WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameziagiza halmashauri zote nchini zenye maeneo ya kumbukumbu za historia ya ukombozi, yatunzwe kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Bashungwa alitoa maagizo hayo mkoani Ruvuma kwenye ziara ya kikazi na juzi alitembelea maeneo ya urithi wa ukombozi wa Afrika katika wilaya ya Tunduru Kata ya Masonya Mkoa wa Ruvuma.
“Natoa maagizo kwa halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma na halmashauri zote nchini, zitunze maeneo haya ya urithi wa ukombozi na mimi nitaenda kila halmashauri kuhakikisha maeneo kama haya tunayatunza na kuyahifadhi,” alisema.
Eneo moja alilolitembelea lilikuwa kambi ya mafunzo ya kijeshi ya wapigania uhuru wa Msumbiji chini ya Samora Machel.
Waziri Bashungwa pia alitembelea nyumba aliyokuwa akifikia Samora Machel na nyumba aliyokuwa akifikia Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Akiwa wilayani hapo, Bashungwa alipokewa na viongozi wa wilaya hiyo na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa wilaya.