loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samia ataja siri mafanikio madini

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema nchi nyingi za Afrika kwa kipindi kirefu hazijanufaika na rasilimali madini walizonazo ikiwemo Tanzania, hivyo mwaka 2016 Serikali ya Tanzania ilifanya mageuzi yaliyosaidia kuimarisha sekta ya madini na Taifa kuanza kunufaika na rasilimali hiyo.

Pia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi tano wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Siku Tatu wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania ulioanza juzi na kuhitimishwa leo.

Samia alitaja baadhi ya mageuzi ambayo serikali iliyafanya katika kuimarisha sekta ya madini kuwa ni kufanya mapitio na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017, kuboresha mazingira ya biashara na kuweka miundombinu wezeshi na rafiki kwa sekta hiyo.

Alisema mageuzi hayo yaliimarisha ushiriki wa nchi na wananchi katika mnyororo wa thamani na uchumi wa madini kwa kuzuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi, kuanzishwa kwa minada ya masoko ya madini nchini na kuanzishwa kwa Tume ya Madini.

“Mageuzi haya yalisaidia kuzuia usafirishaji wa madini ghafi kwenda nje ya nchi kama ilivyokuwa kwa mchanga wa makinikia na kuhakikisha uongezaji thamani unafanyika hapahapa nchini kwa kujenga viwanda vya uchenjuaji, kuanzishwa minada ya masoko ya madini ili kuwawezesha wachimbaji wadogo na wa kati kupata masoko ya uhakika na kudhibiti utoroshaji, kuanzishwa kwa Tume ya Madini ili kuimarisha usimamizi na udhibiti wa sekta ya madini,” alisema Makamu wa Rais.

Alisema mabadiliko ya Sheria ya Madini hayakulenga kuwaonea wawekezaji bali kuweka mazingira yenye uwiano katika mgawo wa mapato kwa pande zote mbili kama inavyodhihirika kwenye makubaliano kati ya serikali na Kampuni ya Barrick uliowezesha kuanzishwa kwa kampuni ya ubia ya Twiga pamoja na ubia kati ya Kampuni ya LZ Nickel ya Uingereza kwa kuanzishwa kwa Kampuni ya Tembo.

Kutokana na mageuzi hayo yaliyofanywa na serikali kwenye sekta ya madini, Makamu wa Rais alisema sekta hiyo imeendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa.

Alisema mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi asilimia 5.2 mwaka 2019. Alisema mwaka 2019 madini ya dhahabu yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5,252.06 yaliuzwa na kuliingizia Taifa Dola za Marekani milioni 369.50 kama mrahaba na ada ya ukaguzi.

“Ni matumaini yetu kwamba ifikapo mwaka 2025 mchango wa sekta hii ufikie asilimia 10 katika Pato la Taifa, aidha katika mwaka huu wa fedha, Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya Sh bilioni 526.72 sawa na wastani wa Sh bilioni 43.9 kwa mwezi, lakini imeshakusanya Sh bilioni 360.74 katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu,” alisema Samia.

Kuhusu wachimbaji wadogo, alisema serikali inatambua mchango wao katika sekta ya madini, hivyo inaendelea kubuni na kuimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo au kuwapatia leseni kwenye maeneo yenye taarifa za kijiolojia.

Aliwataka wachimbaji wakubwa na wadogo kuzingatia utunzaji wa mazingira kwenye shughuli zao za uchimbaji hata kama madini yanachangia Pato la Taifa na kutoa ajira nyingi.

Aliwataka wafukie mashimo baada ya kuchimba, kupanda miti, kuacha matumizi mabaya ya kemikali za kuyeyushia madini, kutotiririsha maji yenye kemikali kwenye mito na kutomwaga sumu kwenye ardhi.

Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema zaidi ya asilimia 90 ya sekta ya madini inaendeshwa na sekta binafsi licha ya kuwepo kwa changamoto chache kwa baadhi yao kujihusisha na utoroshaji wa madini.

Biteko alisema katika kipindi kifupi kilichopita kulikuwa na matukio 102 ya utoroshaji wa madini yenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya milioni 20, karati zaidi ya 6,000 na kilo zaidi ya 163 zilikamatwa.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema washiriki wa mkutano huo ni nchi 24 ikilinganishwa na nchi 10 zilizoshiriki mwaka jana.

Alisema pia kampuni 49 zinashiriki ikilinganishwa na kampuni 10 mwaka jana, lakini pia mawaziri wa madini 19 wa nchi za China, Jamhuri ya Czech, Brazil, Ghana, Burundi, Sudan, Sudan Kusini, Zambia, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Angola, Nigeria, Zimbabwe na Kenya walishiriki mkutano huo wengine moja kwa moja wengine kwa njia ya mtandao.

Katika mkutano huo wa jana, Makamu wa Rais pia alikabidhi zawadi wa wachimbaji saba kati ya 38 waliofanya vizuri zaidi katika kipindi cha mwaka uliopita.

Miongoni mwa waliokabidhiwa zawadi hizo ni mchimbaji mdogo wa madini ya rubi, Gabriel Laizer kwa kumiliki leseni ya uchimbaji na kufanya shguhuli zake kwa kutimiza matakwa ya sheria pamoja na Zamda Abdallah Adam kutoka kundi la wanawake aliyefanya vizuri zaidi katika shughuli za uchimbaji madini, kufuata sheria, mpangilio mzuri wa kampuni yake, kutoa ajira kwa Watanzania na kuchangia mapato ya serikali.

Wengine ni Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Geita (GGM) iliyochukua tuzo tatu ikiwemo ya utunzaji wa mazingira na usalama migodini, mchango kwa jamii na ushindi wa jumla. Mwingine aliyepewa tuzo au zawadi ni Mgodi wa dhahabu wa Shanta kwa ushirikishaji na uwezeshaji Watanzania katika sekta ya madini.

MAMLAKA ya Mawasiliano (TCRA), imezitaka kampuni za simu ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi