loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ndoa za utotoni na adha doa za utotoni na adha za kufukuzwa na waume

BAADHI ya wasichana katika Kata ya Tinde, Shinyanga vijijini, walioolewa katika umri mdogo, wameeleza walivyofukuzwa na waume zao huku wakinyang’anywa mali walizoshiriki kuzichuma.

Wasichana hao pia wameeleza walivyojikuta wahawana mwelekeo katika maisha huku wakihangaika na watoto.

Wanakiri kwamba kutokana na kuolewa katika umri mdogo, hawana pia elimu inayoweza kuwasaidia katika maisha mapya ya nje ya ndoa na pia hawajui waanzie wapi kudai jasho lao lililopotea walipokuwa kwenye ndoa.

Pili Bundala ambaye sasa ana umri wamiaka 20 anasema aliolewa akiwa na umri wa miaka 13 na kukaa kwenye ndoa kwa miaka saba ambako alibahatika kuzaa watoto wawili, wa kwanza ana umri wa miaka sita na wa pili miaka mitatu.

Kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu yeye na mwanawe mdogo baada ya kufukuzwa na mumewe, ameamua kutafuta kibarua cha kuosha vyombo kwa mamalishe.

Pili anasema alipoolewa alimkuta mumewe akiwa hana mali yoyote, wakaanza kushirikiana kwa bidii kulima na kufanikiwa kununua samani za ndani pamoja na kiwanja.

Anasema mumewe waliyekuwa wakiishi naye katika kijiji cha Kayombo wilayani Nzega mkoani Tabora alianza kumnyanyasa baada ya kupata mwanamke mwingine, akamfukuza na kuuza kila kitu na fedha hizo ndizo katumia kuolea mwanake mwingine.

“Tulipata mpunga gunia 20, tulikuwa tukilima mahindi na kuyamwagilia kipindi cha kiangazi na kupata shilingi laki sita. “Baadhi ya vitu tulivyonunua ni redio ya kisasa (subwoofer), kuweka umeme jua na kununua televisheni inayotumia umeme jua na vingine vingi.

Vyote mume wangu ameuza bila kunipatia hata shilingi moja,” anasema Pili. Msichana huyo anasema aliamua kuondoka na mtoto wake mdogo na mwingine kumwacha kwa baba yake na hajui kama mwanae huyo aliyebaki na baba yake anapata matunzo mazuri kutoka kwa mama yake wa kambo ambaye anasikia pia ni binti mdogo.

“Nashukuru nimepata kibarua kwa mamalishe cha kuosha vyombo ili kupata fedha za kujikimu. Kwa siku ninalipwa shilingi 2,000,” anasema.

Jesca Marco (19) ambaye pia anaishi Tinde, masimulizi yake hayatofautiani sana na ya Pili. Yeye anasimulia namna alivyoolewa akiwa bado mtoto na kuishi na mumewe kwa miaka mitatu.

Anasema walijikita katika kilimo na kupata mazao mengi lakini muwewe alipopata mwanamke mwingine alianza kumnyasa na hatimaye kumfukuza huku akimnyang’anya kila kitu ikiwa ni pamoja na nguo zake.

Jesca anasema baada ya mumewe kumfukuza akiwa na nguo moja aliyokuwa amevaa siku hiyo, aliamua kutafuta kazi kwa mamalishe ya kutengea wateja chakula na kuosha vyombo ambapo analipwa shilingi 2,000 kwa siku.

“Baada ya mume wangu kunifukuza sikushtaki sehemu yoyote kwa sababu hata sijui pa kuanzia. Nilimuacha tu aendelee na maisha yake kwani alikuwa na mwanamke mwingine.

Aliniona takataka, akaninyang’anya nguo zote na mpaka sasa wazazi wangu hawajui kama nimeachika,” anasema Jesca. Mebo Waziri, mama yake Pili Bundala anakiri kumwoza bintiye katika umri mdogo na kisha mwanae kukumbana na manyanyaso makubwa kutoka kwa mumewe hadi kuachika.

Hata hivyo, Mebo anasema anafikiria kumshitaki aliyekuwa mume wa mwanae kwa kitendo alichofanya ili haki ipatikane kwa wote. Anasema mwanae kalima sana kwa ajili ya familia yake lakini kaishia kufukuzwa akiwa hana chochote.

Getrude Samson na Mariamu Kulwa wanaojishughulisha na biashara ya mama lishe, wanasema wasichana wengi walioolewa katika umri mdogo na wengine kupata mimba za utotoni wamekuwa wakifika kutafuta kazi ya kuosha vyombo au kupika ili wapate fedha hata kidogo za kujikimu.

Getrude anasema Pili alipokwenda kuomba kazi ya kuhudumu na kusikiliza namna anavyohangaika na mwanae baada ya kufukuzwa na mumewe, akakubali kumwajiri.

Getrude anakiri kwamba wasichana wengi wakiwemo wanaoolewa katika umri mdogo wafanyiwa vitendo vingi vya ukatili baada ya kuzaa na mapenzi motomoto kuisha.

Anasema wasichana hawa wanaoolewa katika umri mdogo ni rahisi sana kunyanyaswa na waume zao kulinganisha na wale walioolewa wakiwa tayari wamekomaa kiakili kwa kuwa ni rahisi kuwaburuza.

Anawaasa wazazi kuacha kukimbilia mahari na kuoza watoto wao wakiwa hawajakomaa kiakili na mbaya zaidi wengine wanawatoa shule ili waolewe.

Mkazi wa kijiji cha Jomu, kata ya Tinde, Kituro Zacharia, anasema kuwa jamii bado haina uelewa mpana wa namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili kwani wakiona watu walio kwenye mahusiano ya kimapenzi wanafanyiana vitendo vya kikatili jamii inaona kama jambo la kawaida.

Anasema jamii wakiwemo baadhi ya polisi wamefikia kuona kama masuala ya unyanyasaji ndani ya ndoa siyo ya kuingiliwa wakiita ni ‘mapenzi ya watu wawili’ na kwamba wataelewana badaye, lakini anataka jamii iondoe huo mtazamo.

Mtendaji wa kijiji cha Jomu, kata ya Tinde, Cheyo Maganga, anasema kuwa ukatili dhidi ya wanawake na watoto upo kwani baadhi ya wanawake wamekuwa wakija kushtaki namna walivyonyang’anywa mali walizochuma pamoja waume zao sambamba na wanaume hao kulalamikiwa kwa kutelekeza watoto. “Suala la baadhi ya wanaume kutelekeza watoto na kuwafukuza wake zao ni changamoto.

Inakuwa mbaya sana kwa mabinti wanaoolewa katika ndoa za utotoni kwa sababu huwa bado wadogo kujua wafanye nini,” anasema mtendaji Cheyo.

Diwani wa kata ya Tinde, Jafari Kanolo, anasema kuwa changamoto ya ndoa za utotoni zipo na kwamba ni jambo linalopaswa kupigwa vita.

Anasema baadhi ya wanaume wanaooa watoto wadogo hufanya hivyo kwa tamaa na wakishatimiza tamaa zao, wanatafuta watoto wengine tena wa kuoa na kuwafukuza hawa wa awali.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kata ya Tinde, Eva Mlowe, anasema kuna kamati za kutokomeza ukatili wa kijinsia za kila kijiji na kwamba zinazotoa elimu kwenye jamii ili kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa aina hiyo.

Anasema kipindi cha miezi mitatu katika kata hiyo, kuna akina mama wanane walioripoti kufanyiwa ukatili lakini wengine wamekuwa hawaripoti.

“Kesi za wasichana walioolewa katika umri mdogo kufanyiwa ukatili na waume zao zipo na lakini nyingi haziripotiwi kutokana na wahusika kutokuwa na elimu au mwamko wa kupigania haki zao na hivyo hubaki kunyamaza tu.

“Hivi tunavyoongea yupo binti wa miaka 20, ninaye kwangu, ana mtoto wa miaka saba. Huyu binti kafukuzwa na mumewe waliyekuwa wanaishi miaka mingi na wamechuma naye mali nyingi. Hivyo naisimamia kesi hii kuifikisha mahakamani ili huyu binti naye apate haki yake,” anasema Mlowe.

Mlowe anasema kila kijiji hivi sasa kuna kamati za Mtandao wa Kutokomeza Ukatili dhidhi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) zinazotoa elimu kwenye jamii namna ya kuripoti vitendo vya ukatili vya aina yoyote pindi mtu akifanyiwa ili hatua ziweze kuchukuliwa na kila mmoja apate haki yake.

Aisha Omary, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambaye pia ni katibu wa Mtakuwwa, anasema wamepatiwa kiasi cha shilingi milioni 25 zilizofadhiliwa na Woman Fund Tanzania (WFT) kwa ajili ya kutekeleza mpango huo katika kata 13 ikiwemo kata ya Tinde.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lyidia Kwesigabo, anasema suala la baba kutelekeza watoto na mama kunyimwa haki yake ni ukatili na kwamba mkoa wa Shinyanga unaongoza nchini kwa ukatili huo kwa asilimia 78 .

“Vitendo vya kikatili kwa wanawake na watoto vinapaswa kukomeshwa. Jamii inatakiwa itoe ushirikiano na kuwapatia watoto malezi yaliyo bora kwa wazazi wote kushirikiana ili kujenga taifa imara.

Wazazi, hususani wa kiume wasiwatelekeze watoto.

Unaweza kumfukuza mwanamke akiwa na mwanao mchanga.

Ni muhimu wazazi wote wawilinde watoto kwa nguvu zote na kuwapenda,” anasema Kwesigabo. Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, anawataka wanawake na watoto wanaonyanyaswa kutumia madawati ya jinsia ambayo yako katika vituo vya polisi karibu vyote kutoa malalamiko yao.

Anasema madawati hayo yameboreshwa na yana wataalamu ambao wamefundishwa kushughulikia watu waliofanyiwa vitendo vya ukatili ili haki ipatikane kwa pande zote.

“WANANCHI waliopata hati za hakimiliki za kimila baada ...

foto
Mwandishi: Na Kareny Masasy

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi