loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM atuma rambirambi kifo cha Maalim Seif

JPM atuma rambirambi kifo cha Maalim Seif

RAIS John Magufuli ametangaza maombolezo ya siku tatu na bendera kupepea nusu mlingoti kwa upande wa Tanzania Bara kutokana na kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Rais alisema hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter jana, ambapo alituma salamu za pole kwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kutokana na kifo hicho cha Maalim Seif.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar Dk Mwinyi, familia, Wazanzibari, wanachama wa ACTWazalendo na Watanzania wote. Mungu amweke mahali pema peponi, Amina,” alisema Rais Magufuli katika akaunti yake ya Twitter.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema amepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa ya kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Alisema hayo jana wakati akitoa salamu zake za rambirambi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.

Mama Samia alitoa pole kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, familia ya marehemu, Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Wakati huohuo, akizungumzia kifo cha Maalim Seif, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Humphrey Polepole alisema ni pigo kwa Taifa kwa sababu Maalim Seif alikuwa kiunganishi kikubwa kwa wapinzani na Serikali ya Zanzibar.

Alisema Maalim Seif alikuwa muungwana aliyekubali kuunganisha nguvu kwa njia ya maridhiano, ili kusaidia maendeleo ya Zanzibar.

Polepole aliwataka wanasiasa wengine nchini, kuiga mfano wa utendaji kazi wa Maalim Seif kwa maendeleo ya siasa na Taifa. Mwenyekiti wa Chama Cha TLP, Augustine Mrema alisema kuwa amesikitishwa na kifo cha Maalim Seif na amewaomba Watanzania wote wawe na uvumilivu na utulivu wakati huu wa majonzi makubwa.

Mrema alibainisha kuwa anamjua Maalim Seif na kutambua uwezo wake mkubwa katika siasa tangu mwaka 1995 wakati yeye (Mrema) akiwania urais kupitia NCCR-Mageuzi na Maalim alikuwa akiwania urais wa Zanzibar kupitia CUF.

Alisema licha ya kuwa walikuwa wagombea wa maeneo tofauti, lakini walishirikiana kikamilifu katika siasa, kwa kuwa wote walikuwa wapinzani na tena wenye ushawishi mkubwa.

Msemaji wa Chama Cha CUF, Abdul Kambaya alisema kuwa Taifa na wanasiasa kwa ujumla wamepoteza mtu jasiri na mwanasiasa ambaye alikuwa kinara wa mabadiliko ya siasa nchini.

Alisema kuwa Maalim Seif alikuwa ni mtu mwenye uwezo wa kutuliza vuguvugu la kisiasa pale linapozidi ; na kuwa alikuwa na uwezo wa juu wa kushirikiana na kuwatia moyo wafuasi wake.

Alisema kuwa alikuwa na busara na maamuzi, ambapo siyo yenye tija tu kwake bali hata chama alichokiongoza. Alibainisha kuwa CUF itaendelea kuenzi mazuri kutoka kwake na kuwataka Chama Cha ACT- Wazalendo kuenzi mazuri hayo ya Maalim Seif.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi