loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bashungwa aziandikia taasisi utekelezaji agizo la JPM

Bashungwa aziandikia taasisi utekelezaji agizo la JPM

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeziandikia barua wizara, idara, taasisi na mashirika ya umma kuziagiza kutekeleza mara moja agizo la Rais John Magufuli la kutoa taarifa kwa umma kuhusu shughuli wanazofanya.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Hassan Abbasi alisema hayo jana mjini hapa wakati akifanya wasilisho katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Dk Abbasi ameeleza kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameandika barua hizo juzi na zimeshatumwa kwa taasisi hizo za umma kwa utekelezaji.

"Jana (juzi) waziri ameandika barua na tumezituma kwa wizara na taasisi zote za umma kutekeleza agizo la Rais Magufuli. Tumeagiza wataalamu wa mawasiliano kwa namna zao watoe taarifa hizo," alisema Dk Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali.

Akizindua Jengo la Jitegemee lenye kituo cha televisheni na redio mali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dar es Salaam, Rais Magufuli aliagiza kutolewa kwa taarifa zinazohusu serikali bila kikwazo huku akisisitiza waandishi wawe wazalendo kwa nchi yao.

Dk Abbasi alisema kuanzia sasa wataanza kufanya tathimini ya utoaji wa taarifa, na katika hilo ameagiza Jukwaa la Wahariri Tanzania na waandishi wa habari, kumpa taarifa ya taasisi zinazoficha taarifa

Lakini pia aliwataka wanahabari kueleza pia taasisi za umma, zinazofanya vizuri katika utoaji wa taatifa.

Na katika hilo, aliipongeza Tanesco akisema ni moja ya taasisi za umma inayotoa habari bila kificho na imekuwa ikitangaza shughuli zake kwa kina.

Akifafanua,  alisema utoaji wa taarifa za serikali ni muhimu kwa sababu za kimkakati, lakini pia zinawezesha serikali kuaminika kwa wananchi.

Aidha, alisema utoaji taarifa umesisitizwa katika mikataba ya kimataifa pamoja na Katiba ya Tanzania na sheria, zikiwamo Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya 2016 na Sheria ya Huduma za Habari ya 2016.

Aliwahimiza watendaji wa serikali, kuacha kuficha au kutotoa taarifa, kwani hilo ni takwa la kisheria na siyo utashi wao.

Kwa wanahabari, Dk Abbasi aliwataka kutoa taarifa kwa usahihi na umakini na pia kutanguliza mbele uzalendo.

"Mwandishi mzuri ni yule anayefanya kazi kwa utafiti na usahihi akiweka umakini. Tuache kufakamia mawazo na nadharia za watu wa nje ambao wanasema bila utafiti," alisema Dk Abbasi.

Aliwataka waandishi kutoona haya kutangaza na kupongeza mazuri ya serikali, akitoa mfano wa ujenzi wa Mradi mkubwa wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, ambao una manufaa makubwa ikiwamo kumaliza mgawo wa umeme nchini ambao huko nyuma vyombo vya habari viliripoti sana.

Awali, akifungua kikao kazi hicho cha siku mbili, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani aliwataka wanahabari wanapoandika habari zao kuzingatia mambo matatu, kasi, ubunifu na usahihi.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Morogoro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi