Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameagiza utunzwaji wa kumbukumbu za Historia ya Ukombozi kwa Halmashauri zote zenye maeneo hayo hapa nchini.
Bashungwa ametoa agizo hilo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma alipotembelea maeneo ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika na kubainisha kuwa maeneo hayo yanapaswa kutunzwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.
“Naagiza halmashauri zote hapa nchini zitunze maeneo haya ya Urithi wa Ukombozi na nitahakikisha nafika kila halmashauri kwa lengo la kuwahimiza kuyatunza na kuyahifadhi maeneo haya muhimu” amesema Bashungwa.
Maeneo aliyotembelea Waziri huyo ni pamoja na kambi ya wapigania uhuru wa Msumbiji chini ya Samora Machel, nyumba aliyokuwa anafikia kiongozi huyo wa harakati za uhuru pamoja na aliyokuwa anafikia Hayati Julius Kambarage Nyerere kipindi cha harakati za ukombozi mkoani humo.