loader
Dstv Habarileo  Mobile
Dk Bashiru Ally ateuliwa Katibu Mkuu Kiongozi

Dk Bashiru Ally ateuliwa Katibu Mkuu Kiongozi

Na Mwandishi Wetu RAIS John Magufuli amemteua Dk Bashiru Ally Kakurwa (pichani) kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Hayo ni kwa mujibu wa taaarifa iliyotolewa na Ikulu kwa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam jana.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Kakurwa alikuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dk Bashiru anachukua nafasi ya Balozi John Kijazi aliyefariki dunia Februari 17 mwaka 2021 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, alikokuwa akipatiwa matibabu. Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua Dk. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Balozi.

Taarifa hiyo ya Ikulu ilisema jana kuwa uteuzi wa Dk. Bashiru, ulianza jana na ataapishwa leo saa 3:00 asubuhi Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Katika Serikali ya Awamu ya Tano iliyoingia madarakani mwaka 2015, Dk Bashiru anakuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa tatu, ambapo wa kwanza alikuwa Balozi Ombeni Sefue aliyefuatiwa na Balozi John Kijazi.

Wengine waliowahi kuwa Makatibu Wakuu Kiongozi tangu tulipopata Uhuru mwaka 1961 ni Dunstan Omari, Joseph Namata, Dickson Nkembo, Timothy Apiyo, Paul Rupia, Marten Lumbanga na Philemon Luhanjo.

Dk Bashiru aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM mwezi Mei mwaka 2018 akichukua kijiti kutoka kwa Abdulrahman Kinana.

Uteuzi wa Dk Bashiru kuwa Katibu Mkuu wa CCM, ulifanyika siku chache baada ya kukabidhi ripoti ya Kamati Iliyochunguza Mali za CCM.

Kamati hiyo iliundwa Desemba 2017 na Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM.

Wajumbe wengine wa Kamati hiyo walikuwa ni Albert Chalamila, Komanya Kitwala, Walter Msigwa, Albert Msando, Galala Wabanhu, William Sarakikya, Mariam Mungula na Dk Fenella Mukangala.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi