loader
Dstv Habarileo  Mobile
Balozi Kijazi alikuwa kiongozi wa mfano - Abdulla

Balozi Kijazi alikuwa kiongozi wa mfano - Abdulla

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amemuelezea Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kuwa alikuwa kiongozi wa kupigiwa mfano, aliyeunganisha serikali katika shughuli za kiutendaji.

Akitoa salamu za Serikali ya Zanzibar wakati wa kuaga mwili wa Balozi Kijazi, Abdulla alisema Balozi Kijazi ni kiongozi ambaye alitoa ushirikiano kwa kila mtu na alikuwa daraja zuri la kuunganisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika shughuli za kiutendaji.

Makamu huyo wa Rais ambaye alimwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, aliomba Watanzania kuendelea kuombea Taifa na wananchi wote.

“Kwa masikitiko makubwa tumeupokea msiba huu, lakini tunaendelea kumwombea, kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar na Mheshimiwa Rais, tunatoa pole kwako, tunatoa pole kwa familia, na tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema marehemu wote,”alisema Abdulla.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika salamu zake kwa niaba ya watumishi wa umma, aliitaja siku ya jana kuwa ilikuwa ngumu. Alisema msiba wa Balozi Kijazi ni pigo kubwa kwa taifa na isitoshe wiki tatu zilizopita alishiriki mazishi ya kaka yake mkubwa wilayani Korogwe.

Majaliwa alisema Balozi Kijazi amefanya mambo makubwa ndani ya Serikali ikiwemo umakini, uhodari, uchapakazi. Alisema alikuwa na mapenzi mema kwa watumishi wenzake, kwa kuwapa miongozo ya kusimamia shughuli mbalimbali za serikali.

“Balozi Kijazi alikuwa Meneja wa kwanza wa Tanroads Mkoa wa Lindi na alifanya kazi nzuri sana. Pia natambua wakati akiwa Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri lakini pia alikuwa Katibu wa Kamati ya Sheria na Katiba ya ndani ya Bunge na alitusaidia sana kusimamia na kuipitia miongozo yote ya utunzi wa sheria zilizokuwa zinaingizwa ndani ya Bunge, hakika tumepoteza kiongozi,”alisema Majaliwa.

Alimpa pole Rais John Magufuli kwa kuondokewa na mtendaji aliyefanya kazi nzuri . Alisema Balozi Kijazi alikuwa daraja la watumishi wa umma kwa Rais, aliyesimamia itifaki na miongozo ya serikali.

“Ni jambo zito kulipokea. Amefanya mambo makubwa sana mengi ndani ya serikali. Kama watumishi wa umma, tunajua umakini uhodari na uchapakazi wake alivyokuwa na mapenzi mema katika kutupa miongozo… hakika tumepoteza kiongozi,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema ni wajibu kuenzi yale yote mema mazuri aliyofanya Balozi Kijazi katika utumishi wake na katika uhai wake. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alisema mahakama ilimtegemea kwa kiwango kikubwa.

“Kuna mambo mengi yalihitaji uharaka kumfikia Rais. Balozi Kijazi alikuwa dirisha muhimu sana kumfikia Rais… alijenga taswira ya Katibu Mkuu Kiongozi anatakiwa kuwa mtu wa namna gani,” alisema.

Akizungumzia umakini wake, alisema, “Nakumbuka sana namna alivyopenda kuwa makini kwa mambo madogo madogo sana ambayo wengine tungeweza kuyadharau, kwa mfano wakati tunafanya mazoezi ya kumuapisha Mheshimiwa Rais, aliyasimamia mazoezi yale kana kwamba ndiyo uhalisia halisi, alikuwa makini kwa kila kitu hata mambo madogo.”

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson katika salamu zake kwa niaba ya Spika Job Ndugai, alisema Balozi Kijazi alikuwa mtu mwema na mnyenyekevu aliyeheshimu pia wadogo, jambo aliloshauri kila mtu kuishi maisha ya namna hiyo.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi