loader
JK: Tanzania hakuna mchumi kama Ndulu

JK: Tanzania hakuna mchumi kama Ndulu

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema mpaka sasa hakuna mchumi bora Tanzania kama Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu.

Kikwete aliyasema hayo jana nyumbani kwa marehemu Mbweni Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam alipokwenda kusaini kitabu cha maombolezo kutokana na kifo cha gwiji huyo wa uchumi kilichotokea juzi. 

Alitaja sababu ya Profesa Benno Ndulu kuwa mchumi bora kuwa ni kutokana na ujuzi na mchango wake mkubwa katika uchumi wa dunia na kutambulika kwake kulikosababisha kutumika kujenga chumi za nchi mbalimbali duniani. 

Alisema ubora wa Profesa Ndulu katika masuala ya uchumi alianza kuuona tangu akiwa Waziri wa Fedha, na kwamba, baada ya kuanzisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwaka 1996, alimteua Profesa Ndulu kuwa Mwenyekiti wa Bodi.

“Nilipokuwa Rais nilitamani sana Profesa Ndulu awe mshauri wangu katika masuala ya uchumi, lakini nilishindwa kumtoa katika mambo ya kimataifa ambako alikuwa tegemeo kubwa kwa Benki ya Dunia,” alisema Kikwete ambaye kitaaluma ni mchumi.

Alisema wakati huo aliamua kumuomba Profesa Ndulu ushauri kuwa ni nani anaweza kuwa mshauri wake katika masuala ya kiuchumi. 

Alisema baada ya Profesa Ndulu kupokea ombi hilo, alimpendekeza Dk Philip Mpango ambaye sasa ni Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Kutokana na kuhitajika kwa kiasi kikubwa katika nchi yake, Gavana wa Benki Kuu wakati huo, Dk Daudi Balali alimwomba Kikwete amtafutie msaidizi na kiongozi huyo alimpendekeza Profesa Ndulu hivyo akawa Naibu Gavana BoT hadi Balali alipofariki dunia na kumwachia kiti Profesa Ndulu.

Msemaji wa familia, Exaudi Ndulu alilieleza HabariLEO kuwa Profesa Ndulu alinunua eneo kwa ajili ya kuzikwa pindi atakapoaga dunia.

Huku akionesha stakabadhi za manunuzi ya viwanja hivyo, Exaudi alisema mwaka 1988 kiongozi huyo alinunua viwanja viwili katika Wilaya ya Kinondon, na kwamba kimoja atazikwa mama yake mzazi na kingine atazikwa yeye mwenyewe.

Alisema baada ya mama mzazi wa Profesa Ndulu kufariki dunia mwaka 2011, alizikwa katika eneo hilo hivyo kilibaki kiwanja ambacho atakazikwa Benno Ndulu kesho.

Balozi Ami Mpungwe

Baadhi ya watu wa karibu na marehemu Profesa Ndulu, wamemwelezea kuwa alikuwa tegemeo la dunia katika masuala ya uchumi. 

Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Ami Mpungwe alisema anatoka katika eneo moja na marehemu Ifakara mkoani Morogoro.

Balozi Mpungwe alisema kutoka katika utoto wao, walifahamiana kiasi cha kuzidi urafiki wao na kufikia katika kiwango cha kuwa kama ndugu. 

Alisema akiwa shule ya msingi mwaka 1958, Ndulu alikuwa darasa moja mbele yake wakati huo yeye alikuwa darasa moja na Jaji Mstaafu Salum Masati mwaka 1959 katika Shule ya Msingi Mtakatifu Francis mjini Ifakara mkoani Morogoro.

Alisema baada ya hapo maisha ya elimu ya sekondari, kila mtu aliekekea upande wake ambako Ndulu alikuwa Azania na walikutana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1971. 

Alisema wanafunzi waliohitimu mwaka 1974 ni Profesa Ndulu, Mizengo Pinda ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, George Mkuchika na marehemu Ditopile Mzuzuri.

Balozi Mpungwe alisema wakiwa UDSM, Ndulu aliwatangulia darasa moja watu waliokuja kuwa maarufu akiwemo yeye mwenyewe, Jakaya Kikwete na Maalim Seif Sharif Hamad. 

Alisema kilichombeba Benno shuleni ni kuwa alikuwa anasoma kwa bidii na hakuwa mtoro shuleni na kufanikiwa kufaulu vizuri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kubakizwa kama mhadhiri wa uchumi katika chuo hicho.

Pia mafanikio yake yalisababisha hata Chama cha Ukombozi cha ANC cha nchini Afrika Kusini kumchukua mwaka 1992 hadi 1993 kwa ajili ya kutengeneza sera za uchumi wa Afrika Kusini. Baadaye hata ilipoingia madarakani Serikali ya Cyril Ramaphosa alimtumia pia kama mshauri wa uchumi.

Pia Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abby Ahmed na Waziri Mkuu wa Sudan wote walimwomba atoe mchango wake katika kuimarisha uchumi wa nchi hizo. 

Profesa Ndulu aliaga dunia juzi Jumatatu katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa kesho Kinondoni.  

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/867c8f6f5ab3d73cef8d11e5dbb7921e.jpg

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi