loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wanawake washirikishwe katika uamuzi kudumisha haki

JUZI taasisi isiyo ya kiserikali inayoshirikisha jamii kubadili maisha ya wanawake, vijana na watoto (Tiba), Mtandao wa Sisters Without Borders na asasi inayosaidia utekelezwaji wa haki na sheria katika jamii (B2JF) ziliendesha kampeni ya siku katika Kitongoji cha Magomeni C Kata ya Magomeni jijini Dar es Salaam  na Mangesani Kata ya Dunda wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

 

Katika kampeni hiyo iliyohusu umuhimu wa wanawake kushirikishwa katika vyombo na ngazi mbalimbali za maamuzi, Tiba ilizungumzia njia bora za kuwashirikisha wanawake katika maamuzi na namna jambo hilo linavyosaidia kudumisha amani na haki. Sisters Without Boarders na B2JF nao waligusia suala hilo sambamba na wanawake na ujasiriamali. 

 

Kimsingi, taasisi (vikundi) hivyo vilifanya jambo jema hasa ikizingatiwa kuwa wanawake wana uwezo mkubwa katika kutoa maamuzi yanayosaidia kuimarisha na kujenga jamii inayozingatia utu, haki, amani na ustawi wa jamii. 

 

Kimsingi, mwanamke akishirikishwa kwenye kamati za usuluhishi za kata au kitongoji na zikapelekwa kwa mfano kesi za unajisi wa watoto, au kubakwa kwa wanawake au mjane kudhurumiwa haki, mchango wake utasaidia haki kupatikana zaidi kwa urahisi.

 

Yapo mambo mengi ambayo mwanamke anaweza kusaidia upatikanaji wa suluhisho lake.

Izingatiwe kuwa haki baina ya wanawake na wanaume inapokuwa katika jamii, amani ambayo ni msingi wa maendeleo hupatikana na kudumu katika ngazi zote tangu familia.

 

Tanzania ni kati ya nchi zinazotekeleza mikataba mbalimbali ya kimataifa, inayosisitiza ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

 

Kwa msingi huo, ushiriki wa wanawake katika vyombo na ngazi tofauti za maamuzi ukiimarishwa, utasaidia kuboresha amani, haki na utulivu katika jamii.

 

Hata hivyo, ili washiriki kikamilifu wanapaswa kuanza kushirikishwa katika masuala mbalimbali tangu ngazi za familia hadi taifa.

 

Ili kufanikisha hilo, tangu akiwa mdogo, mwanamke ahusishwe katika mijadala mbalimbali ya kifamilia na sauti yake isikilizwe na maoni yake kufanyiwa kazi.

 

Ikumbukwe kuwa wanawake kama walivyo baadhi ya wanaume, wanayo mawazo bora na uwezo mkubwa wa uongozi.

PAMOJA na kwamba siku 21 za maombolezo zimemalizika ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi