loader
Dstv Habarileo  Mobile
Misikiti, makanisa yaendelea kuombea taifa

Misikiti, makanisa yaendelea kuombea taifa

MISIKITI na makanisa ya madhehebu mbalimbali nchini, yameitikia mwito wa  Rais John Magufuli wa kufanya maombi na dua maalumu ya kuombea taifa, Mungu alinusuru na majanga ikiwamo ugonjwa wa corona. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na HabariLEO jana, baadhi ya viongozi wa dini walisema mwito wa Rais umewapa nguvu ya kufanya maombi maalumu na dua, ambazo zitakuwa endelevu mpaka janga hilo litakapomalizika nchini.

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma, alisema kama ambavyo tamko lao la Jumapili iliyopita linavyoelekeza, walifanya dua maalumu kwa taifa Ijumaa lakini dua ni endelevu.

“Mwitikio ulikuwa wa wastani si kama mwaka jana. Lakini tunaendelea kuwahamasisha. Sisi tunaendelea kuhamasisha kuliombea taifa kwa majanga yote ikiwamo maradhi. Kufunga ni siku tatu (Ijumaa), lakini kuomba dua ni endelevu. 

“Mwito wangu ni ule ule kwamba Uislamu umeeleza usafi, huu unatuweka mbali na maradhi, tuhakikishe tunanawa mikono, tutumie vitakasa mikono, uvaaji sahihi wa barakoa sehemu ya mikusanyiko, si barakoa moja inavaliwa siku mbili mpaka tatu, huyo atakuwa anaeneza virusi,” alisema Mruma.

Alitoa mwito kwa misikiti yote nchini kufupisha ibada na sala zisiwe ndefu na misongamano isiwe mikubwa huku akisisitiza watu waendelee kufanya kazi bila hofu, kwani kila Mwenyezi Mungu alilotaka liwe litakuwa, na asilotaka haliwezi kuwa.

Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema walianza dua Ijumaa na itandelea kwa mwezi mzima kupitia sala za kila siku.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk Abednego Keshomshahara, alisema wamepokea mwito wa Rais Magufuli na watafanya maombi ya jumla leo katika makanisa yote na kama walivyofanya mwaka jana, watafanya maombi maalumu kwa siku tatu.

“Tunawasiliana na wachungaji kupitia mtandao wao tufanye maombezi kwa siku tatu, lakini ya wote ni kesho (leo) kwenye makanisa yetu yote. Maombi mengine tutayafanya kupitia sala za makundi, familia na taasisi. Hata hivyo hata kabla ya mwito huo wa Rais tulishaanza na ni endelevu” alisema.

Askofu Keshomshahara alitoa mwito wa kuendelea kumtegemea Mungu katika kulivusha taifa kwenye janga la corona na maradhi mengine na kuzingatia masharti ya afya; huku wakimtanguliza Mung na kumtegemea bila kukata tamaa.

Kwa upande wa  Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kupitia Rais wake, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, lilitoa mwito hivi karibuni kwa viongozi wa kanisa hilo, kuchukua hatua kuliombea taifa na kuzingatia miongozo yote ya afya iliyotolewa na Serikali mwaka jana kuhusu kujikinga na corona.

Lilitaka pamoja na maombi ambayo yanaendelea katika kila jimbo, waumini wakae umbali kutoka mtu na mtu, kuwepo maji ya kunawa mikono na vitakasa mikono, wavae barakoa, maji ya baraka yasiwepo milangoni na wakati wa kupeana amani, waendelee kuinamiana na si kushikana mikono.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) inayosimamia madhehebu 12 ya Kikristo, Mchungaji Moses Matonya, alisema katika kuitikia mwito wa Rais Magufuli, leo makanisa yote yameshapata taarifa na yatafanya maombi kwa Taifa, lakini watapanga maombi maalumu ya kitaifa kama walivyofanya mwaka jana.

“Hata kabla hajasema Rais sisi tulikuwa tunasali na sasa tunafurahi Rais ametamka na hivyo hakuna kigugumizi tena kuhusu hili,” alisema Mchungaji Matonya.

Akizungumza jana wakati akitoa salamu za serikali kwenye misa ya mazishi ya Marehemu Balozi John Kijazi iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Agustino, Jimbo Katoliki la Tanga, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwashukuru viongozi wa dini kwa kuitikia mwito wa Rais Magufuli wa kuliombea taifa kwa siku tatu kuanzia juzi ili Mwenyezi Mungu aiponye nchi hii na magonjwa ya kuambukiza. 

Alisema mwitikio umekuwa mzuri na serikali inatambua nafasi ya viongozi wa dini katika kulifanya Taifa kuwa tulivu na wananchi kuendelea kushirikiana.

“Mheshimiwa Rais alipokuwa anaueleza umma wa Watanzania jana (juzi) kuondoa hofu, pia aliwaomba viongozi wa dini kutuongoza kufunga siku tatu, nawashukuru sana viongozi wa dini, nimeshuhudia jana (juzi) swala zote za Ijumaa wameanza kutekeleza kwa kuzungumza na waumini kuliombea taifa hili.

“Hata leo (jana) kwa Wasabato nawashukuru sana, lakini pia naona maandalizi ya Wakatoliki kesho (leo) kuendelea kuliombea taifa hili,”alisema Majaliwa.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi