loader
Dstv Habarileo  Mobile
IGP: Hali ya usalama nchini ni shwari

IGP: Hali ya usalama nchini ni shwari

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),Simon Sirro amesema hali ya usalama wa nchi ni shwari na wahalifu wachache waliokuwa wakisumbua kwenye vitendo vya utekaji barabarani, wote wamekamatwa na wanashughulikuwa na vyombo vya sheria.

Akizungumza jana mbele ya Rais John Magufuli, Sirro alitoa onyo kwa watu ambao wamekuwa wakifungwa jela kwa makosa ya uhalifu wa kutumia silaha na mengine na kisha kutumikia vifungo vyao, lakini baada ya kutoka wanaendelea kutenda uhalifu mitaani na kusema jeshi hilo halitavumilia mtu wa aina hiyo.

Alisema hayo katika hafla ya kufungua majengo ya ofisi, madarasa na bweni la wanafunzi katika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi ambako Sh milioni 799 zimetumika kujenga majengo hayo mawili ya ghorofa.

Akizungumzia hali ya usalama nchini, Sirro alisema zipo changamoto ndogo ikiwamo vitendo vya ubakaji, ambavyo aliomba viongozi wa dini kusaidia vita hiyo.

Sirro alisema vitendo hivyo vipo nchini na kuitaka jamii wakiwemo wazazi na walezi, kufanya uchunguzi wa shule au vituo wanavyowapeleka watoto wao wadogo, kusoma kufahamu mazingira yake kwani baadhi ya maeneo hayo wakiwemo walimu wanahusishwa na vitendo hivyo ya ubakaji.

Akizungumzia wanaorudia kufanya makosa licha ya kufungwa, Kamanda Sirro alisema, “Hatuna tena muhali na wahalifu wanaotumia silaha wala kujihusisha na ugaidi, Watanzania walishasahahu kunyang’anywa fedha zao, sasa tunasema mama mkanye mwanao, mke mtunze mumeo, vinginevyo mtawakosa.

” Rais Magufuli alisema polisi wanao uwezo wa kuwalazimisha watu hao wasiojutia makosa, kuacha uhalifu. “Hao wafungwa wanaotoka vifungoni na kurudi uraiani kama hawajutii makosa yao na wanaendelea kufanya uhalifu, walazimisheni kuacha kwa nguvu, uwezo huo mnao”,alisema .

Kuhusu nidhamu kwa polisi, Kamanda Sirro alisema mwaka 2019 askari 1,055 walishitakiwa kwa makosa mbalimbali na mwaka jana askari wengine 174 walifukuzwa kwa vitendo vya utovu nidhamu. Kwa upande wa makosa ya barabarani, Sirro alisema yamepungua kwa asilimia 33.3 na kwa mwaka wa fedha 2021/22 wanategemea yapungue kwa asilimia 40.

foto
Mwandishi: kunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi