loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Umeme wa jotoardhi kutumika nchini ifikapo 2025

TANZANIA inatarajia kuanza kutumia umeme wa jotoardhi ifikapo mwaka 2025 huku mikoa 16 ikiwa na maeneo yanayofaa kufua umeme huo.

Meneja wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Kato Kabaka, alibainisha hayo wakati akitoa mada katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kinachofanyika mjini hapa.

Alisema tayari nchi imeanza miradi ya jotoardhi katika maeneo mbalimbali na matarajio ni kuwa ifikapo mwaka 2025 Tanzania izalishe megawati 200 za jotoardhi.

Kwa mujibu wa Kabaka, mikoa yenye maeneo yanayofaa kufua umeme wa jotoardhi ni Arusha, Dodoma, Iringa, Pwani, Kilimanjaro, Kagera, Katavi na Mbeya, Shinyanga, Morogoro, Mara, Rukwa, Singida, Songwe na Tanga.

“Maeneo hayo mengi yanapatikana katika Bonde la Ufa la Afrika Mashariki linalopita hadi Kenya na inaelezwa kuwa katika bonde hilo kuna takriban megawati 15,000 za jotoardhi na wenzetu Kenya tayari wanazalisha megawati 700 za jotoardhi na megawati 800 za umeme,” alisema.

Aliongeza Tanzania inakadiriwa kuwa na megawati 5,000 za jotoardhi.

Kabaka alisema hadi sasa kampuni ya TGDC imeshafanya utafiti zaidi kwenye maeneo ya Songwe, Ngozi - Mbeya, Mbaka Kiejo - Mbeya, Luhoi - Pwani, Ibadakuli - Shinyanga, Kisaki - Morogoro na Natroni - Arusha.

Alisema yapo maeneo yaliyokuwa yamefanyiwa utafiti wa kina na yalikuwa tayari kwa uchorongaji wa visima vya utafiti na uhakiki wa nishati.

Maeneo hayo ni Ngozi, Mbaka - Kiejo na eneo la Songwe. Mradi wa majaribio unaendelea vizuri.

Alitaja matumizi ya moja kwa moja ya nishati ya jotoardhi kuwa ni kupasha moto mitambo viwandani, kupasha joto nyumba na vitalu kwa ajili ya kilimo, kupoza na kugandisha.

Mengine ni kukaushia mazao ya kilimo, kupasha joto maji kwenye mabwawa ya kufugia samaki na ya kuogelea, shughuli za utalii na hutumika kwa tiba.

Kabaka alisema kwa Tanzania, nishati ya jotoardhi ina manufaa mengi na miongoni mwa hayo ni nishati asilia na jadidifu, inapatikana kwa uhakika mkubwa na zaidi, na uzalishaji umeme wa uhakika.

Manufaa mengine ni kupunguza athari mbaya za mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Aidha, hutoa nishati safi na salama kwa kutumia ardhi kidogo, teknolojia iliyothibitishwa kisayansi na inazidi kuimarika.

Nishati ya jotoardhi hutokana na joto litokalo kwenye miamba ya joto likiwa kali na lisilo na ukomo, hali inayoliwezesha kuchemsha maji ya mvua yanayoingia ardhini kupitia mpasuko mbalimbali katika uso wa dunia.

Inaelzwa kuwa, nishati hii ni safi na endelevu ikijulikana kama nishati jadidifu kutokana na kuwa na uwezo wa kutumika tena. Hupatikana chini ya ardhi kwenye kina kirefu, katika miamba ya joto ilioyo chini ya uso wa dunia na chini zaidi katika miamba iliyoyeyuka yenye joto kali iitwayo "magma".

 

 

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi