loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli asema Ilala ilistahili kuwa jiji

Magufuli asema Ilala ilistahili kuwa jiji

RAIS John Magufuli amesema Manispaa ya Ilala imepandishwa hadhi kuwa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa ina vigezo, hivyo wanastahili, ni haki yao na hawakupendelewa.

Alisema jana kuwa kuanzia sasa aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Omary Kumbilamoto anakuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alitangaza uamuzi wa Rais Magufuli kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuanzia Februari 24 mwaka huu.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la Soko la Kisasa la Kisutu jijini Dar es Salaam, Magufuli alisema Manispaa ya Ilala ina hadhi ya kuwa jiji.

"Manispaa ya Ilala mnastahili, hamkupendelewa, ni haki yenu kwa sababu hata katika mapato mnaongoza. Kwa nini mlinganishwe na manispaa nyingine, na kwa uamuzi huo aliyekuwa Meya wa Ilala ndiye Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na Naibu Meya wake"alisema Rais Magufuli.

Alisema anafahamu kuna watu walikuwa wanaitazama nafasi hiyo ya meya na wengine walishajipanga kugombea. Alisisitiza kuwa hakuna kufanya uchaguzi au kugombea.

"Nyie ndio mabosi wa jiji hili (Dar es Salaam) na nyie ndio mabosi wangu nitakapokuwa nakuja jijini humo, na madiwani wa Manispaaa ya Ilala ndio madiwani wa jiji na bajeti yenu itaongezeka na kuwa kubwa ili itumike kusaidia kutatua changamoto za jiji na maeneo yake yote,"alisema Rais Magufuli.

Jafo alimshukuru Rais Magufuli kwa kuamua hilo. Alisema kuwa juzi hakufahamu kwamba Rais alitoa maelekezo ya kulivunja jiji la Dar es Salaam.

"Nakushuruku Rais Magufuli, jana (juzi) wakati ukiwa Ubungo mimi nilikuwa nakusubiri kule Mbezi Louis stendi, sikujua yaliyojiri, nikapata taarifa kwamba umetoa mchakato wa kufanya jiji jipya na ukanipa maekelezo ya kuvunja jiji na kupandisha Manispaa ya Ilala hadhi kuwa jiji jipya"alisema.

Alisema mara nyingi majiji yanapovunjwa, ugomvi hutokea kwa watu kuanza kugombea mali, hivyo kwa maelekezo ya Rais majengo yote kwenye Manispaa ya Ilala yatabaki kuwa mali ya manispaa hiyo.

"Lakini Rais Magufuli ukasema kama ni rasilimali nyingine kama magari, fedha na kadhalika Tamisemi itatoa mwongozo wa kugawana na kwamba kwa msingi huo mipaka ya jiji la Dar es Salaam itakuwa mipaka ya Wilaya ya Ilala ambayo inahusisha pia bandari, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Ikulu ya Magogoni na maeneo mengine”alisema Jafo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/04c563dca30803f55ef60352bfce0f36.jpg

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameweka jiwe la ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi