loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bwawa la umeme la Nyerere kujazwa maji Novemba

WAZIRI wa Nishati , Dk Medard Kalemani, amesema bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP) litaanza kujazwa maji Novemba 15 mwaka huu na hadi Aprili 15, 2022 litakuwa limejaa.

Dk Kalemani jana alimuagiza mkandarasi na msimamizi wa mradi huo ahakikishe shughuli zote za maandalizi ziwe zimekamilika kabla ya Oktoba mwaka huu ili ujazaji wa maji kwenye bwawa uanze Novemba 15 mwaka huu.

Alitoa agizo hilo alipombelea kukagua mradi huo unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115. Ujenzi wa mradi huo umepangwa kukamilika Juni 14, 2022.

"Hizi ni habari njema kama tunafikia kuona  tunaanza kujaza maji kwa ajili ya kuanza kufua umeme ni faraja kwetu , lakini kwa leo ninaagiza  kwa mkandarasi na hili ni agizo mahususi mkandarasi asimamiwe akamilishe kazi hii haraka ndani ya mpango kazi wake " aliagiza Dk Kalemani.

Alisema bwawa hilo litakuwa na kimo cha mita 131, urefu wa mita 1,125 na ujazo wa mita bilioni 35.5 za maji.

Dk Kalemani alitoa maagizo matatu kwa mkandarasi wa Arab Contractors na Elsewedy Electric kutoka Misri aongeze idadi ya wafanyakaze, apeleke vifaa vya kutosha na afanye kazi usiku na mchana.

"Hapa panapojengwa bwawa hili alete wafanyakazi wa kutosha, sijaridhika na idadi ya wafanyakazi waliopo, ninataka kuona kazi hizi zinafanyika usiku na mchana  " alisema.

Dk Kalemani alimtaka msimamizi wa mradi huo ahakikishe anamsimamia mkandarasi ili kuona bwawa hilo linajazwa maji ndani ya mkataba na si anavyotaka yeye ya kulijaza hadi Desemba mwakani na akaagiza kazi hiyo iishe Aprili 2022.

Alihoji kuhusu  maelekezo aliyoyatoa kuhusu mapitio ya mpango kazi wa mkandarasi ili aweze kufidia muda unaopotea wa  siku 10 hadi 15.
 

“Mmemweleza nyie lakini mmeniambia hawezi kuuleta na kama hawezi kuuleta anafanya nini hapa, na wewe mhandisi mkazi wa mradi huu nimekuambia una mamlaka kwenye mkataba "alisema Dk Kalemani.

Alisema mhandisi mkazi wa mradi huo, ana uwezo  wa kumkataa kiongozi wa wakandarasi (Mohammed Hassan)kwa kuwa yeye (Waziri) hajaridhishwa na ufanyakazi na utendaji wa kiongozi wa wakandarasi.

"Ndiyo maana nimeelekeza mpitieni mkataba mkatae, kwa dalili hii hatuwezi kufika nataka kuona nikataporudi hapa Aprili mwaka huu nisimkute ,nikute msimamizi mwingine, bosi wao mwingine anayeweza kuwasimamia kwenda mbele, hawezi kwenda tofauti na makubaliano ya mkataba na sitaki kuona mkandarasi anapingana na maelekezo ya mwajiri wake " aliagiza Dk Kalemani.

Alisema tayari serikali imemlipa mkandarasi trilioni 1.902 hadi Februari mwaka huu ambazo ni asilimia 100 ya malipo ya mpango kazi wake.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Rufiji

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi