loader
Dstv Habarileo  Mobile
Daraja la Juu la Kijazi lazinduliwa kwa mbwembwe

Daraja la Juu la Kijazi lazinduliwa kwa mbwembwe

RAIS John Magufuli amezindua barabara za juu kwenye makutano ya barabara za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro jijini Dar es Salaam zilizopewa jina la Daraja la Juu la Kijazi.

Rais Magufuli alisema amelipa daraja hilo jina la Kijazi kutambua na kuenzi mchango wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi .

Balozi Kijazi alifariki dunia Februari 17 mwaka huu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alikokuwa amelazwa. Magufuli alisema jana jijini humo kuwa barabara hizo ni alama itakayodumu kwa miaka mingi na kuwa kitambulisho cha jiji la Dar es Salaam.

“Tumepata alama ya pekee ya jiji hili, tuitunze idumu miaka mingi, barabara hizi zinasaidia kuondoa msongamano wa magari kwenye makutano haya, kwa maana sasa unapita moja kwa moja kwenda ama Mwenge, au Kimara, au Buguruni au Posta hakuna tena msongamano,”alisema Rais Magufuli.

Alisema Barabara hizo kuitwa jina la Kijazi limetokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika sekta ya ujenzi na kwamba Kijazi ndiye aliyehangaika na masuala ya ujenzi kwa muda mrefu katika Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kabla ya kumwachia kijiti Mhandisi Patrick Mfugale.

Alisema ujenzi wa barabara hizo umekamilika kwa wakati na kuwapongeza wajenzi wote waliohusika akiwemo wasimamizi wa mradi Tanroads, mkandarasi kampuni ya China ya Ujenzi iitwayo China Engineering Construction Co-operation (CCECC) ambao wametumia miaka mitatu kuutekeleza.

“Niwashukuru wakandarasi hawa, wametekeleza mradi kwa wakati, hawakutoa visingizio, nitoe mwito kwa makandarasi wote nchini hatutaki visingizio vya kutokamilisha miradi kwa wakati kwa sababu zozote ikiwemo corona, hawa wamekamilisha na corona ipo, sasa wasiotekeleza kwa wakati waondoke,älisema Rais Magufuli.

Aliwaagiza watendaji wa wizara ya ujenzi na watendaji wengine wote wanapokwenda kukagua miradi wakikuta mkandarasi anatoa visingizio kwa kutokamilisha mradi kwa wakati aondolewe.

”Barabara zimekamilika hapa pamoja na changamoto za kidunia na lile la Salender, linaendelea na Novemba au Desemba mwaka huu litakamilika, kadhalika ujenzi wa barabara njia nane kwenda Kibaha unaendelea, hatutaki visingivio na mimi niwaombe watendaji wangu wa ngazi zote mkienda kukagua miradi kusiwepo na kisingizio chochote”alisisitiza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Vyombo vya ulinzi na usalama vitunze na Tanroads wafunge kamera katika barabara hizo juu ili wale wavunjao sheria na kufanya uharibifu wabainike na kuchukuliwa hatua haraka, Akizungumzia ujenzi daraja hilo la juu, Mfugale alisema umerahisha usafiri kwani magari 68,800 kwa wakati mmoja na kwamba hivi sasa msongamano haupo .

Mfugale alisema barabara hizo zina uwezo wa kutipisha magari yenye uzito wa tani 180 za magari kwa wakati mmoja na kwamba mradi huo utadumu kwa muda wa miaka 100 na zaidi kutegemeana na matunzo ya miundombinu.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alisema gharama zote za mradi huo ni shilingi bilioni 252.64 na kwamba shilingi bilioni 244 kati ya fedha hizo ni za malipo ya mkandarasi mjenzi na mkandarasi mshauri na Shilingi Bilioni 8.37 zimelipwa fidia ya ardhi kwa wananchi.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi