loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanzania, EU wasaini mikataba 6 ya bil 308/-

SERIKALI ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) wamesaini mikataba ya miradi sita yenye thamani ya Euro milioni 111.5 sawa na Sh bilioni 308, itakayotekelezwa nchini kwa miaka minne.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa EU nchini Tanzania, Manfredo Fanti kwa niaba ya Umoja huo, walisaini mikataba hiyo jana jijini Dodoma ukiwa ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya pande mbili, ulioanza miaka 45 iliyopita.

James alisema msaada huo wa EU kupitia Mpango wa Ushirikiano wa 11 chini ya Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya (EDF), umezingatia mahitaji na changamoto zilizoanishwa katika Mipango ya  Maendeleo wa Taifa hasa Mpango wa Pili wa Maendeleo (2016/17-2020/21 na Mpango wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA II).

Alisema tangu ulipoanza ushirikiano baina ya EU na nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP) mwaka 1975, Tanzania imepokea kutoka EU Euro milioni 2,394 sawa na Sh trilioni 6.6 za msaada na Euro milioni 270.9 sawa na Sh bilioni 748.2 za mikopo ya masharti nafuu kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB).

"Fedha hizi zinazotolewa zimekuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya uchumi, uboreshaji wa sera, miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, nishati, kilimo, mazingra na mabadiliko ya tabianchi," alisema James.

Alisema miradi hiyo sita ni wa kuboresha sekta ya nishati wa Euro milioni 35 sawa na Sh bilioni 96.6 na wa matumizi endelevu ya nishati ya kupikia wa Euro milioni 30 sawa na Sh bilioni 82.8.

"Miradi mwingine ni wa kusaidia mnyororo wa thamani katika ufugaji wa nyuki wa Euro milioni 10 sawa na shilingi bilioni 27.6, wa kuboresha huduma ya afya ya mimea nchini ili kuongeza usalama wa chakula wa Euro milioni 10 sawa na shilingi bilioni 27.6, wa kusaidia kuboresha mazingira ya biashara, ukuaji na ubunifu wa Euro milioni 23 sawa na shilingi bilioni 63.5 na wa ushirikiano wa kitaalumu awamu ya pili wa Euro milioni 3.5 sawa na shilingi bilioni 9.7," alisema James.

Alisema mradi wa kuboresha sekta ya nishati, unalenga kuendeleza sekta hiyo kwa kuboresha utoaji huduma na thamani ya huduma kwa wateja wa Tanesco, pia kuanzisha kanzidata ya masuala ya nishati kwa ajili ya mipango na uamuzi, upatikanaji wa nishati safi, mazingira mazuri ya biashara na kuboreshwa kwa sera ya nishati ili kuleta tija na ufanisi na kuimarisha maarifa na uchambuzi wa taaarifa. 

Alisema, mradi wa matumizi endelevu ya nishati ya kupikia, unakusudia kusaidia uzalishaji endelevu wa nishati itokanayo na miti, kuboresha matumizi ya bora ya nishati hiyo na kuongeza matumizi ya nishati ya kisasa bora kwa maeneo ya mijini.

James alisema mradi wa kusaidia mnyororo wa thamani katika ufugaji nyuki  unakusudia kuimarisha mchango wa sekta ya ufugaji nyuki katika kukuza uchumi na kusaidia kuharakisha upatikanaji wa asali wenye ubora inayozalishwa katika mazingira mazuri ili kuchochea soko la asali inayozalishwa nchini.

Alisema,lengo la mradi wa kuboredha huduma ya afya ya mimea nchini ni kuongeza usalama wa chakula, na kuongeza upatikanaji wa mazao salama na bora ya kilimo katika masoko ya kitaifa na kimataifa.  

James alisema mradi huo utahakikisha mfumo wa kitaifa wa udhibiti uingizaji na usafirishaji nje wa bidhaa za kilimo unaimarishwa na taasisi zinazotoa huduma za afya ya mimea, zinatumia mfumo sahihi wa ufuatiliaji na usimamizi.

Alisema mradi wa kusaidia kuboresha mazingira ya biashara, ukuaji na ubunifu, unalenga kuimarisha mazingira ya biashara kwenye mifumo ya leseni, vibali, kanuni na tozo kama ilivyoanishwa kwenye mpango wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.

James alisema mradi huo unalenga kuimarisha Shirika la Viwango Tanzani (TBS), kwa kulipatia vifaa na kuboresha mifumo yake ya kutekeleza majukumu kikamilifu.

Pia alisema utaangalia ubunifu katika ujasiliamali, upatikanaji wa mitaji midogo, kuwajengea uwezo vijana na wanawake wanaojihusisha katika viwanda na biashara ndogo na za kati.

Kuhusu mradi wa ushirikiano wa kitaalamu, alisema, unalenga kuwezesha nchi kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kupitia ushirikianio na EU na unakusudia uimarishaji wa miradi inayoendelea kutekelezwa kupitia Mpango wa 11 wa EDF na kusaidia Serikali kuandaa miradi mipya itakayofadhiliwa kupitia mpango ujao wa ushirikiano wa 2021-2027.

Balozi wa Umoja wa Ulaya, Fanti alisema makubaliano ya kutoa fedha hizo, yanalenga kutatua changamoto zikiwemo za kukua, maendeleo ya sekta binafsi na ajira, uchumi shirikishi na biashara na kuondoa changamoto za tabia nchi.

"Fedha hizo zilizotolewa kama msaada na EU zinalenga kuimarisha ushirikiano baina yao ili serikali kuandaa mazingira wezeshi katika kulata maendeleo ya uchumi endelevu (SDGs), kuzalisha kazi nyingine na kuboresha ubora wa maisha ya Watanzania," alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe alisema mradi wa kuboresha nishati, utaisaidia kuhakikisha Tanesco inafikia azma ya kusambaza umeme kwa kila Mtanzania.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Aloyce Nzuki  alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, watekeleza mradi wa kusaidia mnyororo wa thamani katika ufugaji nyuki katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Katavi, Shinyanga, Singida na Tabora na Zanzibar.

Alisema, mradi wa matumizi endelevu ya nishati ya kupikia, utatekelezwa katika mikoa inayotumia nishati ya kuni kwa wingi ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mwanza na Tabora na Tanga ili kuelimisha wawanchi kuacha kutumia nishati hiyo na kuanza kutumia gesi.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi