loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bashiru: Niombee nikidhi matarajio ya Rais

Bashiru: Niombee nikidhi matarajio ya Rais

KATIBU Mkuu Kiongozi, Dk Bashiru Ally amewaomba Watanzania kumuombea atekeleze majukumu yake, kama yalivyo matarajio ya  Rais John Magufuli.

Akizungumza baada ya kuapishwa jana kushika wadhifa, Bashiru alimshukuru Rais Magufuli kwa imani kubwa aliyoionesha kwake kwa kumteua katika wadhifa huo mkubwa.

Dk Bashiru ambeye pia ameteuliwa kuwa Balozi, aliapishwa Ikulu Dar es Salaam katika hafla  iliyohudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, mawaziri na viongozi mbalimbali wa chama na serikali.

Alimshukuru rais kwa imani aliyonayo kwake, kwa kuwa hiyo ni mara pili kumteua kwa ajili ya kutumikia taifa. Mara ya kwanza  alimteua kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mei 2018 na juzi  alimteua kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi.

Kwa mujibu wa Bashiru, Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, alimpa kazi za mwezi mzima ambazo alitakiwa kuzianza muda wowote kuanzia sasa akiwa Katibu Mkuu wa Chama, lakini juzi wakati akiendelea kupitia mafaili yake, alipata taarifa ya uteuzi wake kupitia mitandao ya kijamii.

“Mshituko wa taarifa hiyo hauniwezeshi niseme mengi, bado natafakari sana nitafanya nini au nitafanya vipi kukidhi matarajio yako kwa imani uliyonipa kwa mfululizo. Niwaombe Watanzania wote mniombee ili niweze kukidhi matarajio ya Mheshimiwa Rais,”alisema  Dk Bashiru.

Aliongeza, “Lakini jambo la pili ni mila, maadili na miiko ya kazi hii ambayo upande mmoja ni Balozi na upande mwingine ni Katibu Mkuu Kiongozi. Hizi si kazi za maneno bali ni kazi za kusikiliza, kujifunza, kuchambua, kuamua na kutenda, kwa hiyo nitakuwa nazungumza kwa tahadhari na umakini, nakuahidi Mheshimiwa Rais sitakuangusha.”

Aliwashukuru pia viongozi wakuu wa Serikali, Bunge, Mahakama na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Kamati Kuu na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ambao kwa pamoja walimpa ushirikiano mkubwa katika nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM.

Aliahidi kusimamia mambo muhimu ikiwamo mawasiliano ndani ya Serikali na kati ya umma, uzalendo, uadilifu na utumishi kwa wananchi pamoja na kusimamia haki na wajibu.

Katibu Mkuu Kiongozi alisema mambo hayo matatu, atayasimamia kwa karibu zaidi kwa kuwa ndiyo mambo ambayo Rais Magufuli amekuwa akiyasisitiza mara nyingi hata katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu jijini Dar es Salaam aliyohitimisha juzi.

Dk Bashiru alisema atahakikisha mawasiliano ndani ya serikali na mawasiliano kati ya serikali na umma, yanasimamiwa vizuri ili ifanye kazi kama timu moja kupitia utumishi wa umma lakini pia idara, taasisi, wizara.

Alisema atahakikisha mamlaka mbalimbali serikalini, zinatoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa wananchi wajue mambo yanayofanywa na serikali yao.

Jambo la pili ambalo aliahidi kulisimamia kwa karibu ni umuhimu wa uzalendo, uadilifu na utumishi kwa wananchi hasa katika kutatua kero zao. “Mheshimiwa Rais nakuahidi hili nitalisimamia kwa sababu wewe pia umelisimamia kwa nguvu zote,”alisema.

Jambo la tatu ambalo aliahidi ni kusimamia haki na kusisitiza wajibu wa kila mmoja wao.

Alisema atahakikisha kila uamuzi unaofanywa na vyombo husika, unazingatia haki hususani za wanyonge ikiwamo ushuru, kodi na tozo mbalimbali kwa kuhakikisha misingi ya kisheria na haki inazingatiwa pamoja na kusimamia uwajibikaji ili Taifa lipige hatua ya kutosha ya kimaendeleo.

Kuhusu mtangulizi wake, Balozi John Kijazi aliyefariki hivi karibuni, Dk Bashiru alisema ameliachia taifa hazina kubwa ya tabia njema, uungwana, uchapakazi na upole.

Alisema hawezi kuahidi kwamba atakuwa kama Balozi Kijazi, lakini anamuomba Mwenyezi Mungu ayaendeleze aliyoyafanya wakati wa uongozi wake.

Akizungumza kwa niaba ya Spika Job Ndugai, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, alimpongeza Dk Bashiru na kumhakikishia ushirikiano wa Bunge.

Dk Tulia alisema ushirikiano waliopata kutoka kwa Balozi Kijazi wanautarajia pia kutoka kwa Bashiru, awe kiungo kati ya Serikali na Bunge kwa kuwa mambo mengi kabla hayajapelekwa bungeni yanapita mikononi mwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Jaji Mkuu wa Tanzania,  Profesa Ibrahim Juma, alisema anamfahamu  Dk Bashiru kwa muda mrefu lakini pia ni mwanafunzi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, mwanafunzi wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, mwanafunzi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mwanafunzi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete na pia ni mwanafunzi wa Rais Magufuli.

Profesa Juma alisema Mahakama inategemea  watumishi wa umma,  kwa kuwa soko lao linatoka Serikali Kuu na wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Utumishi na Katibu Mkuu Kiongozi.

Alimuomba Katibu Mkuu Kiongozi, kutembelea Mahakama kuona maboresho yanayofanyika kwa kuwa akiyaelewa maboresho hayo, atawasaidia kwa upande wa serikali kwa sababu wawezeshaji wa maboresho ya mahakama ni Serikali na Bunge.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi