loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Machinjio ya Vingunguti kufunguliwa Machi

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga amemuelekeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jumanne Shauri kuhakikisha kuwa Machinjio ya Vingunguti inaanza kutoa huduma mapema mwezi Machi mwaka huu.

Nyamhanga alisema hayo jana alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa machinjio hiyo ya kisasa na kubaini ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.

“Kwa kuwa ujenzi wa machinjio hii umeshakamilika kwa kiwango cha kuanza kutoa huduma, sasa inatakiwa kazi zianze hata kwa kuchinja ng’ombe, mbuzi na kondoo wachache mpaka hapo mtakapokamilisha ujenzi kwa asilimia 100,” alisema.

Pia alieleza kuwa machinjio za kisasa zinajengwa katika halmashauri saba nchini, lengo ikiwa kuzijengea uwezo halmashauri ziweze kujitegemea kimapato.

Alitaja maeneo ambayo machinjio hizo zinajengwa kuwa ni Manispaa ya Lindi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Mpanda, Iringa na Halmashauri ya Mji wa Geita.

“Machinjio hii ikianza kutoa huduma itakuwa inakusanya shilingi bilioni mbili mpaka shilingi bilioni tano kwa mwaka, sasa mapato hayo yatawezesha Jiji la Dar es Salaam kupunguza utegemezi kwa Serikali na kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Nyamhanga.

Aliutaka uongozi wa jiji hilo kuanzisha kampuni kwa ajili ya kuendesha Machinjio hayo ya Vingunguti.

Kwa upande wake, Shauri alisema mpaka sasa wameshaajiri wafanyakazi 150 na wameanza mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi miwili sasa ili waweze kuelewa vizuri kazi hiyo, kwa kuwa walitoka kwenye machinjio ya kawaida na sasa wamekuja kwenye machinjio ya kisasa.

“Tumeajiri wafanyakazi 150 na tukaongeza wengine 150, hivyo tutakuwa tumetoa ajira za moja kwa moja 300 na zile zisizo za moja kwa moja 3,000 kwa maana ya wale wanaoleta mifugo, wafanyabiashara wanaochukua nyama kupeleka buchani na wale wanaosafirisha nyama hizo,”  alisema.

Shauri alisema mradi  huo umegharimu Sh bilioni 12.4 kwa kazi za ndani na za nje pamoja na kufunga mitambo yote. Alisema kuwa machinjio hiyo itafanya kazi kisasa na itatengeneza sausage na nyama ya kusaga.

Meneja wa Ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti, Mburuga Matamwe alisema mradi umekamilika kwa asilimia 98 kwa kazi za ndani na za nje. Alieleza kuwa machinjio hiyo ina uwezo wa kuchinja ngombe 1,500 na mbuzi na kondooo 3,000 kwa siku.

JOPO la Majaji 12 nchini Marekani limemtia hatiani ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi