loader
Dstv Habarileo  Mobile
…Aonya kutishana corona, atangaza maombi siku tatu

…Aonya kutishana corona, atangaza maombi siku tatu

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kuondoa hofu katika kipindi hiki, ambacho dunia inapita wakati mgumu wa kukabiliana na ugonjwa wa corona. Badala yake, ametaka wachukue tahadhari, wamtangulize Mungu na waache kutishana na kuogopeshana.

Aidha, ametangaza siku tatu za maombi na kufunga ambapo Waislamu walianza jana, Wasabato wanatarajiwa kuanza leo na Wakristo wengine wataanza kesho Jumapili.

Akitoa salamu jana jijini Dar es Salaam kwenye ibada ya kuaga mwili wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi aliyefariki dunia juzi, Rais Magufuli alieleza kusikitishwa na vitendo vya kutishana na uzushi, vinavyofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii.

Miongoni mwa uzushi uliofanywa ni dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliyezushiwa amefariki dunia ilihali yupo hai na anaendelea na matibabu.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa Serikali haina mpango wa kufungia watu majumbani mwao na Mungu aliyeiepusha Tanzania na madhara makubwa ya ugonjwa wa corona mwaka jana, ataiepusha na mwaka huu.

Alisema magonjwa ya kifua na kupumua, yataendelea kuwepo na hayakuanzia Tanzania pekee bali nchi nyingi zina wagonjwa, jambo alilowataka wananchi kusimama kwa pamoja na kuchukua tahadhari zote huku wakimtanguliza Mungu asiyeshindwa. Tusitishane “Niwaombe Watanzania katika matatizo yote yanayotokea yawe yanatufanya tuwe wamoja, hofu ni mbaya.

Ulipoingia ugonjwa wa kubana mafua mwaka jana tuliushinda kwa kumtanguliza Mungu pamoja na juhudi nyingine mbalimbali, unapoona kitu huwezi kukitatua wewe, mwambie Mungu ndiye muweza, lakini inafikia mahali tunatishana sana, tusitishane,’’alisema Rais Magufuli. Akitoa mfano jinsi wananchi wanavyotishana na kuzusha hofu na taharuki katika jamii, Rais Magufuli alisema mfano mzuri ni taarifa za uzushi wa kifo unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango .

“Leo nimetumiwa meseji na Waziri wa Fedha, Dk Mpango ambaye amelazwa Dodoma naomba niisome hapa meseji yake aliyonitumia kwa faida ya wale waliokuwa wakitweet kwamba amekufa,”.

Rais Magufuli alisoma ujumbe huo aliosema Waziri Mpango alimtumia jana asubuhi ukisema: Mheshimiwa Rais, asante sana nimepata ujumbe wako kupitia kwa mke wangu, kwa neema ya Mungu ninaendelea vizuri , ninakula ninafanya mazoezi ya kifua na kutembea.

Aliendelea kusoma ujumbe huo wa Dk Mpango ukisema, “Hao wanaonizushia kifo kwenye mitandao niliwaombea msamaha kwa Yesu wakati wa sala ya jioni jana (juzi). Rais, Mungu akubariki na akupe neema na ujasiri zaidi katika kuliongoza taifa letu katika wimbi hili. Naungana nawe na familia katika kifo cha mpendwa wetu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Kijazi.”

Rais alisema Watanzania watambue kwamba magonjwa yapo na yataendelea kuwepo, magonjwa ya kifua ya kupumua na mengine yataendelea kuwepo na hayakuanzia Tanzanzia.

Alisema kuwa zipo nchi zimepoteza watu wake wengi ila Tanzania Mungu ameisaidia kipindi kilichopita. Asisitiza tahadhari Akisisitiza wananchi kuchukua tahadhari na kumtanguliza Mungu, Rais Magufuli alisema “Magonjwa yapo na yataendelea kuwepo, hayakuanzia hapa, zipo nchi zimepoteza watu wake wengi sisi Tanzania Mungu ametusaidia sana kipindi cha mwaka uliopita… tukimtanguliza Mungu hashindwi, tumefika mahali hapa njiani watu wanaanza kusita nguvu za Mungu za katika maisha yetu.’’

Alisema imefikia mahali wananchi wameanza kutegemea nguvu za ubinadamu. Aliwataka Watanzania kutambua Mungu yupo na ndiye muweza wa yote na aliwashukuru viongozi wote wa dini kwa kuendelea kuomba.

“Tuendelee ndugu zangu Watanzania kusimama na Mungu, tulishinda mwaka jana, inawezekana hili ni jaribu jingine, nalo tukisimama na Mungu tutashinda, tusitishane na kuogopeshana tutashindwa kufika. Inawezekana kuna mahali tumemkosea Mungu, inawezekana kuna mahali tunapata jaribu kama Waisraeli walivyokuwa wakienda Kaanani. Tusimame na Mungu ndugu zangu Watanzania,”alisisitiza Rais Magufuli.

Alisisitiza, “Kama kufa tutakufa. Unaweza kufa kwa malaria au kansa au magonjwa mengine, kifo kipo ila kamwe tusimuache Mungu, huo ndio wito wangu kwenu. Tusimame na Mungu ndugu zangu.”

Maombi maalumu Akishauri wananchi kufanya maombi maalumu, Rais Magufuli alisema Waislamu walitangaza muda wao wa kuomba. “Na niliambiwa na Mufti niwaombe tena Watanzania kama kuna mahali tulitetereka tuendelee kumuomba Mungu.”

Aliwataka Wasabato wanaosali leo Jumamosi pamoja na Wakristo wengine wanaoabudu Jumapili, waombe na kufunga kwa siku tatu, jambo alilosema ana uhakika ushindi upo.

“Nataka niwape nguvu hiyo ndugu zangu Watanzania. Tutahangaika sana, Mungu ni mwenye uwezo wa kila kitu. Niwaombe viongozi wa dini kama ambavyo mmekuwa mkifanya hivyo, endeleeni kuhimiza maombi, tutashinda, tulishinda mwaka jana, tutashinda mwaka huu na tutashinda miaka yote kwa sababu kamwe Mungu hajaweza kuliacha taifa hili,” alisema.

Alisema mwaka jana taifa liliishinda corona mpaka nchi ikaingia kwenye uchumi wa kati na uchumi ukaendelea kupanda ili hali ugonjwa ukiwapo. Alisema na miradi ya maendeleo, iliendelea kutekelezwa bila nchi kuwafungia watu.

“Hata sasa hatutaweka ‘lock down’ kwa sababu tunajua Mungu yupo siku zote. Niliona nitoe huu wito ndugu zangu kwa sababu mimi ni kiongozi wenu, nina wajibu wa kuwakumbusha kwamba taifa hili liko mikononi mwa Mungu na Mungu ataendelea kusimama,”alisema Rais Magufuli.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi