loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM aisuka upya Dar

JPM aisuka upya Dar

John Magufuli ameivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaama na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosaininiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo mabadiliko hayo yameanza jana.

Taarifa hiyo ilisema: Kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 84 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji ) Sura ya 288, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli ameipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuanzia leo tarehe 24 Februari,2021.

Taratibu nyingine za kisheria zitakamilishwa ikiwa ni pamoja na kuhamisha shughuli za iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo imevunjwa leo kwenda Halmashauri mpya ya Jiji la Dar es Salaam na kuwapangia vituo vipya vya kazi watumishi wa Halmashauri iliyovunjwa.

Aidha, mgawanyo wa mali na madeni ya iliyokuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam ambayo imevunjwa leo utafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (mamlaka za Miji) Sura ya 288 na Sheria nyingine zinazohusika.

Naipongeza iliyokuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa kupandishwa hadhi kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Mkutano na wananchi Jana akizungumza na wananchi wakati akizindua Daraja la Juu la Kijazi katika makutano ya barabara za Mogororo, Mandela na Sam Nujoma jijini Dar es Salaam Rais Magufuli alisema atalivunja na kulisuka upya jiji la Dar es Salaam kwa kuipa hadhi hiyo moja ya manispaa kwenye jiji na kulivunja Baraza la Madiwani.

Rais Magufuli alisema, anafanya hivyo kwa sababu hakuna tija yoyote kwa sasa kuwa na jiji lenye madiwani wasiochaguliwa na wananchi na wanatumia fedha.

“Niwape taarifa, nataka kufanya mabadiliko kidogo,hii ya kuwa na manispaa zinazowakilisha maeneo halafu unakuwa na jiji halina maeneo yoyote hili hapana, hivyo ninategemea kulivunja Jiji la Dar es Salaam, kuwa na madiwani ambao wanakaa hapa juu wanachangiwa hela hawana miradi ya maendeleo wanakula posho na hawakuchaguliwa na wananchi hili nitalikataza.

Nazungumza hapa ili wale wanaojiandaa kuwa mameya wa jiji la Dar na wanakaa hawana maeneo wajue hicho kimekwisha’’ alisema. Alisema katika muundo mpya moja ya manispaa ya jiji hilo itapandishwa hadhi iwe jiji na akasema anaona Manispaa ya Ilala inafaa kwa kuwa ipo katikati ya jiji.

“Dodoma ni jiji lakini huwezi kukuta limechukua eneo fulani na kulifanya ndio jiji linaning’inia juu, Mwanza nako kuna Jiji unakuta Nyamagana Na Ilemela sehemu moja ina jiji nyingine zinabaki kuwa manispaa’’alisema Rais Magufuli.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alisema jana kuwa suala la Rais Magufuli kupandisha hadhi manispaa ya Ilala liko kwenye mamlaka yake na kwamba muundo huo ni wa kawaida nchini.

Alisema Dar es Salaam haitakuwa yenyewe yenye muundo huo usiokuwa na Halmashauri ya jiji, kwani mikoa mingine kama vile Mbeya, Arusha na Tanga nayo ina muundo kama huo na inafanya kazi vizuri.

“Haya ni mamlaka aliyonayo Rais, na muundo huu ni wa kawaida hapa nchini. Kama ilivyo Mbeya, Tanga, Ilemela na Arusha na maeneoe mengine, Dar es Salaam nayo sasa itakuwa na sura hiyo,”alisema Jafo.

Rais Magufuli alisema ukiwa na manispaa nne au tano na unakuwa na madiwani wasio na uwakilishi wa wananchi na halafu wanatengewa bajeti ya fedha, hayo ni matumizi mabaya.

“Kwa hiyo tujiandae kisaikolojia wale waliokuwa wanautaka umeya wa jiji la Dar, Meya atapatikana kutoka Ilala au mojawapo ya Manispaa za hapa,draft (rasimu) ya kubadilisha jiji hili nimeshaletewa na Jaffo nikitoka hapa nakwenda kuisaini ili turahisishe mambo, tuokoe fedha zilizokuwa zinapotea”,alisema Rais Magufuli.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick RAIS

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi