loader
Dstv Habarileo  Mobile
Madarasa mapya King’ongo yamuokoa Jafo, Kunenge

Madarasa mapya King’ongo yamuokoa Jafo, Kunenge

RAIS John Magufuli amesema kama mazingira katika Shule ya Msingi King’ongo yasingeboreshwa angewatumbua viongozi kadhaa wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo.

Aliyasema hayo jana wakati anazindua Daraja la Juu la Kijazi katika Makutano ya Barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela jijini Dar es Salaam.

Magufuli alisema watendaji wanapaswa kutembelea maeneo kukagua na kutafuta suluhu ya changamoto badala ya kusubiri hadi kero hizo zizungumzwe na wananchi.

“Wabunge na watendaji wote lazima tuwe tunatembelea maeneo yetu na sio kusubiri kuona taarifa mitandaoni, kama ile Shule ya King’ongo, tujipange kutatua kero, nashukuru RC (Mkuu wa Mkoa) wa Dar es Salaam alivamia pale na kuanza kushughulikia, lakini kwa kweli ile shule ingekuwa hadi leo haijajengwa mngekoma, nilitaka kutoa demo, nigeanzia na RC, DC (Mkuu wa Wilaya), Mkurugenzi, sijui Mwenyekiti wa council (baraza) mpaka mwenyekiti wa Kijiji na Waziri” alisema Rais Magufuli.

Alisema viongozi wanapaswa kutatua kero za wananchi kwa sababu ndio waliowachagua na wanataka kuona matokeo ya ahadi zilizotolewa.

“Tunawajibu wa kuwatumikia wananchi huo ndio mkataba wetu kwao, kwa hiyo RC nakushukuru malaika walikugusa ukawahi haraka haraka, nilikuwa nakuangalia, nikasema una bahati kwa sababu mkuu wako wa wilaya alishaanza kulalamika akasema wanatumiwa, sasa wanatumiwa wakati wanaeleza ukweli, kwa hiyo sisi tunawajibu wa kutekeleza yale tunayotakiwa kutekeleza”alisema Rais Magufuli.

Madarasa tisa mapya yamejengwa katika shule hiyo kutekeleza agizo la Rais Maguful alilotoa Januari 18 mwaka huu, alipozungumza na wananchi katika Shule ya Sekondari ya Ihungo mkoani Kagera.

“Namshukuru mwandishi ameitoa kwenye mitandao, viongozi wakaanza kusema ni masuala ya kisiasa, hayo mambo ndio napenda kuyajua, nazungumza nikiwa Kagera nikifika Dar es Salaam niyakute madarasa yamekamilika na wanafunzi hawakai chini, nitakwenda kuitembelea, kama wanasikia `message sent’ (ujumbe umefika),” alisema.

Aliyasema hayo baada ya kuona video iliyokuwa ikionesha wanafunzi wakikaa chini ya miti wakati wakisoma huku mwalimu akitumia daftari kama ubao.

Kadhalika, katika video hiyo iliyosambaswa kwenye mitandao ya kijamii inaonesha uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati na kuonesha baadhi ya wanafunzi waliokuwa darasani wakitumia mifuko maarufu kama viroba kutandika chini ili waweze kuketi kusoma hali iliyomuudhi Rais Magufuli na jamii na akatoa maagizo ya kero hizo kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.

“Kuna shule ipo Dar es Salaam, Ubungo bado wanafunzi wanakaa chini, madarasa mengine yamebomoka, madawati yamevunjika, Mkuu wa Wilaya yupo, Mkuu wa Mkoa yupo, mkurugenzi yupo na Mbunge wa Ubungo yupo tena yupo hapa ni profesa” alisema. Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 2,505 na ujenzi wa madarasa tisa umegharimu shilingi milioni 205 na kila darasa limegharimu shilingi takribani milioni 20.

foto
Mwandishi: Na Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi