loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM: Balozi Kijazi ameondoka kishujaa

JPM: Balozi Kijazi ameondoka kishujaa

RAIS John Magufuli amesema marehemu Balozi Kijazi ameondoka hapa duniani kama shujaa, hivyo Watanzania hawanabudi kuyaenzi mambo aliyoyaamini akiwa duniani na kuyatekeleza.

Akitoa salamu wakati wa ibada ya Misa Takatifu ya kumwombea marehemu Balozi Kijazi iliyofanyika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alieleza alivyomfahamu Balozi Kijazi tangu mwaka 1995 alipoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

Alisema akiwa Naibu Waziri alitembelea maeneo mengi na kukutana na wahandisi wa mikoa. Alisema alipotembelea barabara za Dodoma alibaini kuwa zote zilikuwa zinapitika japo zilikuwa za vumbi.

Magufuli alisema alimuuliza Balozi Kijazi sababu ya barabara zake kuwa nzuri kuliko za wahandisi wengine wa mikoa wakati fedha zinazotolewa ni sawa.

Alisema Kijazi alimweleza kuwa alichofanya ni kuhakikisha kila senti inayotengwa na serikali, inatumika kwenye barabara na kwamba anawasimamia kikamilifu wakandarasi waliopewa kazi ya kuzitengeneza.

Alisema aliporudi wizarani, alimshauri Waziri wa Ujenzi wakati huo, Anna Abdallah kumpandisha cheo Balozi Kijazi kuwa Mkurugenzi ili asimamie barabara zote nchini kama alivyofanya Dodoma.

Waziri alikubali ombi na Kijazi akawa anashughulikia matengenezo ya barabara zote nchini na nyingi zikaanza kupitika. “Kijazi alikuwa hakai ofisini, alikuwa anatembelea barabara zake.

Mwaka 2000 baada ya uchaguzi, nikachaguliwa kuwa Waziri, nilipokuwa Waziri nikajua Rais Mkapa ataniletea Katibu Mkuu mwingine, siyo kawaida kwa waziri kuomba Katibu Mkuu, nikaja Ikulu kumuona Mzee Mkapa, kumuomba Balozi Kijazi awe Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,”alisema Rais Magufuli.

Aliongeza “Kufanya hivyo najua nilikuwa nafanya makosa. Mzee Kikwete (Jakaya) anafahamu, lakini nikaona ngoja nijilipue ili kusudi nimueleze tu Mzee Mkapa, Mzee Mkapa aliniangalia kwanza.

Nafikiri alinishangaa, wala hakunipa jibu; mwaka 2001 au 2002, Mheshimiwa Balozi Kijazi akateuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, alifanya kazi kweli kweli, mageuzi mengi yalifanyika Wizara ya Ujenzi na barabara nyingi zilitengenezwa katika kipindi chake.”

Magufuli alisema, kutokana na utendaji wake mzuri, mwaka 2005 Rais mstaafu Jakaya Kikwete alimteua Kijazi kuwa Balozi wa Tanzania nchini India, ambako pia alifanya mambo mengi ikiwamo kuifanya India kuwa karibu na Tanzania na kuwafanya viongozi wakuu wa nchi hizo mbili kutembeleana.

Alisema alipochaguliwa kuwa Rais, alitafuta mtu wa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi ndipo akamuona Kijazi anafaa.

“Nikamwita kutoka ubalozini nikamteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, alikuwa mnyenyekevu, hajikwezi, hakuwa na makuu, saa zingine ukitaka kumtumbua mtu anakueleza Mheshimiwa labda usubiri kama siku mbili hivi uangalie, na kweli ukikaa siku mbili unakuta umeshabadilisha mawazo. Ipo mifano sitaki kuitoa hapa, wapo wengine hawakutumbuliwa kwa sababu ya Kijazi,”alisema.

Alisema Balozi Kijazi pia alikuwa na uwezo mkubwa wa kuchambua vizuri miswada, iliyokuwa inatoka kwa makatibu wakuu na kulifanya Baraza la Mawaziri kufanya kazi kwa wepesi.

“Kwa hiyo kwangu mimi na kwa Baraza la Mawaziri na watendaji wote ndani ya Serikali, tumepoteza mtu muhimu sana. Mnaona alizaliwa mwaka 1956 lakini mpaka leo alikuwa bado Katibu Mkuu Kiongozi, maana yake alipofika wakati wa kustaafu mwaka 2017, nikajaribu kutafuta mtu wa kuziba pengo lake nikakosa, nikamwongeza miaka miwili, nikifikiri baada ya miaka miwili nitapata mwingine.

“Ikaisha miaka miwili. Mwaka 2019 sikupata. Nikamwongeza tena miaka mingine miwili, kwa hiyo natoa pole sana kwa familia,”alisema Rais Magufuli.

Awali, Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dk Joseph Matumaini, aliwaambia waombolezaji wakati wa Ibada hiyo ya Misa Takatifu kuwa jambo kubwa mbele za Mungu, siyo idadi ya miaka aliyoishi duniani bali namna alivyoishi.

Padre Matumaini alisema maisha ya milele ya mwanadamu baada ya kifo, yanategemea maisha yake ya duniani namna alivyoishi katika uhusiano wake na Mungu, uhusiano wake na watu wengine pamoja na ulimwengu.

“Katika maisha yetu kuna mafumbo mengi na fumbo mojawapo ni kifo, kifo kinatisha lakini ndiyo njia tunayopaswa kuipitia ili kuyaendea maisha yajayo. Na ili mtu uweze kuyaendea vizuri maisha ya ufufuko, basi inategemea sana maisha yako ya hapa duniani, hapa duniani tupo kwenye hija na inategemea sana namna unavyoishi na siyo miaka unayoishi, ”alisema Padre Matumaini.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi