ya kero zao namna zitakavyotatuliwa na siyo majibu ya kisiasa ya kufunika kombe ili mwanaharamu apite.

 

Kwa wingi wao, wabunge hawa wa CCM  wanapaswa kutanguliza maslahi ya wananchi wao kwa kuondoa haya makandokando ya hapa na pale kwamba Bunge hili kwa sababu limetawaliwa na chama kimoja tu basi litakuwa la ndiyo tu mzee. Wabunge wanatakiwa kuwa-prove wrong wale wote waliokuwa na msimamo hasi.

 

 

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni 0657475347

“WANANCHI waliopata hati za hakimiliki za kimila baada ...

foto
Mwandishi: Bwanku M Bwanku

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi