loader
Ubalozi Kenya yahimiza diplomasia ya afya

Ubalozi Kenya yahimiza diplomasia ya afya

UBALOZI  wa Kenya nchini umeweka wazi nia yake ya kuongeza ushirikiano na Tanzania katika matibabu ya saratani kwa kuhakikisha diplomasia ya utamaduni na afya  inaimarishwa ikiwamo wananchi wa Kenya kutumia Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kupata huduma.

Balozi wa Kenya nchini,  Balozi Dan Kazungu, alieleza hayo jana alipofanya ziara katika Taasisi ya Saratani Ocean Road akiwa ameambatana na Ofisa wa Ubalozi huo, Dk Rosylne Angola.

Wakati nchi hiyo ikihimiza ushirikiano huo, kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage, alisema idadi ya wagonjwa wanaotoka nchi za jirani ikiwamo Kenya kuja kupata huduma katika taasisi hiyo imeongezeka kutoka wagonjwa 24 mwaka 2017 hadi wagonjwa 128 mwaka 2020.

Katika ziara hiyo, Balozi Kazungu alifanya kikao kifupi cha majadiliano ya kuimarisha ushirikiano na uongozi wa ORCIA pamoja na Dk Mwaiselage, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga za Saratani, Dk Crispin Kahesa na Mkurugenzi wa Mipango, Daudi Maneno.

"Ziara ililenga kubadilishana mawazo ya jinsi ya kuzidi kuboresha ushirikiano mzuri unaofanywa baina ya Serikali ya Kenya na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maeneo mengi ikiwamo sekta ya afya," alisema Dk Mwaiselage.

Mwaiselage alisema serikali kupitia taasisi hiyo imeboresha huduma zake mbali mbali ikiwamo za kuzuia saratani kwa kufanya chanjo za HPV na HBV pamoja na ugunduzi wa dalili za awali.

"Huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia mashine zenye teknolojia ya kisasa ambazo ni sawa na zile zinazopatikana nchi za Ulaya,” alisema na kusisitiza maboresho hayo yameongeza idadi ya wagonjwa kutoka nchi jirani na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kutoka 164 mwaka 2014 hadi wagojwa watatu mwaka 2020.

Alisema katika kikao hicho walijadiliana jinsi ya kushirikiana katika shughuli za kijamii katika taasisi na miongoni mwa shughuli waliyoridhia ni kuboresha mazingira kwa kupanda miti ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Hayati Profesa Wangari Maathai aliyefariki Septemba 25, 2011 kwa saratani ya mlango wa kizazi.

 

Profesa Wangari alitunikiwa nishani ya Nobel kwa jitihada za kutunza mazingira nchini Kenya na Afrika kwa ujumla. Alikuwa ni  mwanamke wa kwanza nchini humo kupata Shahada ya Uzamivu (PhD) na alijikita katika kuhamasisha upandaji miti na utunzaji wa mazingira kupitia mpango wake wa Greenbelt movement.

Alisema shughuli hiyo ya upandaji wa miti imepangwa kufanyika Aprili Mosi, mwaka huu katika viunga vya Taasisi ya Saratani Ocean Road kuadhimisha siku hiyo ambayo pia ni siku ya kuzaliwa hayati Profesa  Maathai.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/92b4c3a2d8cc64781da51b817d39b22a.jpg

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Adam ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi