loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Mume kanikimbia Mume kanikimbia kugundua mtoto ni mlemavu, nashindwa kumtibu, kumlisha’

SAA 12:30 jioni ya Februri 15, mwaka huu, nilimkuta akiwa na mwanae wakimsubiri Imamu wa Msikiti wa Nurul-yakini, ulioko Temeke, Mwembayanga, Dar es Salaam. 

Aliniambia amekuja kuomba msaada wa matibabu ya mwanae anayesumbuliwa na upele. Aliniambia pia kwamba mtoto huyo anajikuna sana na kwamba upele humletea homa kali lakini hana pesa za kununua dawa.

Mara moja nilihisi kwamba mwanae huyo atakuwa pia na tatizo la ulemavu kwani alikuwa tofauti na watoto wengine.

Nilipomuuliza kama ameshafanya mawasiliano yoyote na imamu, mwanamke huyo, Zuhura Shabani, Mkazi wa Chamazi, Dar es Salaam, alisema: “Imamu alinipa namba ya viongozi wa Taasisi ya Jamiiyatul Akhlaaqul Islaam (JAI) ili niwaeleze tatizo la mwanangu, lakini sijui nilinakili vibaya namba yao au yeye alikosea kwa kwa sababu kila nikiipiga haipatikani.

Nimekuja tena kwa sababu mwanangu ana homa na anaumia sana. Usiku hatulali.” Nilipomuuliza kuhusu ushiriki wa baba wa mtoto pamoja na majirani katika kusaidia matibabu ya mwanae, majibu yake yakanishiwishi kufanya naye mahojiano haya. Zuhura, alianza kwa kuniambia kwamba mwanae huyo aitwaye Ikram alimzaa mwaka 2019, hivyo sasa ana miaka miwili.

Wakati huo anasema alikuwa akiishi na mumewe raha mustarehe, yeye akifanya kazi kwenye saluni ya mtu na mumwe akijishughulisha na biashara. “Tulikuwa tunashangaa kuona mwanetu yuko tofauti na watoto wengine.

Hakui vizuri kama wengine na wala hakai. Mume wangu akawa anauliza mara kwa mara, mbona mtoto hakai, mbona hivi, nikamwambia hata mimi sijui. Siku moja nikaamua kwenda hospitali kuwaona wataalamu. Nilifika zahanati moja kule Chamazi, nikashauriwa niende hospitali ya CCBRT,” anasema Zuhura.

Anasema watalaamu wa CCBRT walipomchunguza kwa kina Ikram, wakagundua kwamba ana tatizo la mtindio wa ubongo. “Yaani nilivyoambiwa hivyo, roho iliniuma sana, lakini daktari akasema kinachotakiwa ni mtoto kumwanzishia mazoezi, kumpatia lishe nzuri na kumwomba Mungu.

Daktari alisema kama atafanya mazoezi kwa wakati na kupata lishe bora, itamsaidia mtoto hata kujisaidia yeye mwenyewe kama kuweza kukaa, kuvaa akiwa mkubwa na kadhalika.

” Anasema aliporejea nyumbani, akamweleza mumewe alichoambiwa hospitali lakini mwanaume huyo hakupokea vyema taarifa hiyo. “Akatamka kitu ambacho sikukitegemea, kwamba hawezi kuendelea kuishi na mimi.

” Anasema kwa siku chache mumewe alikuwa mkimya sana na siku moja alipokuwa amempeleka mtoto hositali kwa sababu alikuwa anaumwa, aliporejea nyumbani hakumkuta.

“Alichukua vitu vyake vyote na kuniachia godoro, kitanda na kabati. Hadi leo sijui alipo na umepita zaidi ya mwaka,” anasema. Afafanua kwamba kwa sasa bado anaishi kwenye nyumba ya kupanga ambako mumewe alimwacha kutokana na huruma ya mwenye nyumba kwani anadaiwa kodi ya miezi kadhaa.

“Kwa vile aliondoka huku mtoto anaumwa sana, nilijikita kwanza katika kushughulikia matibabu yake na alipopata nafuu, ndipo nikamtafuta huyo mume wangu ambaye tumeishi naye kwa miaka mitatu.

” Zuhura ambaye ana mtoto mwingine aliyezaa na mwanaume mwingine, anasema alipowasiliana na mumewe huyo aliyemkimbia kwa njia ya simu, alimweleza kwamba hana mpango tena wa kuishi naye na wala asimtafute, kisha akakata simu.

“Kila nikimpigia alikuwa hapokei simu baadaye alibadili kabisa namba ya simu.

Sasa hivi sijui alipo wala namba yake sina. Hata ndugu zake wa karibu ambao pia hawanisaidii kuhusu huyu mtoto wanasema hawajui namba yake ya sasa,” anasema Zuhura.

Anasema yeye alikuwa anafanya kazi kwenye saluni ya mtu na kwamba alijaribu kurudi kwenye saluni akiwa na mwanae lakini bosi wake alimwambia kwa hali ya mwanae ambaye hawezi kukaa, itakuwa vigumu kuendelea naye na hivyo akamfuta kazi.

“Mwanangu hawezi kukaa. Mbaya zaidi huwa anapata tatizo la kushtuka ambalo linaweza kumpata hadi kwa nusu saa. Anapokuwa anashtuka analia sana.

Kimsingi kila mara lazima niwe naye kwa hiyo nimeshindwa hata kutafuta kazi kwenye saluni nyingine,” anasema.

Anasema jijini Dar es Salaam ana ndugu zake wawili wa ukoo na kwamba wana habari kuhusu madhila anayopitia na mwanae lakini wote hawana uwezo wa kumsaidia.

“Ukiacha hawa ndugu wa Dar es Salaam, nyumbani kwetu, Magole, Morogoro ninao ndugu wengi tu.

Lakini kwa hili hakuna hata wa kunisaidia. Wapo wanaopenda sana kunisaidia lakini hawana uwezo na mimi siwalaumu kwa sababu ninajua hali zao,” anasema Zuhura ambaye alishafiwa na baba yake mzazi lakini mama yake ambaye pia anahitaji msaada wake, bado yuko hai.

Kwa mujibu wake, amekuwa akipata misaada ya kula na nauli kwa majirani ambao wameshachoka kumsaidia. “Sina chochote cha kuniingizia pesa. Swezi hata kumununulia mwanangu dawa ya Sh 10,000.

Leo nimepata nauli tu kuja kumwona imamu ili aniunganishe na JAI na hata nauli ya kurudi Chamazi sina.

Itabidi tu niombe watu,” anasema. Latifa Mushi ambaye ni muuguzi kitaaluma aliyemwangalia mtoto wakati nikifanya naye mahojiano, alisema tatizo la upele la mtoto huyo mara nyingi hutokana na kuoga maji ambayo siyo safi.

“Huu upele unawasha sana hata ukiwa nao mtu mzima hulali usingizi.

Unawasha sana,” alisema Latifa na kuongeza kwamba makwapa ya mtoto huyo yanaonesha kuwa ana tatizo la utapiamlo.

Muuguzi huyo kitaaluma lakini anayeuza duka la dawa (Pharmacy) alitoa mchango wa Sh 5,000 ili kusaidia dawa za kuweza kumtibu upele mtoto huyo. Mwandishi wa makala haya na watu wengine walichanga zikapatikana Sh 25,000 na kisha mtoto huyo akanunuliwa dawa.

Imamu Msaidizi wa Msikiti wa Nurul-yakin, Shehe Shaaban Chande, anasema: “Ni kweli, huyo mama alikuja hapa msikitini akitaka msaada wa tiba ya mwanae na matumizi mengine. Nikamwambia cha kumsaidia ni kumuunganisha na JAI, ndipo nikampa namba za watu wa JAI. Alikuwa hana nauli ya kurudi Chamazi, nikamsaidia.

Ninashauri aje tena Jumatano pengine akaonana na watu wa JAI hapa hapa msikitini.

” Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kwamba JAI wanaweza kumsaidia katika eneo la tiba ya mwanae lakini si mahitaji mengine kama ya lishe ya mtoto na nauli ya kumpeleka CCBRT kwa ajili ya mazoezi kila mara na huduma nyingine za tiba.

Nilipomuliza Zuhura kwa nini ameruka misikiti ya Chamazi na kuja Temeke, alijibu kwamba kuna mtu aliyemwelekeza kuja Msikiti wa Nurul-yakin kwamba anaweza kupata msaada.

“Nimeshafika kwenye misikiti mitatu ya Chamazi lakini sijasaidiwa.

Nilifika hata Clouds Media na kuwaeleza matatizo yangu na mwanangu kama ninaweza kupata msaada kwa kuwa tatizo la mwanangu ni endelevu wakasema kwa sasa ratiba yao imebana na kwamba wakipata nafasi wataniita.

Walichukua namba yangu ya simu lakini sasa ni mwezi wa nne hawajaniita,” anasema mwanamke huyo ambaye anatembea na nyaraka kutoka serikali ya mtaa wake inayomruhusu kuomba msaada.

Anasema akiwa na nyaraka zake hizo, aliwahi kwenda Msikiti wa Maamur ulioko Upanga ambako pia alielekezwa na mtu akaombe msaada lakini hakufanikiwa kusaidiwa.

Anapoulizwa ni kitu gani ambacho anatamani kusaidiwa kama wapo watu wa aina hiyo, Zuhura anasema: “Maisha ambayo ninaishi na huyu mtoto ni magumu sana.

Ninachoomba kwanza ni mwanangu kuweza kufanyiwa mazoezi au kupata vipimo kwenye hospitali kubwa na lishe ya uhakika. “Lingine ninaomba kama ninaweza kupatiwa mtaji wa biashara ili niwe nakaa hapo kwenye biashara na mwanangu.

Lakini kwa kuwa mimi nina ujuzi wa saluni, nikipata mtu akanifungulia saluni katika eneo zuri ninaweza kuiendesha na kujikimu mimi na mwanangu. Mawasiliano ya Zuhura ni 0714 764 776.

“WANANCHI waliopata hati za hakimiliki za kimila baada ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi